Iran yafanikiwa kutengeza nishati ya nuklia
Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku moja baada ya Iran kutangaza kuwa imepiga hatua muhimu katika mpango wake wa nuklia unaozua utata.Marekani kwa upande wake imelishuku tangazo hilo lililotolewa katika ufunguzi wa kituo kimoja cha nuklia mjini Isfahan.Ikumbukwe kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tayari limeiwekea Iran awamu tatu ya vikwazo baada ya kukaidi amri ya kusitisha mpango wake wa nuklia.
Ufunguzi wa kiwanda hicho cha kutengeza nishati ya nuklia unaashiria kuwa Iran imehitimisha mzunguko maalum wa nuklia unaoanzia katika uchimbaji wa madini ya uranium hadi urutubishaji wake.Katika ufunguzi rasmi wa kituo cha Isfahan Rais Mahmoud Ahmedinejad aliisifia hatua hiyo.
''Iran imeimarisha mpango wake wa nuklia na kupiga hatua mbili muhimu…mosi ni kutengeza nishati ya nuklia na pili ni kufanya majaribio ya aini mbili ya vinu vya nuklia vilivyo na uwezo mkubwa wa kurutubisha madini ya uranium.''
Kiwanda cha kurutubisha uranium cha Bushehr Wakati huohuo Rais Mahmoud Ahmedinejad alisisitiza kuwa nchi yake iko tayari kufanya majadiliano na mataifa ya magharibi kuhusu suala la nuklia.Kwa mujibu wa kiongozi wa Shirika la Nishati ya Atomiki nchini Iran Gholam-Reza Aqazadeh nchi hiyo imeongeza jumla ya vinu alfu moja vipya vya nuklia katika kiwanda chake cha Natanza cha kurutubisha madini ya uranium.Kwa sasa idadi kamili ya vinu vya nuklia nchini humo imefikia alfu 7.Kituo hicho kina uwezo wa kutengeza tani kumi za nishati ya nuklia itakayotumika katika vinu vya nuklia kama kile cha Bushehr.Kinu hicho sharti kitimize masharti ya kiteknolojia ya Kirusi kwasababu kilitengezwa na Urusi na itakayokisimamia katika awamu za mwanzo.
Itakumbukwa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Atomiki IAEA liliripoti kwamba vinu hivyo alfu 7 vimezidi kwa 1500 kiwango ilichokitangaza majuma sita yaliyopita.
Kufuatia tamko hilo Marekani ilitangaza kuwa iko tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Iran hususan katika suala la nuklia.Ifahamike kuwa hatua hii ni kinyume na ilivyokuwa wakati wa utawala wa George W Bush.Chini ya uongozi wa Rais Obama Marekani imebadili sera zake za kigeni na kuinyoshea mkono Iran.Kulingana na msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani Robert Wood ni jambo la msingi kujadiliana na Iran.
''Tuko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Iran.Kwahiyo kuna masuali mengi yanayogubika suala hili la mpango wa nuklia wa Iran ambayo yanahitaji kushughulikiwa.Ikiwa Iran itaweza kuchukua hatua hiyo bila shaka sote tutapata ahueni.''
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Hilary Clinton Marekani imechukua uamuzi huo ili kuweza kuthibitisha iwapo madai hayo ya Iran ni ya kweli.Mataifa ya magharibi yamekuwa yakiilaumu Iran kutaka kutengeza silaha za nuklia dai inalokanusha.Iran kwa upande wake inashikilia kuwa lengo lake ni kutengeza nishati ya nuklia.Marekani inapanga kujiunga na kundi la mataifa manne wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani katika majadiliano ya mpango wa nuklia ya Iran.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kwa upande wake ameipongeza hatua hiyo ya Marekani na kutoa wito wa suluhu kupatikana haraka chini ya misingi ya Baraza la Usalama.Baraza hilo tayari limeshaiwekea Iran awamu tatu ya vikwazo baada ya kukaidi amri ya kusitisha mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium.Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran amesisitiza kuwa nchi yake haitaki kuendeleza uhasama.Wiki iliyopita Iran ilipokea kwa mikono miwili pendekezo la Rais Obama alipokuwa mjini Prague nchini Czech la kusitisha matumizi ya silaha za nuklia uliwenguni kadhalika kusimamisha majaribio ya nuklia.
Mkuu wa Sera za kigeni wa EU Javier Solana, (Kushoto) na msuluhishi wa Iran Saeed Jalili Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana anatazamiwa kuwasiliana na msuluhishi mkuu wa mzozo wa nuklia wa Iran Saaid Jalili kwa lengo la kuandaa mkutano ujao utakaojadili suala hilo.
DPAE/AFPE
0 comments