Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Shivji: Nchi inaporwa na walanguzi wanaojiita wawekezaji wa kigeni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
PROFESA wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Issa Shivji amesema kuna wimbi kubwa la waporaji wanaohamishia uchumi wa nchi, katika nchi nyingine za nje kwa kigezo kwamba ni wawekezaji.

Akizungumza katika kongamano la Ardhi na Ulinzi wa rasilimali katika Katiba, lililoandaliwa na Asasi ya Haki Ardhi, Profesa Shivji alisema kwa miaka 50, baada ya uhuru wananchi wengi, hawana haki ya kupata ardhi badala yake wawekezaji ndiyo wameipata na wamekuwa wakiitumia kupora utajiri wa nchi.

Profesa Shivji alitoa kauli hiyo, wakati kukiwa na vuguvugu la mabadiliko ya Katiba na nchi ikikabiliwa na matatizo makubwa ya umeme na kupanda kwa bei ya vyakula mbali mbali.

“Kumekuwa na uporaji wa ardhi ya kijiji na wawekezaji-wafisadi wa ndani na nje kwa visingizio mbalimbali pamoja na bio-fuels na ulimaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya masoko ya kimataifa. Utakuta matajiri wanatoka Dubai wanakuja kupora ardhi na kuhamishia utajiri wote kwao,” alisema Profesa Shivji.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Shivji alisema maisha yamekuwa magumu, bei za vyakula, zimepanda kwa sababu wananchi hawana nafasi tena ya kuzalisha.

Akitoa mfano, Shivji alisema katika Jiji la Dar es Salaam licha ya kuwa na majengo mengi marefu, asilimia 70 ya wakazi wake wanaishi katika makazi yasiyo rasmi na kufafanua kwamba walanguzi wamepora maeneo ya wananchi na kujenga, maghorofa na wananchi kukosa maeneo ya kuishi.


Alishauri wananchi washirikishwe katika kujadili mfumo mpya wa Katiba utakaotoa fursa kwa wananchi, ili wawe na nguvu ya kumiliki ardhi na rasilimali zao.

Alisema Katiba ya sasa, haisemi lolote kuhusu ardhi badala yake imegusia haki ya wananchi kumiliki ardhi, na kusababisha  utata kuhusu umilikaji wa ardhi.

Naye Odenda Lumumba wa Chama cha Watetezi wa ardhi wa Kenya alitoa uzoefu wa suala la ardhi na jinsi lilivyoingizwa kwenye mabadiliko ya Katiba mpya nchini humo, akisema kuwa walianza mijadala kwa muda mrefu na baadaye, walifanikiwa.

“Tuliandaa mapendekezo yetu na tukayapeleka kwenye mchakato wa Katiba, tunashukuru asilimia 90 ya mapendekezo yetu yamepitishwa,” alisema Lumumba.
Tags:

0 comments

Post a Comment