Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wanasheria wamtega JK muswada sheria ya katiba

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimetishia kwenda mahakamani kupinga Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iwapo Rais Jakaya Kikwete atapuuza malalamiko na hoja za wananchi kupitia makundi mbalimbali wanayoupinga licha ya kupitishwa na Bunge wiki iliyopita.


Rais wa TLS, Francis Stolla aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa upitishwaji wa muswada huo haukuzingatia taratibu na kanuni za Bunge na kumwomba Rais, akiwa sehemu ya Bunge kurekebisha makosa hayo kwa kukataa kuutia saini.


Chama hicho kimemtaka Rais Kikwete kuurejesha upya muswada huo bungeni ili usomwe kwa mara ya kwanza na wananchi wapewe fursa ya kuujadili kwa kina kwa lengo la kuupa uhalali kisheria, kijamii na kisiasa.


Stolla alikuwa akitoa mada wakati wa kujadili Miaka 50 ya Uhuru na changamoto ya mabadiliko ya Katiba kwa jamii za wafugaji, warina asali, waokota matunda na wakulima.
Akizungumza kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Jukwaa la Umoja wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayotetea Haki za Wafugaji (PINGO's Forum), Stolla alisema Rais Kikwete anapaswa kusikiliza kilio cha wananchi ili kuliepusha taifa na vurugu.


Alisema vurugu hizo zitatokana na sheria inayopendekezwa na muswada huo aliodai ulipitishwa kwa kuzingatia utashi wa kisiasa wa vyama badala ya mahitaji ya taifa na jamii.


Alisema sheria hiyo ikipitishwa, itakuwa imejadiliwa na wananchi wa mikoa mitatu pekee, miwili kutoka Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam na Dodoma na Mkoa mmoja wa Zanzibar.


Alionya kuwa Tanzania ina mikoa zaidi ya 25 hivyo “Uwakilishi mdogo namna hii haukubaliki kwenye jambo kubwa na muhimu kama hilo la Katiba ya nchi inayobeba maisha na maslahi ya watu wote.”


Alisema licha ya muswada huo kutofikishwa kwa wananchi kwa lugha na wakati muafaka, pia umebeba maudhui yenye lengo la kuminya haki ya msingi wa watu kutoa maoni. Alisema haki hiyo imeminywa kutokana na Bunge kupitisha kifungu kinachonyima watu wasio wajumbe wa tume ya katiba kuandaa mikutano au majumuiko ya kujadili, kutoa, kukusanya na kuandaa maoni na mapendekezo yao kuhusu Katiba Mpya.
Isitoshe akasema kifungu hicho kinaweka wazi kwamba anayepatikana na kosa hilo atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyozidi milioni 15 au vyote kwa pamoja.


Alisema ili kuitendea haki jamii na umma wa Watanzania, TLS imeunda kamati maalumu ya wanasheria zaidi ya watano inayoongozwa na Profesa Angelo Mapunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kufanya utafiti juu ya vipengele vya sheria vilivyokiukwa na kuhakikisha wanashinda shauri watakalofungua mahakamani iwapo Rais atapitisha sheria hiyo.


Stolla alitaja upungufu mwingine kwenye muswada huo kuwa ni uwepo wa miswada miwili, wa Kiingereza uliowasilishwa bungeni Aprili, mwaka huu na kusomwa kwa mara ya kwanza kabla ya wabunge kuagiza ukaandikwe kwa Kiswahili ili kutoa mwanya kwa Watanzania wengi kuweza kuusoma na kuulewa.


Alisema muswada ulioandikwa kwa Kiswahili uliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza mwezi huu lakini kwa makusudi na kwa kutumia uwingi wa wabunge wa CCM na CUF. Alisema kitendo cha kupitishwa kwa muswada huo ni cha aibu kwa Bunge na kinapaswa kurekebishwa na Rais kwa kukataa kutia saini.


Stolla alitaja kasoro nyingine katika muswada huo kuwa ni muundo wa Bunge la Katiba unaopendekeza wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba hali itakayosababisha mjadala na upitishwaji wa Katiba Mpya kumilikiwa au kutawaliwa na wanasiasa.


Alisema hali hiyo ni hatari kwa sababu wanasiasa hao watapitisha kwa kuhakikisha wanalinda maslahi ya vyama na itikadi zao kisiasa.


WBaada ya makosa haya yote, kimbilio pekee la wananchi kurekebisha makosa haya yaliyofanywa kwa makusudi na Bunge letu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Kikwete,” alisema na kutoa wito:


“Tunamuomba asikilize kilio cha watu wake, atafakari hoja zao na kukataa kusaini sheria hii kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho. Atumie nafasi yake ya sehemu ya pili ya Bunge kurekebisha udhaifu huu.”


“Sifa muhimu kwenye haki siku zote ni kuwa na uwezo wa kuidai na hili litafanyika kikamilifu bila kujali vitisho vya kisheria au nguvu ya vyombo vya dola kwani Katiba tuliyonayo sasa imetoa haki kwa kila mtu kukutana na wenzake na kutoa maoni,” alisema na kuongeza:


“Watapaza sauti kwa njia wanayoona inafaa na pengine ikaleta machafuko nchini. Rais anapaswa kuzingatia hili.”


Alisema muswada huo umeacha mianya mingi inayoweza kutumiwa na watawala kufikia malengo na maslahi yao kama vile kutoweka wazi uwakilishi wa makundi mbalimbali, idadi ya wajumbe pamoja na uundwaji wa tume kukabidhiwa mikononi mwa Rais pekee.


Alisema muswada huo pia unampa Rais mamlaka kuipa tume hadidu rejea na ripoti kuwasilishwa kwake bila kuwepo fursa ya umma kuhoji hata uteuzi na uadilifu wa wajumbe.


Wakichangia mjadala huo, wengi wa washiriki walielezea upungufu wa sheria katika ugawaji na umilikaji wa ardhi maeneo ya vijijini na kutaka Katiba Mpya ianishe ushiriki wao.


Walisema wananchi wamekuwa wakiondolewa kwenye maeneo yao kuwapisha wawekezaji ambao baadhi yao hawafiki hata kwenye uongozi wa Serikali za Mitaa kujitambulisha kwa madai kuwa wamepewa ardhi hizo na mamlaka za juu.


Mkazi wa Kijiji cha Endulen, Ngorongoro, Noolosho Nakuta alieleza kushangazwa na kitendo cha Serikali kutotambua uwepo wao ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwanyima hata maeneo ya kujenga miradi ya kijamii kama zahanati na shule.
Alisema wakati wananchi wanabanwa katika hilo, wawekezaji wanapewa vibali vya kujenga majengo makubwa kama hoteli.

0 comments

Post a Comment