Ratiba ya robo fainali
Jumatano na Alhamisi ni mapumziko kwenye Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini kufuatia kumalizika kwa raundi ya pili ya michuano hiyo.
Orodha ya timu nane bora zilizofuzu kwa robo fainali ilikamilika baada ya mechi za mwisho za raundi ya pili zilipochezwa Jumanne.
Nafasi mbili za mwisho za robo fainali zilichukuliwa na Paraguay na Uhispania kufuatia ushindi dhidi ya Japan na Ureno.
Paraguay ilipata ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Japan kupitia mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare 0-0 katika muda wa kawaida na pia muda wa ziada, kwenye uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria.
Tuta la Yuichi Komano wa Japan liligonga mwamba huku Paraguay wakifanikiwa kufunga penalti zao zote.
Uhispania ilifanikiwa kuifunga Ureno bao 1-0 katika uwanja wa Green Point mjini Cape Town, bao lililofungwa na David Villa katika dakika ya 68.
Sasa Uhispania inasubiri kuchuana na Paraguay katika robo fainali.
Mechi ya kwanza ya robo fainali siku ya Ijumaa itakuwa kati ya mabingwa mara tano Brazil na Uholanzi katika uwanja wa Nelson Mandela Bay, mjini Port Elizabeth.
Robo fainali nyingine siku hiyo ya Ijumaa itakuwa kati ya Ghana na Uruguay katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg, hii ikiwa ni mara ya tatu katika historia ya Kombe la dunia kwa timu kutoka Afrika kufikia hatua ya nane bora.
Itakuwa ni fursa nyingine ya wapenzi wa soka barani Afrika kuungana tena kuishabikia Ghana, kama ilivyofanyika wakati wa mchuano kati ya Black Stars na Marekani.
Siku ya Jumamosi itafanyika robo fainali ya tatu kati ya Ujerumani na Argentina katika uwanja wa Green Point, mjini Cape Town.
Paraguay na Uhispania zitachuana katika robo fainali ya mwisho siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Ellis Park, mjini Johannesburg.
Nusu fainali zitachezwa Jumanne na Jumatano wiki ijayo mjini Cape Town na Durban.
Mshindi wa tatu atafahamika Jumamosi tarehe 10 zitakapokutana timu mbili ambazo zitakuwa zimepoteza kwenye nusu fainali.
Jumapili tarehe 11 ndio fainali itafanyika katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg na bingwa mpya wa dunia kutawazwa.
Mechi za robo fainali zinazotazamiwa kuwa ngumu zaidi ni ile kati ya Brazil na Uholanzi siku ya Ijumaa, na pia Ujerumani dhidi ya Argentina siku ya Jumamosi.
Brazil wameonyesha azma ya kulitwaa kombe hilo kwa mara ya sita katika mechi ambazo wamecheza, lakini Uholanzi nao wanapania kumaliza kiu ya miaka mingi ya kombe hilo, baada ya kucheza fainali mara mbili bila mafanikio.
0 comments