OFISA wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), ametiwa mbaroni na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuliibia shirika hilo fedha zaidi ya Sh1.3bilioni.Tuhuma dhidi ya ofisa huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa), zimekuja wakati ambao Tanesco wanaelezwa kuwa na hali mbaya kifedha, kutokana na madai kuathirika kimapato hali inayochangiwa na hujuma zinazofanywa na watu wasiofahamika katika miundombinu yake.
Kadhalika Tanesco hivi sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuilipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans fidia ya Sh94 bilioni kufuatia tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimtaifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC).
Tuzo hiyo kwa Dowans ambayo iko katika mchakato wa kusajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania ili iweze kulipwa, ilitolewa na ICC kufuatia Tanesco kuvunja mkataba baina yake na Dowans kinyume cha makubaliano ya pande hizo mbili.
Habari za zilizolifikia Mwananchi jana kutoka katika vyanzo vya kuaminika na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, zilisema fedha zilizoibwa na mtumishi huyo zilitokana na mauzo ya umeme wa Luku.
Habari hizo zinadai kuwa ofisa huyo ambaye ni Mhasibu Mwandamizi wa mapato ndani ya shirika hilo, anatuhumiwa kuiba fedha hizo kati ya Oktoba 2009 na 2010 katika ofisi za Tanesco mkoa wa Kinondoni Kaskazini, alikokuwa akifanyia kazi kabla ya kuhamishiwa makao makuu mwaka jana.
Melezo ya Mkurugenzi Mkuu Mhando
Akizunguma na Mwananchi kwa simu jana, Mhando alisema ofisa huyo anatuhumiwa kutenda makosa kwa kushirikiana na wafanyabiashara mbalimbali waliokuwa wakinunua umeme katika ofisi hizo.
“Ni kweli huyo mtu tunaye na anatuhumiwa kushirikiana na ma-vendor wetu (wauzaji wa rejareja). Inaonekana alikuwa akiwauzia umeme mwingi kuliko umeme aliotakiwa kuutoa kulingana na gharama walizolipia,” alisema Mhando.
Alisema suala hilo lilibainika baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa ndani ambao uliwezesha kugundulika upotevu wa kiasi hicho kikubwa cha pesa na kwamba baada ya kubaini tatizo hilo hatua zilizochukuliwa ni kumhamishia afisa huyo makao makuu ili kupisha uchunguzi.
“Kwa kawaida huwezi kumfukuza tu mtu kazi kienyeji, kwa hiyo kwanza “tulim-charge” tukamtaka aandike maelezo ni kwa nini asifukuzwe kazi ,” alisema Mhando.
Alisema baada ya timu iliyoundwa kushughulikia suala hiyo kukaa na kupitia maelezo yake ilibainika kuwa afisa huyo ana hatia na kwamba hatua iliyokuliwa ni kukatisha mkataba wale wa ajira.
“Lakini kwa kuwa hizo ni pesa nyingi na ni za umma tukaona ku-terminate (kukatisha) tu mkataba wake haitoshi hivyo wakaguzi wakaamua kumfikisha polisi kwa hatua zaidi za kisheria;“Kwa hiyo baada tu ya kukatisha mkataba wake na askari wakamkamata hapohapo ofisini,” alisema Mhando.
Kwa mujibu wa habari kutoka kwa vyanzo hivyo afisa huyo alitiwa mbaroni Ijumaa iliyopita akiwa ofisini kwake makao makuu ya Tanesco, ambako alihamishiwa wakati uchunguzi wa tuhuma zake ukiendelea .“Mpaka ninavyokwambia hivi sasa yuko Central (Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam), kilidokeza chanzo chetu na kuongeza kuwa huenda leo ofisa huyo akapandishwa kizimbani kwa tuhuma hizo tuhuma hizo zinazomkabili,".
Hata hivyo kwa mujibu wa habari kutoka katika vyanzo vyetu wafanyabiashara hao bado hawajakamatwa na kwamba bado jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka ili kuwaunganisha katika tuhuma hizo.
Watoa habari wetu walidokeza kuwa kutokana na unyeti wa tuhuma hizo hasa kwa kuzingatia kiwango cha pesa zilizoibwa, polisi wamehofu kumpa dhamana kituoni hapo kwa kudhani kuwa anaweza kutoroka na hivyo kusubiri afikishwe mahakamani kwanza.
Maelezo ya Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alipoulizwa kuhusiana na taarifa za kukamatwa kwa mhasibu huyo alisema kuwa suala hilo haliko chini yake, bali liko ofisi ya Kanda Maalum, hivyo alilielekeza Mwananchi kuwasiliana na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda hiyo, (ZCO), Ahmed Msangi.
Hata hivyo ZCO Msangi alipotakiwa kutoa ufafanuzi alisema kwa upande wake yeye hawezi kulizungumzia, kwa maelezo kwamba si msemaji mkuu isipokuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova.
Naye Kova alipoulizwa alisema asingeweza kulitolea ufafanuzi kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi na kwamba mahali alipokuwa hakukuwa na mawasiliano mazuri.“Kwa sasa siko ofisni, niko nje kidogo ya jijini na mawasiliano huku si mazuri maana hata nakupata kwa shida, lakini kesho nitafanya Press Conference (mkutano wa waandishi wa habari) hivyo njoo kesho nitatoa ufafanuzi wa kutosha,” alisema Kova.
Habari za Kitaifa
Wizi kupitia mashine za Luku
Septemba 7, mwaka jana
Tanesco lilitanga kubaini kuwepo kwa mtandao wa wezi wa umeme kupitia mashine za Luku na vituo feki vya kuuzia umeme huo.
Kufuatia hali hiyo, shirika hilo lilianzisha operesheni endelevu ya kuwasaka wahusika wakiwemo watumishi wake wanaohisiwa kuhusika.
Katika siku ya kwanza ya utekelezaji wa operesheni mashine 7 kati 11 za Luku ambazo awali zilibainika kuwa na tatizo, zilihakikiwa katika maeneo ya Mwenge na Kariakoo zilihusishwa na wizi wa umeme.
Msemaji wa Tanesco, Badra Masoud alisema kupitia kitengo maalumu cha Luku kilichoanzishwa na shirika hilo walikuwa wakifuatilia taarifa za kuwepo kwa hujuma katika shirika hilo kupitia Luku na mita za kawaida, zinayofanywa na baadhi ya wafanyakazi halali wa shirika hilo.
0 comments