Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Serikali yapigia magoti Azaki kuhusu Katiba

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SIKU tano baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Mabadiliko ya Katiba, Serikali imezipigia magoti Asasi za Kiraia (Azaki) kuziomba kutoa maoni kuhusu katiba mpya kwa uhuru na kutumia njia za kistaarabu. Muswada huo ulipitishwa na wabunge wengi wa CCM na CUF Ijumaa wiki iliyopita, huku wale wa Chadema na NCCR-Mageuzi wakigoma baada ya Spika wa Bunge, Anna Makinda, kuwakatalia muswada huo kurejeshwa kwa wananchi.


Akizungumza katika ufunguzi wa tamasha la Azaki Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu, alisema ustaarabu ndiyo utaleta katiba mpya yenye tija na maendeleo kwa Watanzania wote. “Tujadiliane kwa ustaarabu huku tukijenga utamaduni wa kuvumilia maoni yatakayotofautiana na yetu sambamba na kuwa na mtazamo chanya na kuiweka mbele taswira nzuri ya taifa letu kimataifa,” alisema Dk Nagu.


Dk Nagu alizionya Azaki kuepuka kutumiwa na makundi yasiyolitakia mema taifa, ambayo yanaeneza hisia za chuki na uchochezi kwa Watanzania. “Hii ni Tanzania yetu sote jamani… wote tuna wajibu wa kulinda uhuru, amani, utulivu na umoja wetu, Azaki zina uzoefu kwenye utetezi wa haki za makundi maalumu, tumieni uzoefu huo kuliletea maendeleo taifa letu,” alisema Dk Nagu.


Alisisitiza kuwa asasi za kiraia zina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya fikra miongoni mwa Watanzania, kwa lengo la kujenga taifa lenye watu wanaowajibika na wanaoshiriki kikamilifu kujiletea maendeleo.


Pia, Dk Nagu alisema asasi za kiraia zinatakiwa zijiwekee malengo kulingana na yale yalioanishwa katika dira ya Serikali ya maendeleo ya mwaka 2025, kwa sababu ndiyo itakayofikisha taifa kwenye ustawi wa maendeleo ya uchumi. “Malengo ya Serikali na Azaki yanafanana, nayo ni kuwahudumia wananchi katika jitihada zao za kujiletea maendeleo,” alisema Dk Nagu.


Tamasha hilo lenye kaulimbiu ya ‘Miaka 50 ya Uhuru, nafasi ya Azaki katika Ujenzi wa Taifa’, linashirikisha zaidi ya washiriki 300 na linatarajiwa kumalizika kesho. Moja ya mada zitakazojadiliwa ni mchakato wa mabadiliko ya katiba ambayo itajadiliwa leo kwa kuhusisha wataalamu mbalimbali.

0 comments

Post a Comment