Pages

Monday, April 11, 2011

Breaking News... Gbagbo akamatwa


Kiongozi aliyekuwa aking'a ng'ania madaraka nchini Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo, amekamatwa na wapiganaji wanaomuunga mkono Alassane Ouattara katika operesheni ya wanajeshi wa Ufaransa na Umoja wa Mataifa.

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa vikosi vinavyomtii Alassane Ouatarra vimemkamata hasimu wake wa kisiasa, Laurent Gbagbo, ambaye amekuwa akijificha mjini Abidjan.
Kwa mujibu wa msemaji wa Ouattara, Affousy Bamba, aliyezungumza na Shirika la Habari la Reuters, ni kweli Gbagbo amekamatwa. Kwa sasa kiongozi huyo analindwa na Umoja wa Mataifa. Duru za Umoja wa Mataifa zinazithibitisha taarifa hizo.
"Tunahakikisha kuwa anapata ulinzi wa kutosha kama yanavyoeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kuwalinda wadau wa kisiasa. Azma yetu ni kuhakikisha kuwa hapatwi na madhara yoyote." Imesema taarifa kutoka makao makuu ya Umoja huo, mjini New York.
Ufaransa yakanusha kushiriki
Wakati huo huo, vifaru vya Ufaransa vikisaidiana na ndege za Umoja wa Mataifa zilionekana zikipiga doria kwenye barabara za mji mkuu wa Abidjan. Hata hivyo Ufaransa imeyakanusha madai kuwa vikosi vyake vilihusika katika operesheni hiyo.
"Siwezi kuzungumza kwa niaba ya vikosi vya Ufaransa au vyengine vyovyote vile ila vilikuwepo vikosi vya Liconte vilivyokuwa vikishirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na kuyatimiza majukumu yao kwa kulifuata azimio la 1975 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa". Anasema afisa wa Umoja wa Mataifa, Haq.
Kulingana na mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, aliyeko mjini Abidjan, vifaru 11 vya Ufaransa vilivyosindikizwa na ndege chapa M1-24 na malori madogo yaliyowabeba wanajeshi wanaomuunga mkono Alassane Ouatarra yalionekana yakisafiri kuelekea kwenye makaazi ya Laurent Gbagbo.
Malori hayo yanaripotiwa pia kuegeshwa kwenye sehemu muhimu katika eneo la Cocody ambalo ni moja ya machache yanayodhibitiwa na vikosi vya Gbagbo.
Dhamira ya hatua hiyo ni kuwazuia wanajeshi wanaomtii kutosogea. Ifahamike kuwa Laurent Gbagbo amekuwa akijificha kwenye makazi ya rais kwa kiasi ya wiki moja sasa chini ya ulinzi wa vikosi vilivyosalia vinavyomtii.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, shambulio la Jumapili lilikuwa la kulipiza kisasi lile lilofanywa na wafuasi wa Gbagbo walioivamia hoteli ya Ouattara ambako ndiyo makao yake makuu.
Hoteli hiyo iliyo na afisi nyingi za Umoja wa Mataifa ilivamiwa Jumamosi iliyopita wakati wa  mchana na wanajeshi waliojihami kwa silaha nzito waliotokea eneo la handaki alikokuwa anajificha Gbagbo.
Kwa upande mwengine, Alassane Ouattara anatambuliwa na jamii ya kimataifa kama mshindi halali wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Cote d'Ivoire uliofanyika mwishoni mwa mwezi wa Novemba mwaka uliopita.
Hata hivyo Laurent Gbagbo bado anang'ang'ania madaraka. Kwa mujibu wa mkuu wa operesheni za kulinda amani za Umoja wa mataifa, Alain le Roy, ombi la Gbagbo la kusitisha mapigano linaonekana kuwa ilikuwa njama ya kuwawezesha wapiganaji wake kujikusanya upya.
Vikosi vya Ouatarra vimeziteka nyara sehemu nyingi za mji wa Abidjan katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Hata hivyo hofu imetanda kuwa huenda mapigano hayo yakasababisha umwagikaji mkubwa wa damu kwani pande zote mbili hasimu zinaendelea na mapambano.     
Kituo cha televisheni cha Laurent Gbagbo cha RTI, kinachoendelea kurusha matangazo kwenye baadhi ya sehemu za mji yanawatolea wito wanajeshi wanaomtii kupambana na vikosi vya hasimu wao.
Mwakilishi wa Alassane Ouatarra aliyeko mjini London, Isahak Kounate, amewataka raia wote wa Cote d'Ivoire waungane katika kipindi hiki kigumu.
"Hakuna mazingaombwe. Huu ni wakati mgumu. Lazima tufungue ukurasa mpya na tuwe na maridhiano na kuvumiliana. Lazima tufanye kazi kwa bidii na tukiri kuwa makosa yametendeka na tuanze upya kwa pamoja." Amesema Kounate.
Kulingana na wakaazi wa eneo hilo, mapigano makali yameendelea hii leo kati ya kambi mbili zinazohasimiana. Changamoto kubwa inayomkabili Ouatarra ni kuwaunganisha raia wa Cote d'Ivoire waliogawika kwa sababu ya mapigano hayo.

No comments:

Post a Comment