Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Zanzibar ni Shein, BILAL, NAHODHA SI RIZIKI

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Zanzibar ni Shein, BILAL, NAHODHA SI RIZIKI Send to a friend
Friday, 09 July 2010 23:22
Makamu wa Rais Dk Ali Mohamed Shein, akipunga mkono kusalimia wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM na wanachama wengine mjini Dodoma jana, mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM maarujfu kama 'White House'. Dk Shein jana alipitishwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.
Na Waandishi Wetu, Dodoma

MBIO za urais wa Zanzibar ndani ya CCM zilifikia ukingoni jana wakati Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein alipopoibuka na ushindi wa kishindo, akimbwaga mpinzani aliyeonekana kuwa wa karibu, Dk Mohamed Gharib Bilal. Dk Shein, ambaye amekuwa makamu wa rais tangu mwaka 2001 baada ya Dk Omar Juma kufariki, alikusanya kura 117 za wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM iliyokutana mjini hapa jana na kumuacha mbali Dk Bilal ambaye alipata kura 54, ambazo ni takriban nusu ya kura alizopata mshindi.

Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha alishika mkia katika majina matatu yaliyopelekwa na kamati kuu ya CCM iliyokutana jana asubuhi na kumaliza kikao chake mchana. Nahodha, ambaye alikuwa na umri mdogo kulinganisha na wagombea wenzake wawili, aliambulia kura 33 tu.

Dk Bilal na Nahodha walikubaliana na matokeo hayo na kutangaza kumuunga mkono Dk Shein, ambaye sasa anatakiwa kujiandaa kwa mpambano mkali dhidi ya chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, CUF, ambacho kimeshamteua mwanasiasa mkongwe, Seif Sharrif Hamad kuwania kiti hicho kwa mara ya nne baada ya kuangushwa na Dk Salmin Amour mwaka 1995 na baadaye Rais Amani Abeid Karume mwaka 2000 na 2005.

Kumalizika kwa mchakato huo kunaifanya CCM sasa itue mzigo ulioonekana mzito na itamalizia shughuli za kujiweka sawa kwa uchaguzi mkuu wakati wa mkutano wake mkuu uliopangwa kufanyika leo na kesho kushughulikia mambo mablimbali, ikiwa ni pamoja na kumbariki Rais Jakaya Kikwete kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano.

Harakati za kumpata mgombea wa CCM zilitawaliwa na kila aina ya kampeni, huku Dk Shein akikumbana na rafu hata kabla ya kuja Dodoma baada ya baadhi ya watu kusambaza vipeperushi vilivyokuwa na maandishi yanayohoji uhalali wake wa kusimamishwa na chama kuwania urais.

Dk Shein alidaiwa kuwa hakujiandikisha kupiga kura Zanzibar na hajaishi visiwani humo kwa miezi 36 mfulululizo na hivyo kupoteza sifa ya kuwa mgombea. Hata kabla ya kutulia kwa tuhuma hizo, habari zilienea mjini hapa kuwa makamu huyo wa rais aliwasilisha barua ya kujiengua kwenye kinyang'anyiro hicho.

Lakini jana, Dk Shein alionekana kuwa mtu anayejiamini na alisalimiana na wajumbe wengi waliokuwa eneo la majengo ya ofisi za makao makuu ya CCM, akionekana kutaka kura za kila mjumbe, wakiwemo wauzaji wa nguo za chama hicho ambao hufanya shughuli za nje ya ofisi hizo.

Aliwasili kwenye viwanja hivyo majira ya saa 4:25 asubuhi akiwa na ulinzi mkali na alilakiwa na baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Baada ya kusalimiana na baadhi ya wajumbe na viongozi wa CCM, Dk Shein aliyeonekana kujaa tabasamu, alienda moja kwa moja kwa wanachama na wajumbe wa CCM wa mikoa mbalimbali na kuwasalimia kwa kuwapa mkono.
Kitendo hicho cha Dk Shein kilivuta hisia za  wanaCCM wengi ambao walianza kumkimbilia, kujipanga na kusubiri mkono wake.

Lakini Dk Bilal, ambaye awali alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho baada ya kufanya vizuri mwaka 2000, alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida na mara baada ya kutua kwenye viwanja hivyo aliingia ndani moja kwa moja na baadaye kutoka nje na kuelekea kwenye gari kabla ya kurudi ndani bila ya kuzungumza na mtu yeyote.

Baada ya kushuka kwenye gari, Dk Bilal Bilal aliinua kofia yake ya CCM na kuishusha kuangalia waliopo eneo hilo kuingia moja kwa moja kwenye ukumbi wa mikutano.

Balozi Ali Karume, ambaye ni mdogo wa rais wa Zanzibar, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuingia kwenye viwanja hivyo na alipishana na Dk Shein kwa takriban dakika tatu tu.

Balozi Karume aliwasili viwanjani hapo akisindikizwa na wapambe wake, mkewe na baadhi ya wanafamilia waliovalia sare za CCM. Alisalimiana na baadhi ya wazee wa CCM, akiwamo Dk Shein ambaye alimfuatia.

Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha aliingia baada ya Dk Shein na kupokewa kwa bashasha na vijana wa CCM. Baada ya kusalimiana na baadhi ya wazee, Vuai alienda moja kwa moja kuwapa mkono wanachama waliokusanyika kumsubiri.

Kitendo chake kiliibua shangwe kwa wajumbe na watu wengine ambao walimwimbia nyimbo za kumsifu wakati akisalimiana na watu waliokuwepo kwenye viwanja hivyo.

Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shemhuna aliwasili saa 5:08 akifuatiwa na Mohammed Raza na baadaye Mohammed Yusuph Mshamba aliyeingia moja kwa moja mkutanoni na kutoka baadaye kuonana na waandishi wa habari akiidokeza Mwananchi kuwa ana matarajio ya kuteuliwa.

Haroun Suleiman, ambaye ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, aliwasili eneo hilo lakini muda mfupi baadaye, aliondoka. Hata hivyo, wagombea Mohammed Aboud ambaye ni Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Omar Sheha hawakuonekana katika viwanja hivyo.

Mji wa Dodoma na viunga vyake ulifurika wanachama wa CCM ambao wanatarajiwa kuhudhuria mkutano mkuu utakaompitisha mgombea urais wa chama hicho kesho.

Ujio wa watu hao umefanya nyumba nyingi za kulala wageni kufurika  na watu wengi kukosa mahala pa kulala jambo ambalo pia lilisababisha msuguano baina ya wamiliki wa nyumba hizo na wateja ambao awali walikubaliana kwamba wangehama kuwapisha wajumbe hao.

Awali kikao cha kamati kuu ya CCM kilichofanyika jana mjini hapa kilipitisha majina matatu kati ya 11 walioomba kugombea urais wa Zanzibar.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati alitangaza majina hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao hicho cha kamati kuu
Tags:

0 comments

Post a Comment