Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Hukumu ya kihistoria

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania leo itatoa uamuzi wa rufaa ya Serikali kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Tanzania kuruhusu mgombea binafsi katika Uchaguzi Mkuu.

Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani ataongoza jopo la majaji wenzake sita, kutoa uamuzi huo.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa huenda utabadili historia ya siasa nchini, ikiwa itaruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi wa Tanzania.

Kama hilo litafanyika, litakuwa limeongeza mabadiliko mengine makubwa katika yale yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar ambako Baraza la Wawakilishi hivi karibuni katika mkutano wake, lilipitisha muswada utakaokuwa sheria itakayoruhusu kupigwa kura ya maoni ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo.

Ingawa Mahakama ya Rufaa ilikuwa haijatoa uamuzi, ilitoa angalizo kwamba uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ni halali hadi itakapoamua vinginevyo.

Majaji wa Mahakama Kuu, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo Mei mwaka 2006, walikubaliana na maombi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic (DP) Mchungaji Christopher Mtikila na kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu.

Mahakama Kuu iliruhusu mgombea binafsi kwa maelezo kuwa Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mahakama hiyo ilibainisha kuwa Katiba inatamka wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na haiweki masharti, kuwa hilo lifanyike kwa mtu aliyejiunga na chama fulani.

Katika uamuzi huo, iliamriwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ifanye marekebisho ya Sheria Namba 34 ya 1994 ambayo inapingana na kifungu cha 21 (1) cha Katiba ambacho kinampa haki ya mtu kugombea na kupiga kura.

Mahakama Kuu ilimpa Mwanasheria Mkuu kati ya Mei 5, 2006 hadi uchaguzi ujao awe amewasilisha bungeni sheria inayotoa fursa ya kuwapo mgombea binafsi katika uchaguzi bila kutegemea chama chochote.

Rufaa hiyo namba 45 ya mwaka jana, iliyokatwa na Jamhuri pamoja na Jaji Mkuu inasikilizwa pia na Jaji Eusebia Munuo, Januari Msofe, Nathania Kimaro, Mbarouk Salim, Bernard Luanda,na Sauda Mjasiri.

Katika rufaa hiyo, Serikali ilitoa sababu sita za kuikata; kwamba Mahakama Kuu ilikosea kujipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ilikosea kutengua vifungu vya Katiba ya nchi na ilikosea kisheria kupunguza matakwa ya lazima ya Ibara 30 (5) na 13 (2) ya Katiba.

Sababu nyingine ni mahakama hiyo kujipachika mamlaka ya Bunge ya kutunga sheria, kukosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na kuitolea uamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana.

Mara ya kwanza, Serikali ilipokata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama ya Rufaa mwaka 2007, Serikali ilidai mahakama hiyo ilikosea kisheria kutafsiri Ibara za 21 (1) (c), 39 (1) (c) (b) na 69 (1) (b) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa baada ya kukubaliana na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza, kwamba rufaa hiyo haina msingi na imejaa dosari za kisheria.
Tags:

0 comments

Post a Comment