Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - MAGUFULI AAGIZA JENGO LA TANROADS LIVUNJWE

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI  wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli amefichua ufisadi wa Sh5 bilioni uliotaka kufanywa katika manispaa tatu za jijini Dar es Salaam kwenye ulipaji wa fidia za ubomoaji wa nyumba kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara.

Mbali na kufichua ufisadi huo jana, Magufuli ameagiza jengo la Wakala wa Barabara (Tanroads) lililopo ndani ya Kituo cha Daladala cha Ubungo,  libomolewe ndani ya siku tano kuanzia jana kwa kuwa lipo ndani ya hifadhi ya kituo cha mabasi yaendayo kasi.

Dk Magufuli aligundua uozo huo na kutoa maagizo ya utekelezaji jana katika ziara yake ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk Magufuli, majengo ya ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini humo, nayo yapo ndani ya hifadhi ya barabara jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Barabara Namba 167 ya mwaka 1967.

Akizungumza kabla ya kuanza ziara hiyo, Dk Magufuli alisema kuwa Serikali haikuridhika na tathimini ya kwanza iliyofanywa na wathamini kutoka Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke na kuthibitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.

“Gharama za tathmini hiyo ilikuwa Sh27.7 bilioni kwa mali na nyumba 1,487. Lakini kabla ya kulipa, wizara iliona vyema kujiridhisha kwa kutembelea eneo la tathimini husika na kugundua mapungufu kadhaa,” alisema Magufuli na kuongeza:

“Mapungufu hayo ni pamoja na kurukwa kwa baadhi ya mali na nyumba pamoja na gharama za nyumba zenye sifa sawa kutofautiana kutoka manispaa moja na nyingine.”

Baada ya kugundua mapungufu hayo, Dk Magufuli alisema Wizara ilimtafuta mthamini wa kujitegemea ‘Independent Valuer’ ili afanye uhakiki na kurudia uthamini pale ilipohitajika kwa maslahi ya taifa.

"Unajua ilikuwaje? Nyumba zipatazo 61 zenye thamani ya Sh 239,781,542 hazikuonekana, kati ya hizo nyumba 56 zipo katika eneo la barabara ya Jet Corner-Vituka-Davis Corner na nyumba tano ziko eneo la kati ya stendi ya mabasi ya Ubungo na Kigogo,” alisema Magufuli.

Alisema kuwa baada ya tathimini mpya kufanywa, gharama za nyumba zote ni Sh 22,710,003,114,  tofauti na uhakiki uliofanywa na manispaa hizi tatu, uhakiki wa independent valuer umefanya Serikali iokoe Sh5 bilioni.

Alisema kuwa baada ya matokeo hayo, wizara iliamua kukamilisha tathimini ya nyumba 215 zilizokuwa zimebaki katika mradi ambazo zimethaminiwa na kuwa Sh 2,638,726,633 na kwamba hatua hiyo ilifanya tathimini yote kuwa na nyumba 1580 kwa gharama ya Sh 25,348,729,752.

“Tathimini hii imesainiwa na wahusika wote tayari kwa malipo kwa wale tu wanaostahili kulipwa kwa mujibu wa sheria ya barabara namba 13 ya 2007. Wanaostahili kulipwa wataanza kulipwa keshokutwa (Alhamisi), waje na vitambulisho vyao, picha zao tunazo hivyo wasijaribu kufanya uhuni,’ alisema Magufuli

Aliongeza, “ Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakuu wa wilaya na wakurugenzi, kuweni makini sana na hawa maofisa wa ardhi wa wilaya, wanaweza kuitia Serikali gharama zisizostahili, hizi  Sh5 bilioni si zinajenga barabara nyingine.”

Alisema kuwa majina ya wamiliki hao hewa wa nyumba 61 atayakabidhi kwenye mamlaka husika ili wachukuliwe hatua kwa kukiuka taratibu kwa kuwa wamesababisha ujenzi wa barabara hiyo kuchelewa na kuitia Serikali hasara.

Magufuli alimweleza kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiq kuwa manispaa za jijini Dar es Salaam zina watendaji wabaya na kumtaka kuwashughulikia.

“Afisa ardhi gani anagawa viwanja katika maeneo ya barabara?, tuwachukulie hatua na ikibidi tuwaweke ndani. Wanatuharibia halafu wanakuwa wa kwanza katika vikao vyetu, hawa ndio wanaichonganisha Serikali na wananchi,” alisema Magufuli.

Akitoa ufafanuzi wa watu wanaostahili kulipwa katika upanuzi wa barabara inayoanzia Stendi ya Mabasi ya Ubungo mpaka Jengo la Klabu ya Yanga lililopo Ilala, Magufuli alisema kuwa waliojenga nyumba zao kuanzia Mabibo Mwisho mpaka Ilala Mchikichini, hawatalipwa.

“Eneo la Klabu ya Yanga mpaka Ilala Mchikichini kabla ya kuvuka daraja, waliojenga nyumba pembeni ya barabara hii watalipwa fidia kwa kuwa eneo hilo halipo katika sheria ya 167 ya mwaka 1967 na pia halipo katika sheria ya barabara kifungu cha 13ya mwaka 2007,” alisema Magufuli.

Akiwa anapita katika barabara hiyo na kusimamisha magari huku akiwaeleza wananchi kuhama maeneo hayo, Magufuli alisema wengine watakaolipwa katika upanuzi wa barabara hiyo, ni wale waliojenga nyumba zao kuanzia Ubungo Kisiwani hadi Mabibo Ward na kwamba nyumba 201 ndio zitakazolipwa. Alisema mradi huo utagharimu Sh 4,429,336,710.

“Nyumba zilizojengwa katika eneo la barabara ambazo zipo, Mbuyuni, Mabibo Farasi, Mabibo Matokeo, Mburahati Kisiwani, Kigogo Mkwajuni na Kigogo Kati, hazitalipwa kwa kuwa eneo zilizopo ni kwenye Highway Ordinance chini ya Sheria namba 167, na pia zipo katika Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007,” alisema Magufuli.

Mbali na kutembelea barabara hiyo, Magufuli pia alikagua ujenzi wa barabara ya Jet Corner - Yombo Vituka- Davis Corner na kusema kuwa  mradi huo utagharimu Sh 11,989,526,692. Alisema wananchi wote waliojenga pembezoni mwa barabara hiyo, watalipwa.

“Barabara hii ina urefu wa kilomita 10.3. Hawa wote watalipwa isipokuwa katika maeneo ambayo kulifanyika ulipaji kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege,     ujenzi wa Daraja la Mwinyi, nyumba zipo 766,” alisema

Aliongeza, “Nyumba 149 zilizopo maeneo ya Kiwalani Kigilagila na Nyambwela bado zinafanyiwa uhakiki kwa kuwa pia zilihusika katika ulipaji wa fidia wa mradi wa Jet-Lumo miaka ya nyuma, uhakiki zaidi unahitajika.”

Magufuli ambaye alifanya mkutano na kuzungumza na wananchi wa Yombo mara baada ya kuikagua barabara hiyo, alisema kuwa barabara hizo ni kubwa hivyo hazitawekewa matuta bali kutakuwa na alama za barabarani.

Alisema kuwa wananchi watakaochelewa kubomoa nyumba zao zitabomolewa na Serikali na hawataambulia chochote kwa kuwa kila kitu kitachukuliwa na Serikali kwa kuwa nyumba hizo zitakuwa zimeshalipiwa fidia na Serikali.

Alisema kuwa Serikali itatumia sh 17,973,091,427 kwa kulipa fidia.

“Kama nyumba yako imeingia nusu ndani ya eneo la barabara, itabomolewa hiyo nusu na wewe utalipwa kulingana na ulivyobomolewa, hatuwezi kulipa gharama ya nyumba nzima wakati umebomolewa nusu,” alisisitiza.
Tags:

0 comments

Post a Comment