Baadhi ya watuhumiwa wa kesi ya wizi wa Sh 207 milioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) wakijadiliana jambo kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, mara baada ya kesi yao kuahirishwa kutoka (kushoto kizimbani), Farijala Hussen, Bosco Kimela, Iman Mwakyusa na Ester Komu, pamoja na Rajabu Maranda aliyesimama nje ya kizimbai. |
UPANDE utetezi katika kesi ya wizi wa Sh 207 milioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki kuu ya Tanzania (BoT), inayomkabili wafanyakazi watatu wa benki hiyo, akiwemo Bosco Kimela, umewasilisha pingamizi la kisheria kuomba wateja wao wafutiwe mashtaka yanayowakabili kwa madai kuwa wanakinga kisheria.
Pingamizi hilo, liliwasilishwa jana na Wakili Mpale Mpoki mbele ya jopo la mahakimu watatu wanaoisikiliza kesi hiyo, lililokuwa likongozwa na Hakimu Ignas Kitus katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kwa mujibu wa Wakili Mpoki, mahakama hiyo, haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo, kwa sababu sheria ya BoT inazuia wafanyakazi na wajumbe wa bodi kufunguliwa kesi yoyote ya madai.
Wengine ni Imani Mwaposya na Ester Komu ambao wanadaiwa kuwa kati ya mwaka 2003 na 2005 wakiwa waajiriwa wa BoT waliibia benki hiyo, kiasi hicho cha fedha.
Akiwasilisha ombi hilo, wakili Mpoki alidai kifungu cha 69 cha sheria namba 5 ya 2006 ya BoT kinazuia watumishi wake na wajumbe wa bodi kufunguliwa kesi za jinai au za madai katika shughuli zao za kikazi.
Alifafanua kuwa kwa sababu kifungu hicho kimetumia neno (Shall) ni rai yao kuwa washtakiwa hao wanakinga ya kisheria ya kutokushtakiwa kwa sababu haijaondolewa hivyo aliongeza kuwa mahakama hiyo ya kisutu kuendelea kusikiliza kesi hiyo, itakuwa imekiuka taratibu za kisheria hivyo aliiomba mahakama hiyo, iondoe au kufuta mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Hoja hiyo ilipingwa na upande wa serikali na wakili Mkuu wa serikali, Boniface Stanslaus alidai pingamizi hilo, halina msingi kwa kuwa mashtaka yanayowakabili watuhumiwa hao yanaangukia kati ya Julai 2004 na Agosti 2005 na kwamba sheria aliyoinukuu wakili Mpoki ilitungwa mwaka 2006 hivyo haiwezekani hata kidogo sheria hiyo, ikatumika.
Wakili Stanslaus alisema sheria inayoweza kutumika ni ya mwaka 1995 na kwamba sheria ya BoT inatoa kinga kwa wafanyakazi wake na wajumbe wa bodi katika mambo waliyoyafanya kwa nia njema kwa kuzingatia sheria.
Alidai pingamizi kama hilo, liliwasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Septemba 18, mwaka jana na likakataliwa na kwamba jana lilipelekwa katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kuchelewesha kesi.
Hata hivyo hoja hizo za serikali zilipingwa na upande wa utetezi na Wakili Mpoki alidai kuwa ni kweli matukio hayo, yalitokea kati ya mwaka 2004 na 2005 na kuongeza kuwa katika hali ya kawaida wasingeweza kuwasilisha maombi yao ya kinga kwa sheria ambayo haipo na kwamba wamewasilisha ombi hilo, wakiomba kupitia sheria hai.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na mwenzake Farijala Hussein ambao hawahusiki na pingamizi hilo kutokana na kutokuwa wafanyakazi wa BoT.
Maranda na Farijala wanadaiwa kuwa kati ya mwaka 2003 na 2005, walikula njama na kuiibia BoT zaidi ya Sh 207 milioni baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Russias T Ltd imepewa deni na kampuni ya General Marketing ya nchini India. Uamuzi wa hoja hizo utatolewa leo.
0 comments