Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ritta Mlaki ajiondoa jimbo la Kawe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MBUNGE wa Kawe Ritta Mlaki jana alitangaza bungeni kuwa hatagombea tena ubunge kipitia jimbo hilo badala yake atarudi bungeni kwa tiketi ya Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs).

Mlaki alitoa kauli hiyo alipokuwa amesimama kuchangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Miundombinu iliwasilisilishwa bungeni na Waziri Shukuru Kawambwa.

“Mheshimiwa Spika nachukua fursa hii pia kutangaza kwamba sitagombea ubunge wa Jimbo la Kawe mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu,” alisema Mlaki kabla ya kuendelea kuchangia mambo mengine yanayohusu wizara hiyo.

Baadaye Mlaki alilieleza gazeti hili nje ya Ukumbi wa Bunge kuwa uamuzi wake huo umetokana na kuridhishwa kwake na maendeleo kadhaa aliyoliletea Jimbo la Kawe.

Alisema katika kipindi cha miaka kumi alichokuwa mbunge wa jimbo hilo amefanya mambo mengi ikiwamo kuhamasisha jenzi wa shule za msingi na sekondari, upatikanaji wa maji safi na salama na miundombinu.

“Wakati naingia bungeni mwaka 2000, Kawe kulikuwa na shule moja tu ya sekondari ambayo ni sekondari ya Boko na chache sana za msingi, lakini sasa kuna shule 10 za sekondari na nyingi tu za msingi,” alisema na kuongeza

“Jimbo la Kawe pia lilikuwa na tatizo sugu la maji hasa katika maeneo ya Makongo, Bunju, Kunduchi Mtongani na wazo, lakini leo maeneo hayo yote maji sio tatizo tena.”

Alisema akiwa mbunge wa Jimbo hilo amefanikiwa kuhamasisha ujenzi wa zahanati kadha ikiwamo hospitali ya Madale aliyojenga mwenyewe kama mbunge.

“Hii hospitali nimeijenga mimi binafsi kama mbunge, nilitafuta ufadhili na kufanikiwa kuikamilisha, lakini pia kuna hospitali ya Mbopo ambayo pia imejengwa kwa usimamizi wangu,” alisema

Mlaki pia alitaja maendeleo ya miundombinu ya barabara kuwa jambo jingine analojivunia katika kipindi cha uwakilishi wake wa jimbo hilo “Hili nalo liko wazi hakuna anayepinga.”

Alipotakiwa kueleza madai ya baadhi ya watu kuwa uamuzi wake huo umetokana na kuwakimbia wapinzani waliojitokeza kugombea ubunge jimbo hilo mwaka huu alijibu, “Madai hayo nimeyasikia, lakini nataka niseme mbele ya Mungu kwamba mimi ni mwanamke jasiri nisiyeogopa mtu,”

“Mwaka 2000 nilipambana na watu hatari sana, lakini nikashinda vivyo hivyo nisingeacha kugombea eti kwa kuwaogopa hawa wanaojitangaza kuja.”

Watu kadhaa akiwamo mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mbunge Viti Maalum (Chadema) Halima Mdee na mpinzani wake wa siku kupitia CCM Adamjee tayari wanatajwa kutaka kuliwania jimbo hilo.
Tags:

0 comments

Post a Comment