Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - CTI Haikukubaliana na ongezeko la bei ya Umeme. Wamcharukia Mh. Ngeleja

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KAULI ya Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kwamba Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), limeridhia kwa hiari ongezeko la bei ya umeme imelichefua shirikisho hilo ambalo limesema kuwa kauli hiyo haikuwa sahihi.
Ngeleja akiwasilisha mpango wa dharura wa kukabiliana na tatizo la umeme unaotarajiwa kutumia Sh 1.2trilioni, kati ya mwezi huu hadi Desemba mwakani, pamoja na mambo mengine aliisifia CTI kwa kuonyesha uzalendo wa kukubali ongezeo hilo.

Hata hivyo, vyanzo huru vya habari kutoka kwa wajumbe wa kikao kati ya CTI na Tanesco kilichoketi Agosti 5, vilifafanua kwamba hakukuwa na makubaliano ya aina yoyote kuhusu nyongeza hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kilichokubaliwa na CTI ni kuchukua dhamira hiyo ya serikali na Tanesco kisha suala hilo lifikishwe kwenye kikao cha pamoja cha maamuzi ndani ya shirikisho hilo.

"Tulishangaa tumesifiwa bungeni, sisi hatukubali ongezeko la bei ya umeme. Pale tulichosema ni kwamba hatukuwa na mamlaka ya kuweza kufanya maamuzi ya jambo hilo ambalo wala hatukuwa tumelijua awali," kilifafanua chanzo kimoja.

Chanzo kingine kilisema, CTI ambayo iliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji Christine Kilindu , Mwenyekiti Felix Mosha na wajumbe wengine tisa, haikuwa ikijua nini kitakwenda kuzungumzwa kwenye mkutano huo.

Mkutano huo kwa upande wa Tanesco uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji William Mhando.

Alipotafutwa mwenyekiti Mosha kwa njia ya simu hakuweza kupatikana lakini alipoulizwa mkurugenzi Kilindu, naye alihoji, "nani kakwambia hivyo?"

Kilindu hakutaka kuthibitisha wala kukataa badala yake alikata simu na hata alipopigiwa baadaye simu iliita bila kupokelewa.Lakini, Ngeleja wakati akiwasilisha bajeti hiyo iliyokuwa imekwama awali, alisema CTI imeonyesha uzalendo kwani wamesema wako tayari kuongezewa bei ya umeme kama utapatikana kwa uhakika, na kutangaza mkakati huo wa kuongeza bei ili kuipa nguvu Tanesco iweze kujiendesha.

Ngeleja katika mpango huo alisema hadi Desemba mwaka huu serikali itatoa Sh 408 bilioni kusaidia upatikanaji wa umeme huo wa dharura na kwamba hadi Desemba mwakani, jumla ya megawati zaidi ya 800 zitakuwa zimezalishwa huku jumla ya fedha zinazohitajika zikiwa ni hizo sh 1.2trilioni.

0 comments

Post a Comment