Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mahakama: Lema ana kesi ya kujibu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KESI ya kupinga ubunge wa Godbless Lema wa Arusha Mjini, inaendelea kuunguruma leo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutupilia mbali pingamizi za awali zilizowekwa na mawakili wa utetezi, Method Kimomogoro na Timon Vitalis.


Jaji Aloyce Mujuluzi alitoa uamuzi wa pingamizi zilizotaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa madai kuwa, walalamikaji hawakuwa na haki kisheria kulalamikia mambo ambayo yalitamkwa dhidi ya aliyekuwa mgombea
wa CCM, Dk Batilda-Salha Buriani, kuwa akichaguliwa atahamia Zanzibar alikoolewa.


Walalamikaji hao, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo, kupitia kwa Wakili wao, Alute Mughwai na Modest Akida, walidai kuwa kwa nyakati na sehemu tofauti, Lema alitoa kauli zenye dalili ya ubaguzi dhidi ya Dk Buriani, hivyo kuomba mahakama itengue ushindi wake kutokana na ukiukaji kanuni na taratibu za uchaguzi.


Hata hivyo, mawakili wa utetezi, Kimomogoro anayemwakilisha mshtakiwa wa kwanza na Vitalis anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), waliomba mahakama kutupa madai hayo, wakieleza kuwa kisheria aliyestahili kulalamikia maneno hayo ni Dk Buriani siyo wapiga kura.


Jaji Mujulizi alisema baada ya kupitia madai na majibu ya upande wa utetezi, mahakama imeona walalamikaji wana haki kisheria kulalamikia taratibu, mwenendo wa kampeni na mchakato mzima wa uchaguzi, kwa sababu walikuwa wapiga kura waliojiandikisha na wenye haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu uliopita.


Alisema mawakili wa utetezi waliingia kwenye mtego kwa kuacha kuleta pingamizi kuhusu makosa ya kisheria dhidi ya hati ya mashtaka, badala yake walijikita kutafsiri na kurekebisha madai yaliyomo kwenye hati ya mashtaka, kazi aliyosema haiwezi kufanywa na mahakama wala upande wa utetezi.


“Mahakama haiwezi kuweka vipimo vya jumla kwa wapiga kura, mambo wanayoweza kulalamikia na kupinga katika uchaguzi kwa sababu kila uchaguzi huja na mambo na mazingira tofauti. Siyo sahihi mahakama kuzuia mtu yeyote anayedhani ana ushahidi kuthibitisha madai yake kuleta maombi mahakamani," alisema Jaji Mujuluzi.


Alisema katika shauri hilo, mahakama haitachunguza wala kushughulika na ukweli wa maneno yaliyotamkwa, bali kitakachotafutwa ni iwapo maneno hayo yalitamkwa na iwapo yalistahili kutamkwa.


"Kwa maoni na uamuzi wangu, pingamizi hizi zilizowasilishwa mbele yangu hazikidhi mahitaji ya kisheria, hivyo nazitupilia mbali nawajibu ili kutoa nafasi kwa wadai kuleta ushahidi wao kuthibitisha yale waliyowasilisha mahakamani, ambayo pia yatahojiwa na upande wa utetezi," alisema Jaji Mujuluzi.


Kesi hiyo inayovuta umati mkubwa wa wasikiliza kila inapotajwa, itaendelea leo kwa upande wa wadai kutoa hoja za awali kujenga madai yao kabla haijaanza kusikilizwa.

0 comments

Post a Comment