HALI ya kisiasa ndani ya Chadema imezidi kuchafuka baada ya uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha) kuahirishwa kwa miezi sita, huku mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo (jina tunalo) akitishia kumchoma kisu mwanachama anayeaminika kuwa kambi ya naibu katibu mkuu, Zitto Kabwe.
Wakati hatma ya uchaguzi huo ikiwa bado njia panda, mizengwe imezidi kutikisa uchaguzi wa Jumuiya ya Wanawake baada ya mmoja wa wagombea anayeaminika kuwa upande wa Zitto kunusuruka kung'olewa.
Joto zaidi linaloonyesha hali tete ndani ya Chadema, lilipandishwa na hatua iliyotangazwa jana mchana na katibu mkuu, Dk Wilbrod Slaa ya kuahirisha uchaguzi huo hatua ambayo ilipingwa na Zitto na msemaji wa chama hicho David Kafulila ambao wanataka kutangazwa kwanza kwa matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika juzi na kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC), ambacho inasemekana kinafanyika leo.
Wagombea waliokuwa wakiwania nafasi ya uenyekiti wa Bavicha ni John Heche, Dadi Igogo na David Kafulila ambaye licha ya kuwa ofisa habari wa chama hicho, anatarajiwa kuwania ubunge Jimbo la Kigoma Kusini mwaka 2010.
Akitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo jana, Dk Willibrod Slaa alisema uchaguzi huo utafanyika ndani ya miezi sita ijayo.
“Mimi kama katibu nimeshauriana na kamati ya wazee ya chama nikiongozwa na Mzee (Edwin) Mtei, Bob Makani na Balozi (Christopher) Ngaiza tumeubatilisha uchaguzi huo, hivyo utafanyika ndani ya miezi sita ijayo,” alisema Slaa.
“Tumeamua hivi kwa sababu kwanza kufanya uchaguzi ni gharama, tunatumia karibia Sh50 milioni ambazo zinaweza kujenga zahanati moja. Jamani hapa tutawaeleza nini Watanzania.
“Wajumbe walidai kuwa uchaguzi ulijaa rushwa, lakini niliwambia waandike malalamiko kwa maandishi na ujumbe mfupi na wamenipatia nitayafanyia kazi na yatatolewa maamuzi na vyombo husika.”
Lakini Zitto alipinga uamuzi huo akisema katibu mkuu hana mamlaka ya kutoa tangazo hilo na kwamba nanlaka hayo ni Kamati Kuu (CC).
"Lakini pia, chombo pekee chenye uwezo wa kufanya uamuzi huo ni Kamati Kuu, sasa inakuaje chombo kingine kichukue uamuzi tena bila matokeo kutangazwa wala mgombea kukata rufaa," alisema Zitto.
Alifafanua kuwa uamuzi huo umetokana na baadhi ya watu kukataa matokeo hayo baada ya kuweka mbele maslahi binafsi badala ya maslahi ya chama kwa kuwa jambo la msingi katika suala hilo ni matokeo hayo kutangazwa kwanza kabla ya kuahirisha uchaguzi.
"Jambo la kwanza ni kutangaza matokeo na baadaye kama kuna mgombea alikuwa akipinga, anaweza kukata rufaa, lakini matokeo hayajatangazwa wala hakuna aliyekata rufaa," alifafanua Zitto.
Kutokana na utashi wa katiba, Zitto alisema tayari amemwomba katibu mkuu kuitisha mkutano wa CC kujadili suala hilo.
"Nimemwomba Dk Slaa aitishe kikao cha Kamati Kuu tujadili hii hali maana kama viongozi hatutakuwa na busara na chama kitavurugika," alionya.
Alipoulizwa nini mustakabali wa Chadema kutokana na matukio hayo ya vurugu yanayotikisa chama, alijibu: "Viongozi tusipotumia busara chama kitavurugika, lakini tukitumia busara na kuweka maslahi ya chama mbele, tutaweza kutatua haya mambo kwa urahisi."
Zitto alihoji: "Kwanini wazee wasitumie busara kama walizotumia kuniomba mimi nijitoe kwa kutaka wagombea wengine wajitoe au wakubali matokeo kwa kumwachia Kafulila?
"Tukiwa na busara; tukiheshimu demokrasia, tutaweza kuvuka salama. Naamini hilo tu ndiyo suluhisho la kukivusha chama salama."
Naye Kafulila alipinga uamuzi wa kuahirisha uchaguzi kabla ya kutangaza matokeo akisema anataka kutangazwa kwanza kwa matokeo ambayo anaamini, yalimpa ushindi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kafulila alisema haoni sababu ya kutotangazwa kwa matokeo hayo ambayo anaamini alishinda licha ya kutokubalika na sehemu kubwa ya wajumbe wa sekretarieti na wabunge wa viti maalum.
"Ukiangalia hata hayo mambo ya karatasi kuongezeka, utaona labda ulikuwa ni mpango maalumu wa kumwangusha mtu fulani, lakini imeshindikana," aliongeza.
"Kwa kifupi, sikubaliani na uamuzi huo ninachotaka kwanza matokeo yatangazwe na pia baraza halina mamlaka hayo. Hiyo ni kazi ya Kamati Kuu."
Habari zinadai kuwa tangu John Mnyika kuondoka kwenye wadhifa wa uenyekiti wa vijana wa Chadema, kumekuwa na mkakati wa kumdhibiti Kafulila unaofanywa na baadhi ya vigogo wa Chadema kutokana na mgombea huyo kuonekana mwiba kwao.
Kafulila anasemekana kuwa ni mtu anayepinga waziwazi mambo yanayoendeshwa kinyume na taratibu na amekuwa hahofii viongozi wa juu yake kueleza msimamo wake.
Wakati hayo yakiendelea, vurugu zaidi zimezidi kutikisa chama hicho na jana zilifikia katika hatua ya mgombea mmoja wa nafasi ya uenyekiti wa vijana kutaka kumchoma kisu mwanachama ambaye alikuwa akimtetea Zitto Kabwe asitukanwe na mgombea huyo.
Kabla ya kufikia hatua ya kutishiana visu, mgombea huyo alikuwa akibishana na baadhi ya wafuasi wa Kafulila kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema zilizo Kinondoni jijini Dar es salaam.
Wakati Mwananchi inafika kwenye ofisi hizo majira ya saa 7:00, vurugu zilikuwa zimeshapoa tangu saa 5:00, lakini wanachama walikuwa wamekaa kwenye vikundi wakijadili matukio mbalimbali ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mgombea huyo na mwanachama mmoja anayedaiwa kuwa anamuunga mkono Kafulila, walirushiana ngumi kwanza na baadaye ndipo mgombea huyo alipotoa kisu na kumtishia.
Mashuhuda hao walidai kwamba mara baada ya mgombea huyo kutoa kisu, wanachama wengine waliokuwa karibu waliingilia kati na kumtoa eneo hilo.
Mwanachama anayedaiwa kutishiwa kisu aliiambia Mwananchi kuwa alikuwa akimsihi mgombea huyo kuacha kumsema vibaya Zitto kwa kuwa malalamiko yote ya uchaguzi wa juzi yako ngazi za juu za chama hicho.
Mwanachama huyo alifafanua kwamba baada ya kumwambia mgombea huyo maneno hayo, alipandisha ghadhabu zaidi na kuanza kutukana.
“Sasa mimi nilivyoona anamtukana Zitto, nilimwambia aache lakini hakusikia; alikuwa anasema Zitto wako na Kafulila walishirikiana kumwibia kura. Kutokana na kuendelea kuongea ovyo, tulishikana na alivyoona muziki ni mnene alinitolea kisu na kutaka kunichoma,” alidai.
Katika hatua nyingine, Dk Slaa juzi alilazimika kurudi katika ukumbi wa uchaguzi wa Bavicha mnamo saa 6:20 usiku ili kutuliza ghasia zilizoibuliwa na wajumbe mara baada ya kupata habari kuwa kura 20 ziliongezeka katika nafasi ya mwenyekiti.
Wajumbe hao ambao walionekana kuwa upande wa mgombea wa nafasi hiyo, John Heche ambaye ni diwani wa Tarime Mjini, walipinga matokeo kabla hayajatangazwa hali iliyomlazimu msimamizi wa uchaguzi huo, Charles Mwera, ambaye pia ni mbunge wa Tarime, kutoyatangaza.
Dk Slaa, ambaye aliondoka kwenye ukumbi huo juzi saa 7:00 mchana, alirejea kwa mara ya pili saa 6:20 usiku, vurugu zikiendelea baada ya Heche kumpiga ngumi mbili ofisa wa kurugenzi ya uchaguzi ya Chadema, Ali Chitandana na kumlazimu kufanya kazi kubwa kuzituliza.
“Jamani wajumbe nawaomba muwe watulivu kila kitu kilichotokea nimepewa taarifa na Mnyika, kwa hiyo kama kuna mtu ana malalamiko ayaandike na kuyawasilisha makao makuu ya chama kesho (jana) asubuhi ili niyafanyie kazi,” alisema Dk Slaa.
Katika hatua nyingine, wajumbe hao walimweleza wazi Dk Slaa kuwa hawajalipwa fedha zao za posho hali iliyomlazimu katibu huyo mkuu kumwagiza Mtunza Fedha kuwalipa wajumbe hao kutoka mikoa mbalimbali nchini usiku huohuo.
“Wewe Mtunza Fedha walipe wajumbe posho zao; jamani nimeshamwagiza atawalipa wote ila wale ambao wameshakata tiketi kwa ajili ya kusafiri watarudishiwa fedha zao kesho (jana) kwa sababu hamuwezi kuondoka kwa kuwa uchaguzi huu unaweza kurudiwa, lakini yote yatajulikana mara baada ya viongozi kukutana,” alisema Dk Slaa.
“Kwa kweli, nimesikitika sana hiki kitendo kilichotokea leo ni aibu kwa chama. Hapa wapinzani na magazeti yatapata pa kusemea.
Hiki chama ni cha demokrasia; nahitaji kujua kila kitu kilichotokea ili vifanyiwe maamuzi na yeyote atakayebainika kuhusika kwa namna moja au nyingine atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa katiba ya chama.”
Habari hii imeandikwa na Ramadhan Semtawa, Fidelis Butahe, Musa Mkama na Fred Azzah
0 comments