IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, atakuwa miongoni wa wahitimu 2,444 wanaotajia kupata shahada mbalimbali katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Novemba 26 mwaka huu.
Akiwa mhitimu wa 2,444 kwenye orodha ya wahitimu hao wa ngazi mbalimbali, Mwinyi anatajwa kuwa atatunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Fasihi, (D.LETT).
Tangazo la mahafali hayo lililotolewa na Mkuu Msaidizi wa chuo hicho (Taaluma), Profesa Elifas Bisanda, limeeleza kuwa wahitimu hao watatunukiwa shahada hizo kwenye mahafali ya 23 ya chuo hicho yatakayofanyika Bungo, Kibaha mkoani Pwani.
"Mkutano wa mwaka utafanyika wiki hii, Novemba 24 kuanzia saa 3:00 asubuhi na mahafali ya 23 yatafanyika tarehe 26 Novemba, siku ya Jumamosi," ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Profesa Bisanda.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wahitimu wa mahafali hayo, watakuwa wa ngazi mbalimbali ambazo ni Astashahada, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu. Mwinyi atakuwa Mwanafunzi pekee, atakayepata Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Fasihi.
Wengine watakaopata shahada za uzamivu (PHD) katika mahafali hayo na mikoa wanayotoka kwenye mabano ni Cosmas Kapis (DSM), Felix Mlengeki (DSM), Chema Natalia (Dodoma) na Cuthbert Ngalepeka.
Mbali na shahada hizo, Chuo hicho mwaka huu, kitatoa wahitimu sita wa kwanza katika Shahada ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.
Wahitimui hao ni Ikunda Mushi, Andulile Mwailunga na Emmanuel Onyango (Uandishi wa habari) na Enelen Gidion, Mwanzo Millinga na Nicodemus Nyanguh (Mawasiliano ya Umma).
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - 'Mzee Ruksa' kutunukiwa Shahada ya Udaktari OUT
0 comments