'Waliompiga risasi' Nyamwasa, mahakamani
Watu wanne wamefikishwa mahakamani nchini Afrika Kusini wakishtakiwa kwa njama ya kumuua aliyekuwa mkuu wa jeshi nchini Rwanda Luteni General Kayumba Nyamwasa.
Inafahamika kuwa washukiwa hao wanne waliofikishwa mahakamani ni kutoka Tanzania, Somalia na Msumbiji.
Wote wanakabiliwa na mashataka ya kupanga njama ya mauaji na watafikishwa tena mahakamani Julai 14.
Watu wengine wawili waliokamatwa wakati wa msako mkuu wa polisi waliachiliwa baada ya mashtaka dhidi yao kufutwa.
Luteni Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa ambae alikuwa mwandani mkubwa wa Rais Paul Kagame sasa amegeuka kuwa mkosoaji wake mkubwa na alikwenda kuishi uhamishoni nchini Afrika Kusini mapema mwaka huu.
Serikali ya Rwanda inataka arejeshwe nchini humo kwasababu wanaamini amehusika na mashambulio kadhaa ya maguruneti mjini Kigali mwanzoni mwa mwaka huu.
Jenerali Nyamwasa anaamini serikali ya Rwanda ndiyo iliyohusika na jaribio la kumuua kwa risasi alipokuwa anaelekea nyumbani kwake mjini Johannesburg.
Serikali ya Rwanda inakanusha madai hayo kwa kusema hakuna sababu yoyote ya kumuua.
0 comments