IKULU ya Zambia imeagiza kuhamishwa kwa nyani wapatao 200 kutoka kwenye viunga vya eneo hilo, baada ya mmoja wao kumkojelea Rais Rupia Banda.
Tukio hilo lilitokea mapema mwezi Juni, wakati Rais Banda akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na Wanadipolmasia, eneo la nje ya Ikulu.
Kwa mujibu wa wa gazeti la The Post (The Post Newspaper) la Zambia, baada ya tukio hilo Rais Banda alisikika kwa lugha yao ya Nyanja akisema kwa mstuko, : "Ahaa...kanitundila (yaani kanikojolea)," hali iliyofanya watu wote waliokuwepo kwenye mkutano huo kuangalia juu ya mti kuona nyani huyo aliyefanya kitendo cha utovu wa nidhamu.
Gazeti hilo lilifafanua kwamba, Rais Banda baadaye alimwagiza Mtaalamu wa Taasisi ya Wanyama kwenye Bustani hiyo ya Ikulu Munda Wanga, kuwaondoa nyani hao.
Katika zoezi hilo la hamisha hamisha wanyama hao, gazeti hilo lilisema zilitumika jumla ya dola za Marekani 50,000 sawa na zaidi ya Sh 70 milioni za Tanzania.
“…Rais alitaka baadhi ya nyani hao kupelekwa maeneo mengine kutoka makazi ya watu na kurejeshwa porini,"alifafanua Meneja Masoko Fred Hengeveld, kutoka Taasisi ya Wanyama ya Munda.
Gazeti la The Post lilifanua kwamba, katika zoezi hilo jumla ya nyani wapatao 61 walikamatwa na kuondolewa viunga vya Ikulu hiyo.
Tukio hilo la kusisimua ambalo lilitokea Juni 24 wakati Rais Banda akizungumza na waandishi na wana diplomasia hao huku kima hao wakiwa juu ya mti, limeshangaza wananchi wengi wa Zambia kwani ni la kwanza kuwahi kutokea maeneo ya Ikulu tangu marais mbalimbali waliopita kuitisha mikutano kwenye viunga hivyo.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani wamekuwa kete hiyo ya kima kama hatua ya kumdhihaki kiongozi huyo mkuu wa nchi kutokana na kitendo hicho cha 'kutundilwa' na nyani.
Rais Banda aliingia madarakani mapema mwaka huu baada ya kifo cha Rais Levy Mwanawasa, ambaye alifariki kutokana na ugonjwa wa Kiharusi nchini Ufaransa.
0 comments