Siku ya uzinduzi wa mkutano mkuu wa chama cha Republikan nchini Marekani kwa bahati mbaya imeambatana na kuwasili kwa kimbunga Gustav katika eneo la kusini mashariki mwa Marekani. Wakaazi wa mji wa New Orleans wanahama.
Rais wa Marekani George W. Bush huenda asishiriki katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama chake cha Republikan katika jimbo la Minnesota kutokana na kimbunga Gustav ambacho kinasonga mbele kuelekea maeneo ya karibu na Ghuba ya Mexico nchini Marekani.
Huenda pia mkutano huo mkuu wa chama ambao utamuidhinisha rasmi mgombea wake wa kiti cha urais John McCain na mgombea mwenza bi Sarah Palin usifunguliwe leo jioni majira ya huko Marekani sawa na usiku majira ya hapa Ulaya.
Wakaazi wa mji wa New Orleans, sasa wanauhama mji huo baada ya Meya wa mji huo, Ray Nagin kuamrisha wakaazi wote wahame kuepukana na kimbunga hicho, kibaya kabisa alisema kwa maneno haya:
´´Hii ni dhoruba mbaya zaidi katika karne hii. Hakuna dhoruba nyingine mtu anaweza kusema itakuwa na nguvu zaidi ya hii na hatujui itakuwa na ukali kiasi gani´´.
Kimbunga Gustav kimepungua kidogo na kurejea kwenye hatua ya 3 wakati kikiingia katika Ghuba ya Mexico, lakini wadadisi wa hali ya hewa wamesema kuna uwezekano mkubwa kikapiga hatua nyingine ya 4 mnamo masaa machache yajayo.
Kimbunga Gustav ambacho tayari kiliwauwa watu kiasi ya 80 katika visiwa vya Caribbean, kinatarajiwa kufika kwenye nchi kavu ya Marekani baadae hii leo katika maeneo yaliyoko kati ya majimbo ya Mississipi na Texas, kusini mashariki mwa nchi. Amri ya kuwahamisha wakaazi wote wa mji wa New Orleans, ni ya kwanza tokea kimbunga Katrina kupiga eneo hilo miaka mitatu iliyopita na kusababisha hasara kubwa ambapo serikali ilikosolewa kutowajibika.
0 comments