IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KINYANG'ANYIRO cha kurithi kiti cha Rostam Aziz katika Jimbo la Igunga, sasa kimefikia hatua ya wagombea wanatarajiwa leo kuanza kuchukua fomu kwa msimamizi wa uchaguzi huo.
Tayari vyama vya siasa vimemaliza mchakato wa kutoa fomu kwa wagombea wao baadhi ikiwemo CUF vikiwa vimekwishakamilisha kupata mgombea huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwa bad katika mchakato wa kupata mtu atakayepeperusha bendera yake.
Akizungumza na Mwananchi mjini Igunga jana, msimamizi wa uchaguzi huo, Protace Magayane alisema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri na kwamba fomu kwa ajili ya wagombea zipo tayari.
Magayane alisema kuanzia leo Agosti 24 hadi Septemba sita, zitakuwa ni siku za kuchukua fomu kwa wagombea wa vyama na kuongeza kwamba, Septemba saba hadi Oktoba Mosi itakuwa ni kampeni na uchaguzi utakuwa Oktoba mbili.
Alisema Oktoba tatu hadi nne ni kujumlisha kura na hatimaye mshindi kutangazwa na kuvitaka vyama vya siasa pindi vitakapoanza kampeni kuwa na uvumilivu kwa kuheshimiana ili kufanya uchaguzi wenye amani.
"Wakazi wa Igunga ni watu wanaoishi kwa amani na kamwe hawapendi vurugu nawaomba wanasiasa wasitumie vibaya majukwaa kwa kuhamasisha fujo..., tushirikiane tumalize uchaguzi salama," aliasa Magayane.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti mjini Igunga, baadhi ya wagombea wametamba kushinda uchaguzi huo kwa madai wanakubalika zaidi ya wengine.
Waliopitishwa na vyama hadi hivi sasa
Wagombea waliopishwa mpaka hivi sasa na vyama vyao ni Joseph Kashindye (Chadema), Moses Edward (TLP), Leopard Mahona (CUF) na John Maguma wa SAU, wakati kwa upande wa CCM aliongoza katika kura za maoni katika ngazi ya kamati ya siasa ya wilaya ni Dk Peter Kafumu, ambaye hata hivyo, kamati kuu ya chama chake hakijafanya uteuzi.
"Sisi hatuchukuii fomu kesho (leo) tunajipanga kwanza, lakini tumekuja kuwakomboa watu wa Igunga, kama hakuna mizengwe tutashinda kwa kishindo," alisema Kashindye wa Chadema.
Kwa upande wa mgombea wa CUF, Mahona yeye mara kadhaa amekuwa akisikika akitamba atachukua jimbo hilo kwani tayari ana mtaji wa kura 11,000, alizozipata wakati wa uchaguzi uliopita hivyo ana hakika na ushindi.
Wagombea wa SAU na TLP na wao wamekuwa wakijigamba kuonyesha maajabu kwa kuangusha vigogo wanaopambana nao kwenye uchaguzi huo.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Wagombea ubunge Igunga waanza kuchukua fomu leo
0 comments