NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameagiza taasisi za serikali na sekta binafsi kutoa fursa za upendeleo kwa kampuni za ndani ili kukuza uwezo wa wahandisi nchini. Dk Mwakyembe alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam jana wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya kuanzishwa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania (ACET). Alisema miradi inayotekelezwa na kampuni za ndani huwa na ubora wa hali ya juu, kwani wataalamu husika wanakaa nchini hawako tayari kulaumiwa kwa utendaji mbaya. Aliongeza kuwa hakuna taifa lolote duniani linalotegemea wataalamu wa nje kwa maendeleo yake na kwamba, haliwezi kupeleka nje wataalamu wake kuendeleza nchi nyingine. "Kwa sababu tunataka maendeleo, tutatumia mabingwa na wataalamu wetu, wao wanaelewa nchi yetu vizuri na matatizo yetu," alisema Dk Mwakyembe. Alisema gharama ya kutumia wataalamu wa ndani ni nafuu na fedha zinabaki nchini. Naibu waziri huyo pia aliwataka wahandisi hao kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma yao, kwani sekta hiyo imekuwa ikishtumiwa kwa rushwa kutokana na usiri wa utoaji na upokeaji wake. Dk Mwakyembe aliwataka wahandisi hao kuwaumbua watu wanaofanya kazi za sekta yao maeneo mbalimbali wakati hawana utaalamu. Naye Mwenyekiti wa ACET, Mwesigwa Kamulali, alipendekeza miradi inayogharamiwa na serikali itolewe kwa kampuni za ndani, pale inapotokea kuna pengo ndio watumie wahandisi wa nje. Kamulali alisema sheria ya ununuzi na kanuni zake ni kikwazo katika utendaji wao, kwani haina taratibu za kuwapandisha madaraja wahandisi wa ndani na kupelekea miradi mingi kusimamiwa na wahandisi wakazi wa kigeni. |
You Are Here: Home - - Kwa hili TZ Ingetakiwa ilipe kipaumbele tangia miaka ya 90
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments