Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wagonjwa wa mafua ya nguruwe wafikia 600

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

HALI ya ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe nchini ni mbaya baada ya serikali kueleza kuwa watu 599 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo, kati yao 488 wakiwa Watanzania.

Hadi juzi Mkoa wa Manyara ulikuwa unaongoza kutokana na Wilaya ya Mbulu kuwa na wagonjwa 384, Dar es salaam (197), Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza (14) na Mara wanne.

Hata hivyo, mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Meshack Massi aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa Shule ya Msingi ya Ilula iliyo wilayani Kwimba imefungwa na kugeuzwa wodi baada ya wanafunzi wake 120, walimu watano na wanakijiji 17 kugundulika kuwa na homa ya mafua ya nguruwe.

Alisema uamuzi wa kufungwa kwa shule hiyo ulifikiwa baada ya majibu ya vipimo ambavyo vilichukuliwa kutoka kwa wanafunzi 56 wa shule hiyo, kuonyesha kuwa na vimelea vya ugonjwa huo hatari.

Jana kaimu katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Deo Mtasiwa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa idadi ya wagonjwa 599 imetokana na majibu ya sampuli za vipimo 1,390 vilivyochukuliwa kutoka kwa watu 512 waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo.

"Kutokana na vipimo hivyo, idadi ya wagonjwa waliothibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo hatari (positive) ni 599 huku waliopimwa lakini hawakuwa na ugonjwa huo wakiwa 791," alisema.

Hata hivyo, alisema idadi ya wagonjwa waliolazwa katika makambi maalumu kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa huo ni 40 na mmoja amefariki dunia.

“Hadi kufikia jana (juzi) idadi ya wagonjwa waliothibitika kuwa na ugonjwa huu hapa nchini ni 599. Kati ya wagonjwa hao 488 ni Watanzania. Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa na wagonjwa 197 na Mara wagonjwa wanne huku Wilaya ya Mbulu ikiwa na wagonjwa 384, na Kwimba 14,” alisema Dk Mtasiwa.

Kutokana na tishio hilo, alisema serikali imeamua kuteua Wilaya ya Kwimba kuwa kambi maalumu kwa wagonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe na kwamba hadi sasa kuna wagonjwa 40.

Dk Mtasiwa alifafanua kwamba katika mkoa wa Dar es Salaam idadi ya watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo ni 663 na idadi ya vipimo vilivyochukuliwa ni 663, lakini waliothibitika kuugua ni 197 na 4,466 hawakuwa na ugonjwa huo na majibu ya wengine wanne yakiwa hayajatolewa.

Katika mkoa wa Mara, idadi ya watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo ni 16 na idadi ya vipimo vilivyochukuliwa ni 16 na waliothibitika kuugua ni wanne wakati 12 hawakukutwa na ugonjwa huo.

Aidha katika Wilaya ya Mbulu, idadi ya watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo ni 691 na idadi ya vipimo vilivyochukuliwa ni 687 na waliothibitika kuugua ni 384.

Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza idadi ya watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo ni 142 na idadi ya vipimo vilivyochukuliwa ni 24 na waliothibitika kuugua ni 14 na 10 hawakuwa na ugonjwa huo.

"Pamoja na mambo mengine hatua zilizokwishachukuliwa wilayani Kwimba ni kupeleka dawa aina ya tamiflu, tumepeleka vifaa kinga na vifaa vya maabara kwa ajili ya kuchukulia sampuli pamoja na kusitisha magulio yote yaliyokuwa karibu na maeneo ya mlipuko," alisema Dk Mtasiwa.

Alisema kutokana na tatizo hilo kuwakumba wanakijiji wengi, kijiji cha Ilula ambacho kipo kando ya barabara kuu iendayo Shinyanga, kimewekwa chini ya uangalizi maalumu.

Juzi Shule ya Msingi ya Ilula iliyo wilayani Kwimba ilifungwa na kugeuzwa wodi baada ya wanafunzi wake 120 na walimu kadhaa kuugua ugonjwa huo.

Hata hivyo, hadi jana wagonjwa 100 kati ya 142 walioripotiwa kufikishwa katika shule hiyo kwa matibabu, waliruhusiwa kuondoka baada ya kupatiwa matibabu.

Dk Mtasiwa, ambaye pia ni mganga mkuu wa serikali alisema hadi jana wagonjwa 40 tu ndio waliobaki kwenye kituo hicho.

Alisema wagonjwa wengine waliokuwa wamelazwa tangu juzi waliruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu na afya zao kuendelea vizuri.

Aliongeza kuwa Wizara inaendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, dalili za awali za kutambua ugonjwa huo ili kuzuia maambukizi zaidi.

"Hadi sasa (jana) wamebaki wagonjwa 40 ambao wako confined (wamezuiwa) na wanaendelea kupata matibabu, lakini wengine wameshapatiwa matibabu na wameruhusiwa kuondoka," alisema Dk Mutasiwa.

Hofu ya kusambaa kwa maambukizo hayo kuingia katika mikoa ya jirani imekuwa kubwa kutokana na wananchi kuingia katika kijiji cha Ilula na kutoka huku wengine wakipanda mabasi ya abiria toka kijijini hapo kwenda mkoani Shinyanga au Mara bila ya kuwa na uangalizi wowote.

"Akiambukizwa konda wa daladala moja tu tumekwisha," alisema mkazi mmoja wa Kilima Hewa jijini Mwanza, Emmanuel Masato.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Meshack Massi alithibitisha kuwepo kwa uwezekano wa ugonjwa huo kusambaa kutokana na wanakijiji kuingiliana na watu wa mikoa jirani na kwamba mpaka jana wanakijiji hao walikuwa wakiendelea na shughuli zao na kwenda katika kijiji cha Nyasamba kilichopo mkoani Shinyanga kwa ajili ya soko, hali ambayo alieleza kuwa inaweza kuchangia kusambaa kwa ugonjwa huo.

"Tunadhani hilo linawezekana, lakini tumeanza jana na mkuu wa wilaya kufanya mikutano ya hadhara kuwaeleza wananchi juu ya ugonjwa huu, dalili zake na njia za kujikinga, lakini wananchi wa hapa Ilula wamekuwa wakienda kwenye mnada kijiji cha Nyasamba mkoani Shiyanga, wanaweza kuufikisha huko," alieleza.

"Wanakijiji wametueleza jana kuwa watoto wao wamekuwa wakisimama kando ya barabara na kuomba chupa za maji kwa wasafiri wapitao na mabasi, jambo hili pia ni hatari kwa sababu linaweza kusababisha maambukizo kufika kijijini hapo," alieleza.

Baadhi ya wanakijiji wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti walieleza kuwa ugonjwa huo unaweza kusambaa kwenda maeneo mengine toka kijijini kwao kwa vile baadhi ya vijana na mabinti wamekuwa wakienda machimboni katika migodi ya dhahabu kijiji cha Mwanangwa kujitafutia kipato.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Christopher Kangoye alisema kuwa mpaka jana walikuwa wamefanikiwa kufikisha magodoro 60 kwenye shule hiyo na kuandaa utaratibu wa waliolazwa shuleni hapo kupatiwa chakula.

Taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo nchini zilianza wakati iliporipotiwa kuwa mtu mmoja kutoka barani Ulaya alibainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo. Hata hivyo, mtu huyo ambaye alilazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) aliruhusiwa kuondoka kwa maelezo kuwa alishatibiwa.

Baadaye, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitangaza kuwa watu 170 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo na kueleza kuwa wengi walioambukizwa ni wanafunzi ambao ilielezwa kuwa ni rahisi kwao kuambukizwa ugonjwa huo.

Wizara ilisema katika taarifa yake kuwa imeimarisha mfumo wa ukaguzi kwenye viwanja vya ndege kwa ajili ya kudhibiti wasafiri wanaoingia nchini, lakini hali inaonekana kuendelea kuwa mbaya.

Habari hii imeandaliwa na Frederick Katulanda, Mwanza, Sadick Mtulya na Claud Mshana, Dar

Tags:

0 comments

Post a Comment