Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Bakwata: Mambo magumu kwa mbuzi wa sadaka toka Saudia

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

ZAIDI ya Dola 10,000 za Kimarekani zinahitajika kwa ajili ya kugombolea mbuzi wa sadaka waliokwama kwa takriban miezi nane sasa katika bandari kuu ya Dar es Salaam walioletwa Tanzania kutoka nchini Saud Arabia kupitia Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) kama Sadaka kwa Waislamu mara baada ya kukamilika kwa ibada ya Hijja iliyopita.

Mbuzi hao ambao tayari wameshachinjwa na kuhifadhiwa katika kontena maalum la kuhifadhia nyama inasemekana waliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam Januari mwaka huu kama Swadaqa kwa Waislaam.

Akizungumza na Mwananchi Ofisini kwake Bakwata makao makuu, Naibu Mufti wa Tanzania Sheikh Suleiman Gorogosi alisema, jambo lililokwamisha kutolewa kwa nyama hiyo bandarini Dar es Salaam ni ukubwa wa gharama ya kugombolea bandarini hapo.

''Zamani vitu vya taasisi za kidini vilikuwa vikipita bure bandarini lakini sasa kila kitu kimebinafsishwa na tunatakiwa tulipe fedha nyingi ili tuweze kupata mbuzi hao,'' alisema Sheikh Gorogosi.

Alifafanuwa kwamba kuna kipindi fedha iliyohitajika ilifikia Dola za Kimarekani 10,000 kugombolea mbuzi hao, lakini sasa inaweza kuzidi kwa sababu kadiri kontena linavyoendelea kukaa bandarini na ndio gharama inaongezeka.

Aliwataka Waislaam kuwa na subira na kwamba juhudi za kuutoa mzigo huo zinaendelea na kwa sasa maafisa wa Bakwata wanajaribu kuongea na wahusika ili waweze kupunguziwa gharama hiyo.

Alibainisha kwamba suala la kuharibika kwa mbuzi hao kama inavyodaiwa na baadhi ya watu halipo kwani wamehifadhiwa katika mazingira mazuri na kwamba kama kuna muislaam anayeweza kujitolea kutoa hiyo fedha basi muda wowote watatolewa na kufikishwa kwa wahusika.

Kwa Mujibu wa Sheikh Gorogosi, mbuzi hao waliotolewa bure kama Sadaka ni vigumu kutumia fedha nyingi kama hiyo kwa ajili ya kuwagomboa wakati kuna misikiti, madrasa na visima vinahitajika kwa Waislam vijijini.

''Mbuzi wenyewe wametolewa bure, sasa kwa nini sisi tutumie fedha nyingi kuwatoa bandarini. Si afadhali tu fedha hiyo itumike kujenga madrasa, misikiti na kuchimba visima kwa Waislaam,'' alihoji Sheikh Gorogosi.

Alifafanua kwamba walipoingia madarakani miezi miwili ilyopita tayari mbuzi hao wameshakaa bandarini kwa takriban miezi mitano na wao si wa kulaumiwa kwani hata hao walioondoka walishindwa kuwagomboa kwa sababu ya ukubwa wa gharama yake.

Awali Sheikh Gorogosi alianza kwa kusema wao hawazungumzii chochote kwa sasa kuhusu mbuzi hao kwa kuwa suala hilo limeshaandikwa na kutangazwa sana katika baadhi ya vyombo vya habari lakini baadaye alithibitisha kuwepo kwa mbuzi hao na kwamba tatizo ni fedha ya kugombolea.

Aidha sheikh Gorogosi alisema Waislamu wasitegemee kuwa mbuzi hao watagaiwa misikini kama ilivyozoeleka badala yake watagaiwa katika vituo vya kulelea mayatima, wajane, mafukara na masikini ambao ndio walengwa.

Sheikh Gorogosi alitoa wito kwa Waislamu kwamba wanapokuwa na hoja yeyote kuhusu Baraza Kuu la Waislaam Tanzania ni vyema wakaenda ofisini makao Makuu na kupatiwa data kamili kuliko kukaa katika vyombo vya habari na kutoa shutuma.

Hata hivyo Sheikh Gorogosi hakutoa muda maalum wa kutolewa kwa mbuzi hao bandarini lakini alisema kuwa muda wowote itakapopatikana fedha ya kuwagomboa watatolewa na kufikishwa kwa walengwa ambao ni mayatima, wajane, mafukara na masikini.

Wiki iliyopita Mnajimu maarufu nchini Sheikh Yahya Hussein kupitia kituo cha televisheni cha 'Channel Ten' alimtaka Mufti awatoe mbuzi hao na kuwagawa kwa Waislamu.

Sheikh Yahya pia alisema Mufti kama hatogawa mbuzi hao basi ajitokeze mbele ya Umma na kuuomba radhi kabla ya kwenda Hijjah kutokana kuchelewa kutolewa na kugaiwa mbuzi hao kwa Waislaam.

Tags:

0 comments

Post a Comment