IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WATU wawili wamejitokeza kugombea kiti cha Urais kwa tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP), akiwemo Mchungaji Macmillan Lyimo na aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwibara mkoani Mara, Mutamwega Mgahywa.
Katibu Mkuu wa TLP, Rajab Tao alisema hayo jana Dar es Salaam wakati Mchungaji Lyimo aliporudisha fomu.
Tao amesema, wagombea hao walichukua fomu hizo wiki iliyopita na kwamba hadi sasa majimbo 120 nchini, yamepata wagombea wa nafasi ya ubunge.
Kwa mujibu wa Tao, kesho ni mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu na kwamba, Mkutano Mkuu wa TLP kwa ajili ya kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu utafanyika Julai 12, mwaka huu.
Akizungumzia malengo ya kugombea nafasi hiyo, Mchungaji Lyimo amesema, kwa sasa Tanzania inahitaji kizazi kipya chenye dira na mwelekeo mpya wa kutoa tiba ya jinsi ya kurithi rasilimali zilizopo.
“Tanzania ina rasilimali za kutosha lakini ni masikini, ili rasilimali hizo ziweze kunufaisha wote lazima awepo daktari wa kutibu tatizo hilo kwa kuwa kwa kipindi chote hakuna aliyejua tatizo ni kitu gani,” alisema Lyimo.
Alisema ameamua kugombea kiti hicho baada ya kuandika vitabu vyake viwili vyenye; ‘Nuru ya mabadiliko’ na ‘Kizazi kipya kuteka siasa za Tanzania na Afrika’ ambapo anaamini kuwa hakuna atakayempinga kwa hoja kwa kuwa kaweka takwimu zote kisayansi na kiimani pia.
Alisema kwa mfano, Taifa la Tanzania lina maji ya kutosha, ni Taifa la pekee ambalo linahitaji kiongozi wa kizazi kipya chenye dira na mwelekeo mpya wa usawa wa rasilimali zilizopo.
Kuhusu kutenganisha siasa na dini, alisema yeye ni Mchungaji wa kisiasa kutoka Kanisa la Assemblies of God na kwamba, ana nia njema na ni mmoja wa wenye maadili wanaojitoa kwa ajili ya wengine.
Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inakutana leo mjini Dodoma kwa mkutano wa siku moja ambao kwa mujibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, utakuwa na ajenda moja ambayo ni kupitia Rasimu za Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 – 2020 na Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015.
You Are Here: Home - - Wawili TLP waomba kugombea urais
0 comments