IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Elias Msuya
CHAMA cha Jamii (CCJ) kimesema kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ataanza kuhakiki wanachama wake wa jijini Dar es salaam kesho, huku kikitamba kuwa kina mgombea urais ambaye ni maarufu kuliko Rais Kikwete.
Uhakiki huo unafanyika ili Msajili aweze kutoa usajili wa kudumu na hivyo kukiwezesha kwa chama hicho, ambacho kilianzishwa kwa kishindo kikuu hasa kutokaa na habari kuwa kinaungwa mkono na vigogo wengi, kushiriki uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
“Tunao madiwani, wabunge na mgombea wa juu kabisa wa urais, tena atakuwa maarufu kuliko Kikwete,” alisema mwenyekiti wa CCJ, Richard Kiabo katika mkutano na waandishi wa habari alioutisha jana.
"Tumejiandaa vyema kwa uchaguzi katika ngazi zote ikiwemo hiyo ya urais."
Kama kawaida yake, Kiyabo hakutaka kufafanua zaidi kuhusu viongozi hao wala kudokeza juu ya mgombea waliyemuandaa wa nafasi ya urais, lakini naibu katibu mkuu wa CCJ alitangaza jana nia ya kugombea ubunge wa jimbo la Temeke, akisema hata chama hicho kisiposajiliwa, ataingia kwenye kinyang'anyiro akiwa mgombea binafsi.
Kiyabo, ambaye alikuwa akiongea na waandishi kwenye ofisi za makao makuu ya CCJ, alisema kuwa Msajili amewapangia ratiba inayoanza kesho ili kuhakiki wanachama wa chama hicho kipya cha kisiasa.
Kwa sheria ya usajili wa vyama vya siasa, CCJ inatakiwa iwe na wanachama angalau kwenye angalau mikoa 10 ili kiweze kupata usajili wa kudumu ambao utakiwezesha kushiriki uchaguzi mkuu.
“Uhakiki utaanza Juni 3 mkoani Dar es Salaam; Juni 4 watakwenda mkoa wa Pwani ukifuatia na mkoa wa Morogoro Juni 5 na mwisho watakwenda Visiwani Zanzibar,” alisema Kiyabo.
Aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kufika kwa wingi kwenye viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke kwa ajili ya uhakiki huo akisema kuwa utakuwa wa kihistoria,
“Tunawaomba wanachama wetu wafike kwa wingi; kutakuwa na mbwembwe nyingi... itakuwa ni historia,” alisema Kiyabo.
Kiyabo pia alisisitiza kuwa chama chao kimejiandaa vyema na uchaguzi tangu ngazi ya udiwani, Ubunge na Urais, “Tunao madiwani, wabunge na mgombea wa juu kabisa wa urais, tena atakuwa maarufu kuliko Kikwete” alisema Kiyabo.
Kulikuwa na habari kuwa Msajili John Tendwa jana angetoa taarifa, lakini waandishi walipokwenda ofisini kwake walikuta akiondoka na hakueleza kama ameahirisha kutoa taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa ya CCJ kuwa Tendwa amekubali kuanza kukihakiki chama hicho linapingana na kauli iliyotolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Masuala ya Bunge), Phillip Marmo ambaye alikitaka chama hicho kutomtwisha lawama Msajili kwa madai kuwa ombi lao la kusajili chama limetolewa wakati bajeti imeshaisha.
"Tunapomlaumu Msajili wa Vyama vya Siasa kuchelewa kuisajili CCJ wakati mwingine hatumtendei haki kwa kuwa mwaka huu vyama vipya sita vilivyoomba usajili havikutoa taarifa mapema kwa msajili wakati tunaandaa bajeti.
Naelewa CCJ wamepeleka maombi wakati msajili akiwa na kazi nyingine," alisema Marmo huku akishangaa sababu za chama hicho kupatiwa usajili wa muda licha ya kuwa cha tano kuomba usajili.
Lakini jana, viongozi wa chama hicho walimtaka Marmo kuacha kuzungumzia masuala la usajili wa chama CCJ akisema kuwa waziri huyo hahusiki kwenye kazi hiyo ambayo alisema kuwa ni ya Tendwa.
"Tulikutana na Msajili juzi saa 8:00 mchana na akatupangia ratiba ya kufanya uhakiki, hivyo maneno ya Marmo hayana msingi," alisema Kiyabo.
“Marmo anapaswa kuogopwa kama ukoma… hatafakari kabla ya kuzungumza. Sisi hatufanyi kazi na Marmo, tunazungumza na Tendwa. Hata hizi tarehe za uhakiki na mikoa tutakayoanza amepanga yeye,” alisema Dickson Mhiri ambaye ni Naibu katibu mkuu wa CCJ.
Katibu mkuu wa chama hicho, Renatus Muabhi alisema kuwa Mei 31 walipokuwa kwenye harakati za kwenda mahakamani kufungua kesi, walipata simu kutoka kwa Msajili akiwataka wafike ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo.
Alidaio kuwa Tendwa aliwaomba radhi kwa kauli kuhusu usajili wa chama hicho, akisema kuwa zimeibua tafsiri mbaya kwa jamii na kwa chama hicho.
“Tulipokwenda kule tuliingia mimi na mwenyekiti tu; tena Tendwa alisema tusiende na waandishi wa habari. Kwanza alituomba radhi kwa kauli zake kuwa hana fedha za kuhakiki wanachama wetu,” alisema.
Alidai kuwa Tendwa alionyesha unyeyekevu na kwamba alijutia kauli zake hasa kutokana na baadhi ya magazeti kutoa namba yake na kusababisha zaidi ya watu 300 kumtumiwa ujumbe mfupi wa simu kumlaumu.
Alisema kuwa kitendo cha Marmo kupinga usajili wa chama chao kinaonyesha jinsi ambavyo watumishi wa serikali ya CCM wasivyo na mawasiliano baina yao.
“Wakati Tendwa anatupangia ratiba ya uhakiki wa chama chetu, Marmo anasema kuwa chama chetu hakitasajiliwa. Hii ni kuonyesha kuwa serikali hii haina mawasiliano mazuri kwa watumishi wake. Wananchi wanashindwa kuielewa washike la nani,” alisema Muabhi.
Katika hatua nyingine, naibu katibu mkuu wa CCJ, Dickson Mhiri ametangaza nia ya kugombea ubunge wa jimbo la Temeke.
Alisema kuwa hata chama hicho kisiposajiliwa, ana uhakika wa kugombea kiti hicho akiwa mgombea huru.
“Nitamvaa Mtemvu wa Temeke. Pamoja na kwamba chama chetu hakijasajiliwa rasmi, naamini mambo yatakwenda vizuri. Hata ikishindikana nitagombea tu, kwanza si mnajua kesi ya mgombea binafsi inaendelea,” alisema Mhiiri.
You Are Here: Home - - CCJ: Mgombea wetu ni maarufu kuliko Kikwete
0 comments