Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Chadema waiteka Mwanza

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAMTAKA JK KUTOA TAMKO KUHUSU UFISADI, DOWANS NA HALI YA NGUMU YA MAISHA
Frederick Katulanda na Sheila Seizzy, Mwanza
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kililiteka Jiji la Mwanza, pale viongozi wake wa kitaifa walipoongoza maelfu ya waandamanaji katika Jiji hilo.Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa na wabunge kadhaa waliowaongoza maelefu ya wandamanaji katika kile walichosema kuwa ni kupinga kupanda kwa gharama za maisha, malipo kwa Kampuni ya Dowans na kupanda kwa gharama za umeme.

Katika mkututano wa hadhara uliohitimishwa katika Viwanja vya Furahisha, Dk Slaa alitoa siku tisa kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli kuhusu kushamiri kwa vietndo vya ufisadi, malipo ya Dowans na suluhisho la kupanda kwa gharama za maisha kwa Watanzania.

Dk Slaa alisema iwapo Serikali itakaa kimya basi Chadema kitaitisha maandamano ya nchi nzima ili kushinikiza mabadiko kama ilivyo katika nchi za Misri na Tunisia.

Alisema kitendo cha Rais Kikwete kuendelea kukaa kimya kitasababisha Chadema kuchukua hatua ya pili ambayo wataitisha maandamano nchi nzima.

Kabla ya mkutano huo, kulikuwa na maandamano yaliyoanzia katika Uwanja wa Shule ya Msingi Buzuruga na kupita katika Barabara za Nyerere, Pamba na kuingia Barabara ya Kenyatta na ile ya Uwanja wa Ndege na kuhitimishwa katika Uwanja wa Furahisha.

Wakipita katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Mwanza, waandamanaji walikuwa na mabango wakiimba nyimbo mbalimbali za hamasa kuilaumu Serikali kutokana na kile walichosema kuwa ni kufumbia macho ufisadi.

Aidha, akizungumzia suala la Dowans, Dk Slaa alisema kamwe kodi ya wananchi haitotumika kuilipa kampuni hiyo na kwamba kama wanataka kampuni hiyo kulipwa basi zitumike fedha za Rais Kikwete,Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Alisema ujio wa mmiliki wa Dowans, Suleyiman Al Adawi ni mbinu za kutaka kuwahadaa Watanzania.

“Dowans haiwezi kulipwa kwa kodi za wananchi kutokana na kampuni hiyo kuwa mtoto haramu, mama na baba yake ni Richmond na hayo yote yanayofanyika Rais Kikwete anayajua sababu yanafanyikia katika Serikali ya Tanzania, ”alisema Dk Slaa.

Alisema Rais Kikwete ana maswali mengi ya kujibu kutokana na Dowans kwa sababu Serikali ilitoa fedha nyingi za wananchi za kuleta mitambo hiyo ya umeme na kununua vifaa ili Dowans izalishe umeme, lakini leo  nchi ipo gizani.

Kupanda kwa gharama za maisha
Katika hatua nyingine, Dk Slaa alisema kupanda kwa gharama za maisha kunatokana na kupanda kwa umeme pia kukatika kwa umeme ambapo uzalishaji haufanyiki kama inavyotakiwa.

Alisema tabia ya wabunge wa CCM kuwazomea na kuwatisha wabunge wa Chadema wasiongee bungeni ni kazi bure na kusema kuwa kama hawatojirekebisha kwa hilo watawahamasisha wananchi kuwazomeoa wabunge hao majimboni kwao kama ilivyokuwa kipindi kile cha EPA.

Dk Slaa pia alimtahadharisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro kutokuingilia mamlaka ya Halmashauri ya Jiji na badala yake amuachie Meya wa Jiji hilo ambaye ni kutoka Chadema afanye kazi kwani yeye ndiye aliye na mamlaka hayo.

Alisema kwa mujibu wa sheria namba 19 ya mwaka 1999 inamtaka Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya kuwa wawezeshaji na sio watu wa kuingilia mamlaka ya Halmashauri ya Jiji.

Mbowe aonya Serikali kuhusu ufisadi
Kwa upande wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kama Serikali haitaweze kuinua maisha ya Watanzania kwa kuwaondolea ugumu wa maisha, wananchi wanaweza kutumia nguvu kukabiliana na mafisadi.

Wakatia akihutubia adhara hiyo ya watu waliokusanyika katika mkutano huo, Mbowe aliwaomba wananchi hao kuelezea Serikali kuwa wapo tayari kudai haki zao na kusema kuwa viongozi wa Chadema wakiongea CCM wanasema kuwa wanawaongopea wananchi kuwa hawajawatuma.

“Tumenyanyaswa, tumetishwa sasa tunasema kuwa tumechoshwa na tunasonga mbele kudai haki pamoja na uhuru na kama hawatoweza kutupatia nguvu zetu zitakuwa zaidi ya Libya," alisema Mbowe.

“Mnataka na Kikwete ajiuzulu pia,” wananchi walimjibu kwa sauti “Ndiyo” Mbowe aliendela na kusema, “Sawa nimewaelewa kumbe mnataka Rais Kikwete naye ajiuzulu pamoja na Ngeleja na Waziri Mwinyi (Hussein) pia ajiuzulu..ahaa ngojeni kwanza Kikwete tunataka kwanza tumalize kupita mahali pote na kuzunguka yeye inakuja yake babu kubwa kama ya Misri na Tunisia,” alieleza Mbowe.

Alisema Serikali ipo katika mpango wa kukodisha umeme kwa muda wa miezi minne na katika kipindi hicho wanazalisha umeme kwa kutumia kodi za Watanzania Sh 400 bilioni kulipa kampuni inayokodisha mitambo hiyo ya umeme.

Alisema Serikali kukubali kulipa Sh 300 bilioni za kunulia mafuta ni wizi mkubwa na kwamba uvumilivu wa Watanzania umefikia ukomo hivi sasa.

"Tumevumilia vya kutosha, safari hii ni ama zao ama zetu. Hatuwezi kukubali nchi imekaa miaka minne hakuna ufumbuzi wa umeme, taifa linalipa fedha za ajabu, hakuna anayejiuzulu na safari hii hatukubali,"alisema Mbowe na kuongeza:

"Mkuu wa Mkoa anatumia jenereta, Waziri Ngeleja, Waziri Mkuu wote hawa hawajui shida ya umeme, shida iko kwetu wananchi hivyo wananchi lazima tuchukue hatua".

Baada ya hapo aliwauliza wananchi iwapo wanataka Waziri Ngeleja ajiuzulu, wananchi walijibu ajiuzulu na kumtaja Rais Kikwete pia kujiuzulu.

Katiba ya nchi

Mbowe alisema aliwaongoza wabunge kutoka nje kumfikishia Rais Kikwete kutaka mabadiliko na kwamba hatua ile ilibezwa na viongozi wa CCM ambao leo hii wanaushangaza umma kwa kujadili mabadiliko ya Katiba.

Alisema baada ya hatua hiyo, mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliwasilisha bungeni hoja kuhusu suala hilo, lakini haikuweza kujadiliwa na hivyo kuwataka wananchi kuvumilia kwa vile sasa mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya utaanzia bungeni Aprili mwaka huu.

Joseph Mbilinyi na Halma Mdee
Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema kuwa Tanzania haina amani kama Serikali ya CCM inavyowatangazia wananchi.Alisema anashangaa hata wabunge wakiingia bungeni wanakaguliwa, sasa je wananchi wa mitaani.


Jonh Mnyika na Godbless Lema
Pamoja na kuambiwa kumuobaa radhi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisisitiza kauli yake kuwa alidanganya na kusema kuwa kamwe hawezi kuomba radhi.

Alisema Jeshi la Polisi mkoani Arusha liliomba siku 60 kufanya upelelezi wa mauaji yaliyotokea jimboni kwake,  inakuwaje leo anasimama na kuwadanganya wananchi kuwa Chadema ndiyo waliofanya mauaji hayo wakati hata upelelezi haujakamilika.

Kwa upande wake, Mnyika alisema kupanda kwa gharama za maisha ni matokeo ya mafisadi.

Alisema kuwa anashangazwa na agizo la Serikali kushusha bei ya sukari nchini ambayo imepanda mpaka kufikia Sh 2000 kwa kilo moja kutoka katika bei ya kawaida iliyokuwapo ya Sh 1600.

“Watanzania agizo hilo la Serikali limetokana na maandamano ya leo waliposikia tuna andamana kupinga mfumuko wa bei pamoja na Dowans kutokulipwa kwa kodi za wananchi na wao wakajifanya kutoa agizo hilo, ”alisema Mnyika.

Wabunge wa Mwanza
Kwa upande wa wabunge hao wa Chadema mkoani Mwanza waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa watahakikisha wanainua maisha ya wana-Mwanza kwa kusimamia rasirimali zilizopo mkoani hapa na kuifanya wilaya ya Bunda ambayo ndiyo ya kwanza kwa umasikini kuondoka kwenye nafasi hiyo .

Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje alisema kuwa ni aibu kwa wana-Mwanza kuchachuka na maisha wakati mkoa huu uonaongoza kwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo kama zitasimamiwa ipasavyo zitawakomboa wananchi wake.

Maandamano ya Mwanza yamefanyika takribani miezi miwili tangu kutokee mauaji ya raia waliopigwa risasi na polisi mkoani Arusha, wakati walipokuwa wakizuia maandamano ya Chadema mkoani humo.

Katika tukio hilo la Januari 6, mwaka huu polisi wa Arusha walimwaga damu za watu kadhaa na wengine zaidi ya 30 walijeruhiwa miongoni mwao wakiwamo walioshiriki na wasioshiriki maandamano yaliyoandaliwa na Chadema.

Risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika katika jitihada za polisi kuzima maandamano hayo, wakitekeleza amri ya Mkuu wa Jeshi hilo, Ispekta Jenerali Said Mwema ambaye awali aliyapiga marufuku baada ya awali  kuwa yameruhisiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye.
Tags:

0 comments

Post a Comment