Bunge la shirikisho Bundestag na baraza la wawaklilishi wa mikoa-Bundesrat yanatazamiwa kuamua hii leo kuhusu mchango wa Ujerumani katika mpango wa Euro bilioni 750 wa kuinusuru sarafu ya Euro.Upande wa upinzani unashauri zoezi la kuupigia kura mpango huo liakhirishwe.
Licha ya ubishi wa upande wa upinzani taasisi hizo mbili-bunge la shirikisho-Bundestag na baraza la wawakilishi wa mikoa-Bundesrat zinatarajiwa kuupitisha mpango huo wa kuiokoa sarafu ya Euro ulioandaliwa wiki mbili zilizopita.Mchango wa Ujerumani unafikia Euro bilioni 148.Kiwango hicho kinatajikana kuwa kikubwa zaidi kulinganishwa na michango ya wanachama wengine wa zoni ya Euro.Sauti zimeshaanza kupazwa kutoka kila upande.Mwenyekiti wa kundi la wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU katika bunge la shirikisho Bundestag-Peter Altmeier amesema kupitia kituo cha matangazo cha Deutschlandfunk,hii leo,"anaamini fika mpango huo utaidhinishwa kwa wingi wa kura kutoka vyama vinavyounda serikali ya muungano wa nyeusi na manjano."
CDU/CSU na FDP wanajivunia wingi wa kura moja tuu.Serikali ya muungano inayoongozwa na kansela Angela Merkel ina wingi wa kura 312 toka jumla ya kura 622.Wabunge tisaa wa vyama ndugu vya CDU/CSU wanapanga ama kuupinga mpango huo wa mabilioni ya Euro au kutopiga kura upande wowote.Na kwa mujibu wa gazeti la Bild wabunge wasiopungua sita wa kutoka chama cha FDP wanapanga pia kutoupigia kura mpango huo.
Upande wa upinzani wa SPD na walinzi wa mazingira wameshasema ama watapinga au watajizuwia kupiga kura.Wanahoji ingekua vyema kama kama uamuzi huo ungeakhirishwa hadi upatikane muongozo wa Umoja wa Ulaya.
Mwenyekiti wa kundi la wabunge wa chama cha walinzi wa mazingira Die Grüne Jürgen Trittin anasema:
"Zaidi ya hayo,hakuna haja ya kufanya haraka kama ilivyokua katika kadhia ya Ugiriki.Bunge la Ufaransa litaamua mwezi June sawa na Hispania.Na Luxembourg hata bado hawajapanga lini."
Wafuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa shoto Die Linke wameshasema wataupinga mpango huo.
Naibu mwenyekiti wa kundi la vyama ndugu vya CDU/CSU bungeni,Michael Meier ameutolea mwito kwa mara nyengine tena upande wa upinzani na hasa SPD wawajibike ipasavyo ."Ni muhimu kuidhinisha mpango huo ili kuhifadhi sarafu ya Euro"-amesema Michael Meier.
0 comments