Baraza la Mawaziri la Misri limejiuzulu rasmi, huku waandamanaji wenye hasira, wakiendelea na maandamano yao katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
Mawaziri wote wa serikali ya Rais Hosni Mubarak, wamewasilisha barua zao za kujiuzulu leo hii, kufuatia ahadi ya kiongozi huyo ya mapema leo, kwamba angeliivunja serikali yake.
Hata hivyo, waandamanaji wameendelea kumshinikiza Mubarak mwenyewe aondoke madarakani. Zaidi ya watu elfu 50, wanaripotiwa kukusanyika katika uwanja wa Tahrir katika mji mkuu wa Cairo, licha ya onyo la jeshi kuwataka wachawanyike, na licha ya amri ya kutotoka nje iliyotaganzwa.
Wakati huo huo, jumuiya ya kimataifa imeendelea kuitaka serikali ya Misri kuepuka matumizi ya nguvu katika kukabiliana na waandamanaji. Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Hermann von Rompuy amemtaka Mubarak kuzuia umwagikaji wa damu na, badala yake aitishe mdahalo na raia wake.
Rais Barack Obama wa Marekani amesema Mubarak analazimika sasa aipe maana ahadi yake ya kufanya mageuzi.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, akiongea kwenye jukwaa la kiuchumi mjini Davos, Uswisi, amesema kuwa japokuwa utulivu nchini Misri ni jambo muhimu, lakini sio kwa gharama ya uhuru wa kutoa maoni.
Tokea kuanza kwa maandamano haya hapo jana, vyombo vya habari vimeripoti kuwa kwa uchache watu 95 wameshapoteza maisha nchini humo. Mawasiliano ya mtandao wa Intaneti, bado yamekatwa hadi sasa.
0 comments