| ||||||
Na Jackson Odoyo TANZANIA jana ilisherehekea maadhimisho ya miaka 48 tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1961, huku Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akishindwa kuhudhuria kwa mara ya tatu mfululizo. Pamoja na Mkapa pia mawaziri wake wakuu wote wastaafu na wa sasa, Mizengo Pinda wakikosekana katika sherehe hizo. Hata hivyo, gazeti hili lilielezwa kuwa Mkapa na Pinda walikuwa na udhuru. Mawaziri wakuu wa Tanzania waliopaswa kuwapo katika sherehe hizo lakini hawakufika ni pamoja na Rashid Mfaume Kawawa, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim, John Malecela, Jaji Joseph Warioba, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam William Lukuvi aliliambia gazeti hili jana kuwa baadhi ya viongozi hao wametoa taarifa za udhuru lakini wengine hana taarifa zao. Aliwataja mawaziri aliokuwa na taarifa zao kuwa ni Mizengo Pinda aliyesema kuwa yuko nje ya nchi kwa ziara ya kikazi akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye naye yuko nje ya nchi. Lukuvi alifahamisha kuwa Edward Lowassa pia alitoa udhuru kutokana na uchovu baada ya usiku wa kuamkia jana kukesha kwenye sherehe za kumwaga binti yake anayeolewa wiki hii. "Mimi nina taarifa ya Lowassa ambaye jana tulikuwa naye kwenye sherehe za kumwaga binti yake na leo asubuhi kaniambia hatafika kutokana na uchovu na kuwasindikiza wageni wake waliotoka Monduli," alisema Lukuvi na kuongeza: "Mwingine ambaye nina taarifa yake ni Mkapa na Waziri Mkuu Pinda ambao wako nje ya nchi kikazi, waliobaki sina taarifa nao kwa sababu sherehe zimeandaliwa na ofisi ya waziri mkuu hivyo hata udhuru wao huenda wamepeleka huko." Hata hivyo kuna taarifa zinazodai kuwa Mzee Rashid Kawawa ni mgonjwa hivyo dhahiri kwamba isingekuwa rahisi kwake kuhudhuria sherehe hizo. Hii ni mara ya kwanza kwa mawaziri wakuu wote kukosekana katika sherehe za uhuru hasa ikizingatiwa kuwa hizi ni sherehe za kitaifa na wao wamekuwa watendaji wakuu wa serikali. Katika sherehe hizo zilizofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliendelea kung'ara baada ya umati kumshangilia zaidi kuliko viongozi wengine wa kitaifa. Hii ni mara ya pili kwa Mwinyi kushangiliwa katika sherehe hizo baada ya mwaka jana kushangiliwa kwa vifijo na nderemo. Mbali na Mwinyi kiongozi mwingine aliyeshangiliwa uwanjani hapo ni Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsa Vuai Nahodha. Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na mkewe Nadia Karume, Jaji Mkuu wa Tanzania Augustine Ramadhan, Spika wa Bunge Samuel Sitta na mkewe Margaret Sitta. Viongozi wakuu wa vyama vya siasa waliohudhuria sherehe hizo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu Seif Sharrif Hamad na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo. Akizungumzia maendeleo yaliyopatikana katika miaka 48 ya uhuru, Cheyo alisema Tanzania imefanikiwa kufikia malengo mengi na nchi imepiga hatua kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma. “Leo hii tunazungumzia suala la maendeleo na kati ya mambo ambayo ni lazima tuyataje ni suala la elimu, nchi imepiga hatua kubwa katika elimu, pili suala la kilimo hili ni eneo lingine tulilopiga hatua katika miaka 48 ya uhuru na tatu ni suala la barabara,"alisema Cheyo. Alisema kabla ya uhuru Tanzania ilikabiliwa na uhaba wa vyuo, lakini sasa tatizo hilo limeonekana kuwa historia baada ya vyuo vingi kuanzishwa huku vingine vikiendelea kujengwa. Katibu Mkuu Mstaafu CCM, Philip Mangula alisema maendeleo yapo na kila mtu anapaswa kuyakubali kwa sababu Tanzania ya sasa sio kama ile kabla ya uhuru. Sherehe hizo za uhuru zilipambwa kwa gwaride maridadi kutoka majeshi mbalimbali ya ulinzi na usalama yaliyokuwa katika vikundi saba huku kila kundi moja likiwa na wanajeshi zaidi ya 75. Vikundi hivyo vilivyotumbuiza kwa mbwembwe vilianza kutembea kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka muda mfupi kabla Rais Kikwete hajapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride. Hata hivyo kupigwa kwa mizinga hiyo kulisababisha watu 28, wanaume 11 na wanawake 17 kuzirai kwa mshtuko mkubwa walioupata. Muuguzi mkuu wa Manispaa ya Temeke, Lukia Msham aliwaambia waandishi wa habari baadaye kuwa wametoa huduma ya kwanza kwa watu wote waliopatwa na mshtuko huo. Alisema: "Tumeokota watu 28 wakiwamo wanafunzi, lakini baada ya kupatiwa huduma ya kwanza walipata nafuu na kuruhusiwa," alisema. |
You Are Here: Home - - Mawaziri wakuu wakosekana katika Sherehe za Uhuru
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments