IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MKUU mpya wa Wilaya ya Tandahimba, Husna Mwilima ameelezea uteuzi wake huo kuwa ni majibu ya Rais Jakaya Kikwete kwa tuhuma zote zilizoelekezwa kwake na viongozi wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).
Mwilima alisema anamshukuru Rais Kikwete kwa kurudisha heshima na imani yake kwa wananchi iliyotoweka baada ya tuhuma hizo.
Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu uteuzi wake na shutuma zilizotolewa na viongozi wa UWT wakati wanatangaza kumwengua katika nafasi ya ukatibu mkuu.
"Mdogo wangu, mimi sitaki kuzungumza sana lakini, namshukuru Mungu kwa yote, pili namshukuru mheshimiwa Rais kwa kuniteua na kurudisha imani yangu kwa wananchi," alisema Mwilima.
Alipotakiwa kueleza uteuzi huo unatoa funzo gani kwa UWT ambayo ilimfukuza kwa madai ya uwajibikaji mbovu, Mwilima alisema "Nadhani uteuzi alioufanya rais umejibu maswali yote dhidi yangu,".
Wakati Mwilima akiyasema hayo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mahusiano ya kimataifa wa UWT, Sarah Msafiri aliliambia gazeti hili kuwa "Sisi hatuuchukulii kivyovyote uteuzi wake, uteuzi si anafanya rais bwana, ninavyojua mimi akiamua rais hakuna mtu wa kuhoji,â€.
Hata hivyo, Sarah hakuwa tayari kuzungumza zaidi na kusema kuwa yuko safarini kuelekea mkoani Mbeya kwenye kikao.
Mwilima, ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, na Martin Shigela, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Lindi, waliteuliwa kuwa makatibu wa Jumuiya za CCM za wanawake na vijana mapema mwaka jana.
Lakini Husna akajikuta kwenye mgogoro mkubwa ambao vyombo vya habari viliripoti kuwa ulitokana na tofauti kati yake na Sophia Simba, ambaye ni mwenyekiti wa UWT.
Mgogoro huo uliishia UWT kumsimamisha Mwilima mwishoni mwa mwezi Februari ikieleza kuwa uamuzi huo ulifanywa na Baraza Kuu la umoja huo baada ya kuridhika kuwa kulikuwa na udhaifu katika utendaji wake, huku ikikanusha kuwepo kwa tofauti kati yake na Waziri Simba.
Wakati UWT ikimtimua Mwilima kwa madai ya utendaji mbovu, Rais Kikwete juzi alitangaza kumrudishia ukuu wake wa wilaya katika mabadiliko madogo aliyofanya yenye lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji.
Mbali na uteuzi wa Mwilima Rais pia amewabadilisha vituo vya kazi wakuu wengine wa wilaya 15 na kutengua uteuzi wa Thobias Sijabaje aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga kutokana na kutosimamia vizuri ugawaji wa vocha za pembejeo za kilimo katika wilaya hiyo kwenye msimu wa mwaka 2009/2010.
Akitangazwa kusimamishwa kwa Mwilima, Makamu Mwenyekiti wa UWT, Asha Bakari Makame alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Baraza la UWT kilichofanyika Dodoma Novemba 17 hadi 20 mwaka jana.
Alisema baraza lilimsimamisha kwa kuwa msingi wa UWT ni maadili ya kiutendaji na ukweli, kwa kuwa jumuiya hiyo ndio mama na baba wa CCM.
“Hii ni hatua ya kawaida ambayo inafanywa katika jumuiya yoyote na ni utendaji tu, mbona katibu mkuu wa CCM, Philip Mangula aliondoka na sasa yupo Yusuf Makamba,†alihoji.
You Are Here: Home - - Mwilima: Kikwete amewapa majibu kina Sophia Simba
0 comments