You Are Here: Home - - Chuo Kikuu Dar chafungwa
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
*Wanafunzi wote shahada ya kwanza watimuliwa *Kisa ni sakata la mikopo, sera ya kuchangia elimu Na Hilary Komba CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimefungwa kwa muda usiojulikana kuanzaia jana kutokana na mgomo uliofanywa kwa muda wa siku tatu na wanafunzi wa shahada za kwanza waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuondoa sera inayowataka wanafunzi kuchangia elimu ya juu. Akizungumza jana Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Yunus Mgaya alisema Chuo kimelazimika kufungwa baada ya kuona wanafunzi wanaendelea kufanya mgomo kinyume na taratibu na kuhatalisha amani chuoni hapo. Alisema wanafunzi walianza kufanya mogomo tangu Jumatatu wiki hii wakishinikiza Serikali kutoa mikopo kwa asilimia 100 jambo ambalo walikwishaambiwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe kuwa linashughulikiwa. "Tumeamua kukifunga chuo kwa muda usiojulikana kutokana na wanafunzi kukiuka sheria ndondogo za hasa kanuni ya namba 4 yenye vifungu vidogo tisa ili kunusuru hali iliyokuwa ikihatalisha amani chuoni hapa," alisema Profesa Mgaya. Alisema uamuzi wa kukifunga chuo ulitokana na kikao cha 144 cha Baraza la Chuo kilichofanyika Novemba 9 wiki iliyopita kilichoutaka uongozi wa chuo kuhakikisha wanafunzi wanafuata sheria za chuo la sivyo hatua zichukuliwe. Alisema pia Profesa Maghembe alikutana na viongozi wa wanafunzi tarehe juzi akiwataka kuacha mgomo na kuingia darasani kusoma lakini hawakufanya hivyo. Profesa Mgaya aliongeza kuwa pamoja na kupewa ushauri huo jana wanafunzi hao waliendelea kufanya mgomo na uongozi ukalazimika kutoa tangazo chuoni hapo lililosaniniwa na Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Rwekaza Mukandala likiwataka wanafunzi wa shahada ya kwanza kuondoka haraka baada ya chuo kufungwa. Alisema uamuzi huo hautawaathiri wanafunzi wa kozi fupifupi, shahada ya pili, ya tatu na wale wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa kuwa wao hawakushiriki mgomo huo. Alisema pia Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Changombe (DUCE) pamoja na kushiriki kwao awali katika mgomo huo hawataathirika na uamuzi huo kwa kuwa wao wanaongozwa na Bodi nyingine. Sakati hilo lina mizizi kuanzia miaka ya awali ya 1990 ambapo Serikali iliamua kuasisi sera ya kuchangia elimu ya juu ambayo hata hivyo ilipingwa na wadau wengi. Mwaka 2005 Bunge lilipitisha Sheria ya Kuunda Bodi ya Mikopo katika utekelezaji wa sera hiyo lakini wanafunzi wa vyuo vikuu wakiongozwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walifanya mgomo mkubwa uliosababisha Chuo kufungwa kwa muda usiojulikana wakipinga sheria hiyo. Hata hivyo baada ya chuo kufunguliwa uliibuka mgogoro mwingine mkubwa, lakini kwa kuwa mwaka huo ulikuwa wa uchahuzi, wachunguzi wa mambo wanasema Serikali ilisukumwa kulegeza masharti kwa kutoa mikopo kwa asilimia 100 kwa kila mwanafunzi. Mtazamo wa wanafunzi wa elimu ya juu umekuwa kwamba mikopo hiyo inaonekana kuwatenga maskini kwa sababu bado wanapokosa, kupitia tathmini zinazofanyika, ufadhili wa asilimia 100 na kutakiwa kuchangia asimilia inayobaki wengi huapata matatizo. Hoja nyingine ya wanafunzi ambayo ingawa haijitokezi sana ni kupinga msingi mzima wa mikopo wakidai imekuja kubatilisha msingi mzuri wa Serikali kusomesha wasomi wa vyuo vikuu ulioasisiwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wasomiu wengi wa vyuo vikuu wanahoji kwa nini sera ya kuchangia ianze mwaka 1994?Wakati ambapo karibu viongozi wote waandamizi Serikalini huko nyuma walishasomeshwa bure? Mtazamo wa Serikali umekuwa kwamba sera ya kuchangia elimu ni mwendelezo wa sera za kuchangia huduma za kijamii kama vile afya na maji. Serikali imekuwa ikijenga hoja kuwa kutokana na matakwa ya wakati ya kusomesha wanafunzi wengi zaidi tofauti na ilivyokuwa zamani, hivi sasa si rahisi kugharamia idadi kubwa ya wanafunzi walioko vyuo vya elimu ya juu kwa sababu ya gharama kubwa-Wanafunzi wa sasa ni wengi maradufu ya zama za Mwalimu na hata gharama zimeongezeka zaidi ya maradufu. Lakini Serikali pia inajivunia sera hiyo ya uchangiaji ikisema wale wenye uwezo wamejisomesha au kusaidiwa kidogo wakati wale maskini wamekuwa wakigharamiwa kwa asilimia 100. Serikali inaegama katika hoja kwamba kusomesha wanafunzi wote walioko sasa katika vyuo vya elimu ya juu kwa kiwango cha asilimia 100 kama wanavyotaka wanafunzi hao ni sawa na kusomesha wanafunzi wachache zaidi, kinyume cha lengo la kitaifa la kuwa na wasomi wengi. Takwimu za Serikali kupitia Bodi ya Mikopo zinaonesha kuwa kwa sasa wanafunzi wanaogharamiwa kwa asilimia 100 ni takribani asilimia 75 ya wote wanaopewa mikopo kwa sasa ikiwa ni wale wa vyuo vikuu vya umma na walioko vyuo binafsi. Serikali inajenga hoja zaidi, kitakwimu, kwamba iwapo kwa idadi ya sasa ya wanafunzi 60,000 wanaolipiwa mikopo kwa viwango mbalimbali, ikaamuliwa wote walipiwe asilimia 100 bila kujali uwezo wa mhusika, ni wanafunzi 40,000 tu nchi nzima watakaoweza kuendelea na masomo huku 20,000 wakilazimika kurejea nyumbani kwa kukosa udhamini.
0 comments