Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wapo waliocheka, wapo walionuna, wapo walioumiza kichwa Uchaguzi mkuu 2010

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kina nafasi ya kubeba ushindi wa jumla lakini hali ni tete kwa upande wake, Uwazi lina habari kamili.

Hali inaonekana tete hasa kutokana na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ‘JK’, kuonekana ana dalili ya kupoteza wasaidizi wengi waliogombea ubunge sehemu mbalimbali nchini.
Kilango (Same).
Kwa hali ya kawaida, Rais kama mkuu wa serikali, wasaidizi wake ni mawaziri na wabunge wa chama chake kwa sababu huwategemea kupitisha bungeni miswada mbalimbali anayohitaji.

Kwa mujibu wa ‘taa’ ya Uwazi kwenye kata na majimbo yote nchi nzima, kiwango cha wasaidizi alichokuwa nacho JK katika serikali yake ya muhula uliopita, kitapungua kwa kasi kwa sababu wapinzani wameongeza idadi ya wabunge.
Aidha, kwa JK ambaye dalili zipo wazi kwamba anarudi Ikulu, hali ni tete kwa sababu mpaka sasa zipo ripoti kwamba baadhi ya mawaziri wake hawataliona bunge lijalo kupitia majimbo waliyogombea.

MAWAZIRI 
Mpaka tunakwenda mtamboni jana, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Huruma Mkuchika alikuwa na hali mbaya dhidi ya mpinzani wake kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Newala.
Sugu (Mbeya Mjini).
Kukosekana kwa Mkuchika bunge lijalo, itakuwa pigo mara mbili kwa JK katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa sababu Naibu Waziri, Joel Nkaya Bendera aliwekwa kando kwenye kura za maoni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Buriani mpaka tunakwenda mitamboni jana, ilielezwa kwamba alikuwa ameshindwa na Mgombea wa CHADEMA, Godbless Lema Jimbo la Arusha Mjini, ingawa aligoma kusaini matokeo.

Ripoti pia, zilikuwa zinaonesha hali ni tete kwa wasaidizi wa JK, kufuatia matokeo ya awali kuonesha kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alikuwa hana hali dhidi ya Ezekiah Wenje wa CHADEMA katika Jimbo la Nyamagana.
Mnyika (Ubungo).
Aidha, ilielezwa pia kwamba waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo alikuwa na hali mbaya Jimbo la Ilemela, huku Rais wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella ikitaarifiwa alikuwa anaelekea kushindwa Jimboni Ukerewe.

Wasaidizi wengine wa JK waliokuwa na alama nyingi za kupigwa mwereka ni Benson Mpesya (Mbeya Mjini) ambaye alikuwa hapumui mbele ya Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ wa CHADEMA, pia Basil Mramba hali ni ‘tia maji’ Rombo.

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Philip Marmo naye hakuwa na hali nzuri kwenye Jimbo la Mbulu.

Mramba (Rombo).
VIGOGO HOI HOSPITALI
Baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge (vigogo), walishikwa na ugonjwa wa ghafla na kukimbizwa hospitali wakiwa taabani baada ya ripoti kuonesha kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limewapa mkono wa ‘bai bai’.

Hospitali ya Bugando, Mwanza iliripotiwa kuwa vigogo wawili (majina tunayahifadhi) walikimbizwa hospitalini hapo na kupatiwa tiba ya haraka.

WENGINE WALIOLIA
Mgombea Ubunge wa CCM, Hawa Ng’humbi Jimbo la Ubungo alikuwa na hali mbaya kama ilivyo kwa mwenzake wa chama hicho, Angela Kizigha (Kawe).

Iringa Mjini, Monica Mbega (CCM) hali ilikuwa mbaya kwake na kwamba dalili za kushindwa zilijionesha tangu wakati wa kura za maoni ambapo alipigwa mwereka na aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Lugano Mwakalebela.

WALIOCHEKA
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA), amechekelea baada ya kufanikiwa kuwapiga kikumbo wapinzani wake na kurudi tena bungeni.
Mongella (Ukerewe).
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Sugu, ilikuwa ni kicheko Mbeya Mjini wakati aliyekuwa Mbunge Viti Maalum (CHADEMA), Halima Mdee furaha yake ilikuwa wazi Kawe.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uchumi na Fedha, Amos Makalla alifurahia matunda Mvomero, pia Jenister Mhagama (CCM) ni shangwe tupu Peramiho.

John Shibuda (CHADEMA), Maswa Magharibi, John Mnyika (CHADEMA), Ubungo, Musa Azzan Zungu (CCM) Ilala, Milton Makongoro Mahanga (CCM), Segerea, walikuwa na vicheko kwenye majimbo yao baada ya kupata ushindi.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila aliweza kukitoa kimasomaso chama chake baada ya kutangazwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini.
Masha (Nyamagana).
MATOKEO URAIS
Pamoja na Mgombea Urais wa CHADEMA, Willibrod Slaa kuonesha upinzani wa kweli, lakini nguvu yake imeonekano bado dhidi ya JK.

Matokeo yanaonesha kuwa Dk. Slaa aliachwa mbali na JK, ingawa kwenye jumla ya majimbo kumi yaliyotangazwa jana saa chache kabla hatujaenda mitamboni na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji (Mstaafu) Lewis Makame, mgombea huyo wa CCM alikuwa ana asilimia 43.

Majimbo hayo ni Micheweni, Konde, Singida Mjini, Korogwe Mjini, Njombe Mjini, Tumbe, Babati Mjini, Mtwara Mjini, Magogoni na Bukoba Mjini.

Slaa alikuwa na asilimia 18, wakati Mgombea wa CUF, Ibrahim Haruna Lipumba aliweza kuwapiga ‘bakora’ wagombea wenzake kwenye majimbo ya Pemba na Magogoni, Unguja.

Hadi tunakwenda mitamboni matokeo ya majimbo mengi yalikuwa bado kutangazwa washindi na Tume ya Taifa ya uchaguzi ambayo ilikuwa ikiendelea kukusanya matokeo. 
Tags:

0 comments

Post a Comment