Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wabunge wa CCM wakataa kuburuzwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KATIKA kile kinachoonekana ni kukataa kufungwa midomo, wabunge wa CCM jana walikataa mpango wa kujadili yaliyomo katika Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wakitaka isomwe kwanza bungeni ili wapate fursa ya kuchangia kama ilivyo kwa wabunge wengine.
Jana, baada ya Bunge kuahirishwa saa 7:00 mchana, Kamati ya Wabunge wa CCM, ilikutana chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa malengo makuu mawili, la kwanza lilikuwa ni kujipanga ili “kuiokoa” bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 20111/12 ambayo ilikuwa ikakabiliwa na kitisho cha kukataliwa na wabunge wakiwamo wa chama hicho lakini pili, kuweka mikakati ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inayotarajiwa kuwasilishwa leo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho, baada ya kujadili na kukubaliana kuhusu kupitishwa kwa Bajeti ya Ardhi, wabunge hao walikataa kujadili suala la Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inayotarajiwa kuwasilishwa na Waziri wake, Ezekiel Maige kwa maelezo kwamba wakutane tena leo mchana, baada ya kumsikiliza kile atakachowasilisha bungeni.

“Wabunge wamekataa wamesema wanataka kwanza wamsikilize Maige atakuja na nini kesho (leo), halafu hapo ndipo watakapokuwa na kitu cha kusema... kwa hiyo tutakutana tena kesho (leo) mchana,” alisema mmoja wa wabunge hao wa CCM ambaye alihudhuria kikao hicho na kuongeza:

“Kwa ufupi leo hatukuwa na kitu burning (kikubwa) ambacho tumeamua, ila ni kama tumekataa kufugwa midomo, ujue ukisha jadili leo (jana) huwezi kusema tena kesho (leo).”

Vyanzo hivyo vilisema hoja ya kutaka kutojadiliwa kwa suala la uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ilitolewa na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo na kuungwa mkono na wabunge karibu wote bila kufuata utaratibu.

“Baada ya Shellukindo kupendekeza kwamba tujadili suala hilo baada ya waziri kusoma hotuba yake Bungeni, mwenyekiti aliuliza kama kuna mwenye wazo jingine lakini zilisikika sauti za wabunge wakisema kesho, kesho, kesho, kesho,” kilieleza chanzo chetu.

Kufuatia hali hiyo, Pinda alikubaliana na mawazo ya kutojadiliwa kwa suala hilo na hivyo kuahirisha kikao hicho cha Kamati ya Wabunge wa CCM hadi leo saa saba mchana baada ya kuahirishwa kwa Bunge.

Kwa kawaida baadhi ya mawaziri wanaoongoza wizara nyeti hupata fursa ya kuwasilisha muhtasari wa bajeti zao katika kikao cha chama kwa lengo la kutaka kuungwa mkono na wabunge wenye hoja zao huzitoa katika kikao hicho ili Serikali iweze kurekebisha.

Hali hiyo inatafsiriwa na wabunge wa CCM kama mbinu ya kuwafunga midomo wasiseme na kusikika kwa wananchi wao, hali ambayo wanadai huwafanya waonekane watetezi wa Serikali na badala ya kuwawakilisha wananchi.

“Kwa sasa watu tumeshtuka, tumechoka kuwalinda watu na mahali tulipofika ni kwamba Serikali ifanye kazi yake na ituache wabunge tufanye kazi yetu, hatuwezi kuendelea kubebana kwa mambo ambayo yanaweza kurekebishwa,” alisema mbunge mwingine kutoka katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Maliasili na Utalii

Hatua ya wabunge wa CCM kukataa kujadili suala hilo la maliasili na utalii linamweka Maige na wizara yake katika wakazi mgumu wa kupitishwa kwa Bajeti ya wizara yake.

Katika Mkutano huu wa Nne wa Bunge la Bajeti, wizara tatu zimeonja joto ya jiwe baada ya bajeti zao kupita kwa msaada wa Waziri Mkuu, Pinda.

Wizara ya Nishati na Madini ndiyo iliyopata wakati mgumu zaidi kwani bajeti yake iliondolewa bungeni na kurejeshwa wiki tatu baadaye baada ya Serikali kufanya marekebisho na kuja na mpango wa kuliondoa taifa katika tatizo sugu la umeme.

Wizara nyingine zilizokuwa katika hali mbaya kutokana na wabunge wengi wakiwamo wa CCM na wa upinzani kukataa kuunga mkono hotuba hizo ni ile ya Uchukuzi na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kiasi cha kumfanya Pinda kutoa maelezo kwa wabunge huku akiwasihi walegeze misimamo dhidi ya bajeti hizo.

Vikao vya kamati ya wabunge wa CCM vimekuwa vikitumika kusaidia kupitishwa kwa bajeti hizo, lakini safari hii vilishindwa kuiokoa ile ya Nishati na Madini hali inayozua hofu kwamba huenda hali hiyo ikaikumba Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hivi sasa wizara hiyo inakabiliwa na tuhuma kadhaa za ufisadi hasa katika Idara ya Wanyamapori ambayo inahusishwa na wizi na utoroshaji wa wanyama kwenda nje ya nchi, kinyume cha sheria.

Waziri Maige anayeongoza wizara ambayo haina Naibu Waziri, anakabiliwa na mtihani mgumu wa kutoa maelezo kuhusu suala la vitalu vya uwindaji ambalo linadaiwa kugubikwa na utata, pia vigogo kumiliki vibali vya kuvuna misitu ambavyo huvikodisha kwa bei kubwa.

0 comments

Post a Comment