Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kesi ya kudai tume huru ya uchaguzi kufikishwa kortini Des 15

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

CHAMA cha NCCR Mageuzi kimepanga kufungua kesi ifikapo Desemba 15 kudai tume huru ya uchaguzi.

Siku hiyo imepangwa kwa kuwa ndiyo itakuwa mwisho wa notisi yao ya siku 90 waliyoiandika kwa serikali kuilezea nia yao ya kufungua kesi hiyo.

Katibu mkuu wa chama hicho, Samuel Ruhuza aliwaambia waandishi wa habari jana tangu walipotangaza notisi hiyo Agosti 12 mwaka huu, serikali imeshindwa kutekeleza madai yao, hivyo wameamua kwenda mahakamani ili haki itendeke.

“Kwa kuwa Agosti 12, 2009, chama kilitoa notisi ya 90 kwa serikali kuhakikisha inaundwa tume huru ya uchaguzi, halmashauri kuu (ya NCCR Mageuzi) imeelekeza kuwa kesi ya kudai tume huru ya uchaguzi iwe imefunguliwa kabla ya Desemba 15, 2009," alisema.

"Tunaamini kuwa mafanikio ya kesi hii yatapunguza ukiritimba wa chama kimoja nchini na hivyo kuleta ustawi wa taifa.”

Alisema kwamba mfumo wa uchaguzi unasababisha kuwepo kwa malalamiko mengi yasiyokuwa ya lazima.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani, rais ambaye pia ni mgombea, ndiyo anayeteua watendaji wa tume ya uchaguzi, unadhani kuna haki hapo?

Hivi karibuni tumeshuhudia uchaguzi wa serikali za mitaa ambao chama tawala kimetumia mbinu nyingi kushinda kwa kishindo,” alisema.

Akizungumzia maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani, Ruhuza alisema kuwa chama hicho kimeazimia kuzindua mpango wa uchangishaji wa fedha kwa ajili ya uchaguzi huo, mpango ambao utazinduliwa na mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kigoma Desemba 16.

Tags:

0 comments

Post a Comment