Kiongozi wa kundi kuu la waasi amezuiliwa kuingia Chad wakati akitokea Libya kuelekea Sudan.
Kiongozi wa Justice and Equality Movement (Jem) Khalil Ibrahim aliambiwa arudi Libya alipofika uwanja wa ndege wa Chad.
Afisa mwandamizi wa Jem ameiambia BBC kwamba Chad inajaribu kuwashinikiza kuanza upya mazungumzo ya amani na Sudan.
Jem imekuwa na uhusiano mzuri na Chad, lakini mambo yamebadilika katika miezi ya hivi karibuni baada ya uhusiano baina ya Chad na Sudan kuimarika.
Hati za kusafiria za Bw Ibrahim na wafuasi wengine wa Jem zimetaifishwa na kiongozi huyo kwa sasa yupo uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena.
Mwenyekiti wa baraza la bunge la Jem, Eltahir Adam Elfaki ameiambia BBC kwamba hatua hiyo ya Chad haikuwashangaza.
Amesema "Mara nyingi tumekuwa tukitia shaka,"
"Mara nyingi huwa tunatia shaka kwamba mazungumzo yanayofanyika kwa faragha yataathiri uhusiano [baina ya Jem na Chad]."
Kurejesheana uhusiano
Nyakati za nyuma, mara nyingi Jem imekuwa ikiweka majeshi yake nchini Chad na ilikuwa ndio njia ya kupita maafisa.
Lakini mwezi Februari, Rais wa Chad Idriss Deby alikubaliana na Rais wa Sudan Omar al-Bashir kuacha kuwaunga mkono waasi katika nchi zote mbili.
Sudan kwa muda mrefu imekuwa ikiilaumu Chad kwa kuwaunga mkono waasi Darfur, wakati mwaka 2008, Chad imeishutumu Sudan kwa kulisaidia kundi moja la waasi ambalo lilikaribia kufika N'Djamena, kabla ya kushambuliwa.
Haijajulikana kwanini Bw Ibrahim alikuwa anasafiri kutoka Libya kuelekea Chad.
Baada ya kutia saini makubaliano mwezi Februari, Jem iliambiwa kwamba haikaribishwi tena Chad.
Na baadhi ya waangalizi wanaamini hatua ya Chad kukataa kumkaribisha Bw Ibrahim ni dalili kuwa Rais Deby ana nia ya kuheshimu makubaliano yake na Sudan.
Jem ilitia saini wa kusimamisha mapigano na serikali ya Sudan mwezi Februari, lakini mapema mwezi huu ilisusia mazungumzo ya amani yaliokuwa yakifanyika Qatar, ikidai serikali imeanzisha mgogoro upya.
0 comments