Makundi yajipanga upya kwa jaribio jingine 2015
Yadaiwa Dk Bilal hakubaliki kwa Karume
KUINGIA kwa Dk. Ali Mohamed Shein ndiko kulikompa Dk. Mohamed Gharib Bilal nafasi ya Makamu wa Rais kwa maana nyingi, ikiwamo ya kutaka kuzima manung’uniko ya baadhi ya makundi ya wafuasi wake Unguja.
Pamoja na mtizamo huu na mingine mingi, kuna habari pia kwamba Dk.Bilal hakuwa chaguo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, anayemaliza muda wake, Amani Abeid Karume.
Kutokukubalika kwa Dk. Bilal kwa Karume ni jambo ambalo linafahamika wazi. Mwaka 2000 wote walijitokeza kuchukua fomu ya kuwania Urais wa Zanzibar.
Kwa mazingira ya wakati ule, Serikali ikiwa bado chini ya Rais aliyekuwa anamaliza muda wake, Dk. Salmin Amour Juma, ama Komandoo, ambaye Dk. Bilal alikuwa Waziri Kiongozi wake, ilieleweka ni kwa nini Kamati Maalumu ya Zanzibar ilimpitisha kwa alama za juu Dk. Bilal.
Lakini, wagombea wote walipokuja Bara, na kwa kampeni kubwa zilizofanywa na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara marafiki wa Karume walioko Bara, jina la Dk.Bilal halikupita badala yake, Halmashauri Kuu ya CCM ikamtaka Dk. Bilal aondoe jina ili impitishe Karume kuwa mgombea.
Hatua hiyo ya mwaka 2000 ilizua malalamiko ya wazi miongoni mwa wafuasi wa Dk. Bilal, na wengi wao, hawakupata kusahau jambo hilo hadi leo. Na yeye mwenyewe hakupata kusahau.
Ni wakati huo zilipoanza kusikika kauli za kushutumu NEC yenye wajumbe wengi kutoka Bara, kwa maneno kama Tanganyika haiwezi kuendelea kuwachagulia Wazanzibari rais.
Dk.Bilal na wafuasi wake, baada ya kushindwa wakati huo na kukosa nafasi ya kuingiza mgombea wao katika urais mwaka 2005 kutokana na kanuni ya kimya ya CCM kuhusu rais ambaye hajamaliza muda wa miaka 10 wa kikatiba asipingwe, walikaa kimya, huku wakijiandaa kwa 2010.
Wao wakijiandaa, Karume naye alikuwa akijiandaa na kuandaa. Lakini kikubwa akijiandaa kutafuta mtu tofauti na Dk. Bilal. Sababu ni nyingi. Kati ya hizo ni hisia kwamba Dk. Bilal angelipa kisasi cha kutoswa mwaka 2000. Katikati ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu, suala hili la kisasi liliibuka. Lakini Dk. Bilal akajibu kwamba hakutakuwa na kisasi chochote.
Suala jingine linahusiana na uchumi. Katika sura moja, Zanzibar ni eneo dogo kiasi kwamba shughuli yoyote ya uchumi hufahamika kwa urahisi mmiliki wake nani. Inaelezwa kwamba biashara nyingi za Zanzibar sasa ziko mikononi mwa familia na maswahiba wa Karume.
Ni hisia hizi zilizomfanya Rais Karume apachikwe jina la “Hapa Pangu”, kwa maana kwamba ametwaa biashara na maeneo mengi ya biashara. Ni hisia hizi ambazo pia zimewasukuma Wazanzibar wengi kuwaza kwamba Karume hakumpendelea Dk. Bilal kwa vile Dk. Bilal angeweza kuanza kuhoji mambo mengi ya mtu aliyemrithi, zikiwamo mali.
Lakini ukiweka haya pembeni, baadhi ya wafuasi wa Dk. Bilal, na hasa wahafidhina, na hili linaweza kuwa linamhusu Dk. Bilal pia, hawakufurahishwa na hatua ya Karume kutafuta maridhiano na chama kikuu cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kwa Visiwani, taa yake ni Seif Sharif Hamad lakini ambaye kwa hawa ni “ msaliti ” wa Mapinduzi na kwa hiyo kwao kukaa katika serikali moja na CUF ni jambo lisilofikirika.
Hata kama haisemwi wazi, jambo hili la maridhiano lina ukakasi kidogo hata kwa Dk. Bilal mwenyewe na pengine muda ndio utakaotuonyesha misimamo yake halisi mbele ya safari.
Kwamba hatimaye, Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete aliangukia kwa Dk. Bilal ni jambo ambalo lilitarajiwa kwa maana nyingi. Ya kwanza na ya wazi ni “kuwalipa” wafuasi wake ambao kabla ya uteuzi huo walikwisha kuanza kujiapiza kwa kutokumuunga mkono Dk. Shein.
Ifahamike kwamba tofauti za Waunguja na Wapemba linapokuja suala la upigaji kura kuchagua Mpemba au Muunguja ni dhahiri. Hapa hakuna sifa zaidi ya hii. Wangechochewa na ukweli kwamba Dk. Bilal katupwa, Waunguja wengi wahafidhina, wasingempa kura Dk. Shein. Hata pamoja na hatua hiyo nzuri ya Mwenyekiti Kikwete, bado hakuna hakika ya moja kwa moja kwamba Dk. Shein atapita bila kuchubuka.
Lakini sababu nyingine ya kwa nini Kikwete amemchukua Dk. Bilal ni wasifu wa Dk. Bilal mwenyewe. Ingawa kwa hulka yake, ambayo pengine inachangiwa na usomi wake wa fizikia ya kinyuklia ni mtu rigid, yeye ndiye pekee ambaye angefaa katika nafasi hiyo kati ya wale waliojitokeza kuwania urais.
Hata kama Juma Shamuhuna, kwa mfano, ni waziri wa muda mrefu, huwezi kumlinganisha na Dk. Bilal ingawa naye hayuko muda mrefu katika siasa. Hali ni vivyo hivyo kwa Shamshi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi wa sasa ambaye hata Mwenyekiti Kikwete amemtaja kwamba bado ana nafasi baadaye kwa maana ya umri wake.
Wagombea wengine waliosalia, Balozi Ali Karume, Mohamed Raza Dharamshi, Haroun Ali Suleiman, Hamad Bakar Mshindo, Mohammed Yussuf Mshamba, Mohamed Aboud Mohamed, Omar Sheha Mussa, hakika si watu wa ligi moja na Dk. Bilal.
Kwa sababu kadhaa, nafasi ya Makamu wa Rais, na hasa wakati wa Dk.Shein, haikuwa inasikika sana. Ni nafasi nyeti kikatiba. Katiba ya Jamhuri inampa nafasi kubwa Makamu wa Rais, ikitokea ambayo wote hatuyatarajii, Rais akashindwa kuendesha Taasisi ya Urais, Makamu wa Rais anakuwa Rais.
Kwa wote walioomba urais wa Zanzibar, ambao, kwa maana hiyo, wangeweza kufikiriwa katika nafasi ya Makamu, hakuna wa kumshinda Dk. Bilal kwa sifa ya kukalia kiti cha Rais ikibidi, walau kwa muda.
Kuna taarifa, kama ilivyo kawaida ya CCM, kwamba kabla ya jina la Dk. Bilal kupita, ulitafutwa ushauri kwa maana hiyohiyo ya uwezekano wa yeye kukalia madaraka ya juu kabisa ya nchi likitokea la kutokea. Wengi waliopata nafasi ya kushauri walimtaja Dk. Bilal.
Hafahamiki sana ana msimamo upi juu ya Muungano, lakini taarifa zinasema hilo ni kati ya mambo ambayo yalitazamwa hata kabla ya Kikwete na Karume kuafikiana.
Yeye mwenyewe, akizungumza katika hafla ya kumtambulisha katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma juzi Jumatatu, aliahidi mambo mengi likiwamo la kumsindikiza Dk. Shein hadi katika ushindi.
Akizungumzia uwezo wa Dk. Bilal baada ya kumtangaza Jumapili iliyopita kuwa mgombea mwenza wake Kikwete alisema: “ Sina shaka kabisa kwa sifa zake, uzoefu wake na ukomavu wake kisiasa. Atakitetea vyema chama chetu katika kampeni na kumudu vyema mamlaka na majukumu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati safari ya Dk. Bilal ya hatimaye kufika hapa alipofika ikionekana kusuasua tangu mwanzo, safari ya Dk. Shein iliandaliwa muda mrefu. Kuna taarifa kwamba mpango huo unarudi nyuma hadi miaka mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kwa nia ya kupata mtu ambaye angeweza kusaidia kumaliza mivutano isiyo na tija kwa Zanzibar, inayojielekeza katika sura ya uhasama baina ya wana CCM na wana CUF, jopo la watu kadhaa kutoka Pemba na Unguja lilianza mchakato wa nani wa kumrithi Karume ambaye asingekuwa na makundi.
Liliwasiliana na Rais Kikwete kwa maana hiyo. Akalirudisha kwa Dk. Shein mwenyewe. Lilipokwenda kwa Dk. Shein akalirudisha kwa Rais Kikwete kwa maana kwamba Rais ndiye wakati huo alikuwa bosi wake asingeweza kufanya uamuzi wa jambo kubwa kama hilo bila ridhaa ya Rais.
Hata alipoambiwa kwamba tayari Rais Kikwete alikuwa amefahamishwa jambo hilo, Dk. Shein anaelezwa kusisitiza kwamba mpaka yeye mwenyewe azungumze na bosi wake. Baadaye, taarifa zinasema, alikubali.
Lakini hata ukiacha hili, yeye mwenyewe alikuwa hajioni kuwa mwanasiasa wa kiwango cha kushika madaraka makubwa kabisa ya Zanzibar katika hali ya kisiasa iliyokuwapo.
Akizungumza Jumapili mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kutambulishwa, Dk. Shein alisema alikuwa anakusudia kuendesha kampeni za kiungwana, zisizo za matusi na kwamba atawaunganisha Wazanzibari wote kwa nia ya kuleta maendeleo zaidi Visiwani.
Akimzungumzia Dk. Shein, Kikwete alisema: “ Naomba kuchukua fursa hii kumpongeza Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa kuwa mgombea wa CCM kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar. Kulikuwa na wagombea kumi na moja kwenye nafasi hiyo, tena watu makini wenye sifa za kuongoza. Lakini kama ilivyo kawaida ya uchaguzi tatizo mara nyingi si ubora wa sifa za wanaoomba nafasi hizi za juu, tatizo ni kwamba lazima tuchague mmoja. Hawatapata wote bali atapata mmoja na safari hii ni Dk. Ali Mohamed Shein. Wengine ni hazina ya Chama chetu na nchi yetu, na tutaendelea kuwatumia.
“Dk. Ali Mohamed Shein ni kiongozi makini, mtulivu na mwadilifu. Mwana-CCM aliyeiva, kiongozi anayepima mambo, anayeipenda nchi yake na watu wake; kiongozi anayefadhaishwa na umasikini wa wananchi wenzake, mwenye mawazo mazuri ya maendeleo, na kiongozi mpenda ushirikiano, mpenda Muungano na mpenda amani. Nina imani na uwezo wake wa kuwaunganisha Wazanzibari wote – wa visiwa vyote na wa vyama vyote. Nina hakika tutafanya naye kazi vizuri kwa maslahi ya chama chetu, Muungano wetu, na kwa maslahi ya wana-CCM na Watanzania wote.
Tutasubiri kuona ni vipi uteuzi huo wa CCM utakwenda katika Uchaguzi Mkuu ujao, lakini akimzungumzia Dk. Shein, mshindani mwenzake katika nafasi ya Urais wa Zanzibar, Seif alisema: “Nampongeza kwa dhati Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kuwa mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM. Ushindi wa kura 117 ni ushahidi wa wazi wa imani waliyo nayo viongozi wenzake ndani ya CCM kwake na kwa uwezo wake wa uongozi.
“Binafsi nimeupokea uteuzi huu kwa furaha kwa sababu naamini kwamba Dk. Shein ni mtu makini, msomi, mwenye uwezo,busara na hekima na asiyependa makuu. Kutokana na sifa hizo, naamini baada ya uteuzi wake ataweza kuwaunganisha wana-CCM wote warudi kuwa kitu kimoja ili kupata umoja ndani ya chama chao na hatimaye kwa kushirikiana na sisi katika CUF kujenga umoja mpana zaidi ndani ya Zanzibar kwa kushirikisha vyama vyote vya siasa.
“Nimetiwa moyo sana na kauli yake thabiti kwamba anayaunga mkono Maridhiano tuliyoyaanzisha mimi na Rais Amani Karume na kwamba pindi akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atayaendeleza na kuyaimarisha.
“Naamini Dk. Shein ni kiongozi ambaye kwa hulka yake tutaweza kushirikiana kuwaunganisha Wazanzibari wote na kuwaongoza katika kuleta siasa mpya za maelewano na mashirikiano ambazo zitatupa fursa ya kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo makubwa na ya haraka katika kunyanyua hali zao za maisha.
“Tuna bahati kwamba Rais anayemaliza kipindi chake, Amani Karume, ameijengea Zanzibar misingi mizuri ya maendeleo ambayo naamini tutaweza kuitumia vyema katika kutekeleza sera zaidi zitakazolenga kujenga uchumi wa kisasa utakaotoa ajira na fursa tele kwa watu wetu na hivyo kuleta utajiri na neema kwa nchi yetu na watu wake.
“Nataka nimhakikishie Dk. Shein kwamba na mimi pia naiamini na nitaisimamia kwa dhati misingi hiyo hiyo ambayo naamini yeye anaikubali. Kwa pamoja, tutaibadilisha sura ya Zanzibar ili iendelee kuwa nchi ya mfano kwa maendeleo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
“Ni matarajio yangu kuwa Dk. Shein atashirikiana na mimi na Rais Amani Karume katika kampeni za kuwaomba Wazanzibari wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika kura ya maoni Julai 31 kwa kupiga kura ya ndiyo kuunga mkono muundo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Wananchi wakiridhia, na mimi naamini wataridhia kwa asilimia kubwa sana, basi yeyote atakayeshinda kati yangu mimi na yeye Dk. Shein atakuwa amepata ridhaa safi ya kushirikiana na mwenzake katika kuiongoza Zanzibar mpya.
“Baada ya hapo, ni matumaini yangu pia kwamba wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu ukifika, tutakuwa na kampeni za kistaarabu, kampeni ambazo hazitakuwa na malumbano, matusi wala stihizai ili kujenga misingi ya mashirikiano baada ya uchaguzi. Mkiwa na uhasama katika kampeni mnajenga chuki na hivyo mashirikiano yatakuwa yametiwa shubiri.”
Huu ni mtihani wa kwanza kwa Dk. Shein na CCM kwa ujumla, mtihani wa pili ni kati yake na Seif. Kama atavuka mtihani wa pili, basi mtihani wake wa tatu ni kuongoza Serikali ya Pamoja kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake na historia ya Zanzibar, historia ambayo hata hivyo, itategemea sana kura za maoni ya wananchi kama wataridhia Serikali ya Pamoja.
Vyovyote itakavyokuwa, kura hiyo ya maoni, takriban wiki mbili zijazo inaweza kuzua hamasa mpya kabla ya upigaji kura kumsaka Rais wa Visiwa Oktoba 31, mwaka huu.
Kwa ujumla viongozi wakuu wa nchi, Kikwete na Karume walikuwa makini katika kuzipima siasa za Zanzibar na walimuona Shein kama mtu atakayeweza kuwavusha kuelekea maridhiano ya Kitaifa kwa njia ya wastani bila kuwakera wana CCM wenzao na bila kuzuia juhudi zilizoanzishwa katika kuzungumza na wapinzani wakuu visiwani wa CUF.
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba Dk. Shein akishinda katika uchaguzi wa mwaka huu atakuwa Rais wa kipindi kimoja tu (one term President), kwa sababu mbalimbali zikiwamo zile zinazohusiana na joto la uchaguzi wa mwaka 2015 kwa bara na hata Zanzibar ambako kuna dalili za kuwapo mabadiliko.

0 comments