Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CCM Z'bar wasusa mjadala wa mafuta

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAWAKILISHI wa CCM jana walisusa kuchangia sera ya nishati visiwani hapa iliyowasilishwa kwenye Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yusuf Himid.

Sera hiyo iliwasilishwa juzi usiku na kumlazimisha spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kuahirishwa kikao hicho ili kutoa nafasi kwa wajumbe kuipitia kwa kina kwa lengo la kutoa mchango madhubuti na yenye manufaa kwa Zanzibar.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba sera hiyo, iliyokuwa ikisubiriwa na wajumbe wa pande zote mbili, haikuchangiwa kwa uchangamfu kama ilivyotarajiwa kutokana na suala hilo kuzua mjadala mkubwa visiwani hapa.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliwahi kutaka iundwe sera na kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ili Zanzibar iwe na shirika lake la mafuta na kuondokana na kuchangia suala hilo na Bara, lakini hali haikuwa hivyo juzi.

Suala la mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa mambo yaliyowaunganisha Wazanzibari, hasa wa vyama vya CCM na CUF ambao wamekuwa na historia ya kuhasimiana kisiasa kwa zaidi ya miaka 10.

Katika vikao vya baraza hilo mwaka jana, wawakilishi hao walikuwa wakizungumza lugha moja kuwa suala la mafuta liondolewe kwenye mambo ya Muungano, na hata baada ya mshauri wa kitaalamu kueleza kuwa uwezekano wa kupatikana mafuta ni mdogo, walisema watagawana hata kama yakijaa kwenye glasi.

Lakini picha iliyoonekana jana inazua maswali kwenye mshikamano wa Wazanzibari ulioimarishwa na kitendo cha viongozi wawili visiwani humo, Rais Amani Abeid Karume na Seif Sharrif Hamad kukutana mwishoni mwa mwaka jana.

Suala jingine lililowaunganisha CUF na CCM ni juu ya hoja ya utaifa wa Zanzibar ambalo lilipamba moto baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza bayana kuwa Zanzibar si nchi.

Wawakilishi waliochangia sera ya nishati ambayo ilianza kujadiliwa jana asubuhi ni 10 kutoka CUF, lakini ni wawakilishi wawili tu kutoka CCM ambao walichangia hoja hiyo. Katika baraza hilo CCM ina wajumbe 52 na CUF 26.

Wajumbe waliochangia wote waliunga mkono hoja ya suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika mambo ya Muungano.

Waliochangia kutoka CCM ni Ali Denge Makame, ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Amani na Haji Sukeimani Haji, ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Kwahani.

Wajumbe wengi wa CCM walikuwa nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakizungumza na watu wengine.

Jana asubuhi kikao hicho kilikuwa kinaongozwa na Spika Kificho, ambaye majira ya saa 5:00 baada ya kipindi cha maswali na majibu,alionekana kushangazwa kuona ukumbi ukiwa na wajumbe wachache.

Mara kwa mara Pandu aliwataka wawakilishi waingie ndani ili kujadili hoja iliyokuwa mbele yao, lakini ni wachache waliotiia amri hiyo.

"Mheshimiwa Mansoor nakuomba uingie ndani kwa sababu tunataka tuendelee na mjadala,"alisema Kificho na muda mfupi baadaye waziri huyo aliingia ndani na kuomba radhi kwa wajumbe akisema alienda kujiweka sawa kwa matayarisho ya kusikiliza michango ya wajumbe.

Wakati huohuo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameonekana wakinong'ona ya hapa na pale kutokana na hoja binafsi inayotarajiwa kuwasilishwa na kiongozi wa upinzani, Abubakar Hamis Bakari wiki hii juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.

Juzi kamati kuu ya CCM Zanzibar iliunga mkono kwa kauli moja hoja hiyo binafsi lakini pembeni baadhi ya wajumbe walionekana kutofautiana.
Tags:

0 comments

Post a Comment