IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KANISA Katoliki nchini na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) ni miongoni mwa taasisi za dini ambazo zimetajwa kutumiwa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kufanya biashara ya dawa za kulevya.Mmoja wa watoa mada kutoka Kikosi Kazi za Kupambana na Dawa za kulevya aliwaambia wabunge jana mjini Dodoma kwamba, eneo lingine ambalo limekuwa likitumika katika biashara hiyo ni vyama vya michezo vinavyosafirisha wanamichezo wake kwenda nje ya nchi kushiriki michezo ya kimataifa.
Mtoa mada huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema Tanzania iliwahi kupeleka vijana katika moja ya mikutano iliyoitishwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Benedict XVI nchini Australia, na kwamba miongoni mwa vijana hao walibainika kujihusisha na dawa za kulevya na kwamba wengine hawakuwahi kurejea nchini.
Japokuwa mtoa mada huyo hakuweka wazi kwamba vijana hao walisafiri chini ya mwavuli wa Kanisa Katoliki nchini, tukio lilitokea Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika mwaka 2008 katika mji mkuu wa Australia, na kuhudhuriwa na Papa Benedict XVI.
Siku ya vijana duniani ni tukio la kimataifa ambalo huratibiwa na Kanisa Katoliki likiwajumuisha maelfu ya vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani Katika mkusanyiko huo vijana hujadili masuala mbalimbali yanayohusu rika lao na mustakabali wao.
Kwa upande wa Bakwata, alisema baadhi ya watu hujichomeka katika msafara wa watu wanaokwenda kuhiji Makka, lakini wakiwa na nia ya kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya na kwamba, wakipata fursa hutimiza malengo yao.Kuhusu michezo, mtoa mada huyo alisema njia hiyo hutumiwa sana na watu ambao hujitokeza kufadhili safari za wanamichezo husika ili kutimiza matakwa yao ya biashara hiyo haramu.
"Wakati mmoja, mzee Nyambui (Suleiyman) timu yake ya ndondi ilikuwa ikitafuta wafadhili kwenda nje, wakajitokeza wafanyabiashara watatu kwa ajili ya kutoa ufadhili huo, lakini wakatoa masharti kwamba lazima nao wasafiri," alisema na kuongeza:
"Walitoa fedha hizo, lakini walipofika nchini Australia wale jamaa walikamatwa na dawa za kulevya ".
Katika semina hiyo Serikali pia ilitekeleza ahadi yake iliyoahidi juu ya mkanda wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambapo ilionyesha hadharani, huku wabunge wakitaka wahusika wanyongwe mara moja.Kwa muda mrefu kumekuwa na kelele za wabunge na wananchi wakitaka majina na mtandao huo uwekwe hadharani ili wananchi wajua juu kilichoko nyuma ya pazia.
Kikosi Kazi cha Kupambana na dawa za kulevya chini ya Kamishina, Godfrey Nzowa, kilitaja orodha hiyo kwa wabunge huku sehemu kubwa ya waliokamatwa wakionekana kuwa ni raia wa kigeni.Hata hivyo, baadhi ya raia wa Tanzania waliotajwa ni sehemu ya mtandao huo ambao watoa mada walisema kuwa ni mawakala.
“Si hao tu, lakini wapo Watanzania ambao ni mawakala katika vita hiyo ambayo kwa kweli tunakiri kuwa ni ngumu na inahitaji msukumo wa aina yake,’’ alisema mtoa mada.
Aliwataja baadhi ya waliokamatwa kuwa ni pamoja na Mchungaji Ikechuku Okidi wa Kanisa la lililopo Biafla jijini Dar es Salaam.Wengine ni pamoja na Mzee mmoja wa Kanisa, Mkazi wa Mbezi na mwanamtandao mkubwa wa dawa za kulevya ambaye ni mwanamke.
Hata hivyo, watoa mada hao walilalamikia kitendo cha mahakama kuwaachia kwa dhamana watuhumiwa wa dawa za kulevya ambao ni raia wa Pakstani wawili ambao walikamatwa kwa kilo 180 za Heroin.“Tumesikitika sana na kuvunjika moyo kwa kitendo kilichofanywa na mahakama kwa kuwaachia kwa dhamana watuhumiwa wale huku tukiamini kuwa haikuwa haki kufanya hivyo,’’ alisema msemaji huyo.
Katika picha mbalimbali zilizoonyeshwa katika mkanda wa video hiyo, ziliwafanya wabunge kupandwa na jazba na kuanza kupiga kelele wakitaka watuhumiwa wanyongwe pamoja na jaji na mahakimu waliohusika kuwaachiwa huru raia hao wakamatwe na kuwajibishwa.
Mbunge amwaga machozi
Mbunge wa Viti Maalumu Amina Mohamed Mwidau (CUF) jana alimwaga machozi mbele ya wabunge wenzake na kushindwa kuendelea na mchango wake baada ya kueleza kuwa watoto wa dada yake walikufa kwa pamoja baada ya kuathirika na dawa za kulevya.
“Mimi nataka wafanyabiashara hawa wanyongwe mara moja kwani wanaumiza watoto wetu. Watoto wa dada yangu walikufa wote kwa wiki moja kutokana na dawa hizo,’’ alisema na kuanza kulia huku akishangiliwa na wabunge wengine.
Baadhi ya wabunge waliopendekeza kunyongwa kwa wafanyabiashara hao ni pamoja na Moses Machali, Mohamed Sanya, Mohamed Mnyaa na Mohamed Rashid.Kwa upande wake, David Kafulila, yeye alitaka wafanyabishara hao wanyongwe ili watu walioajiliwa kwa kitendo cha kunyonga wasilipwe mishahara ya bure.
Mbunge kijana kuliko wabunge wote kwa majimbo, Ferix Mkosamali (Muhambwe-NCCR Mageuzi), aliwataka wabunge kuigomea bajeti ya Wizara ya Sheria kuwa isipitishwe hadi itakapotoa majibu ya hakimu aliyetoa dhamana kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Kombani azomewa
Kufuatia malalamiko kuhusu kuachiwa kwa raia hao huku Watanzania waliokamatwa nao wakiendelea kusota ndani, ilimuwia vigumu Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani ambaye hotuba yake ilibezwa na wabunge kwa makelele hakuna, hakuna, haiwezekani.
Kombani alisimama na kutaka kutoa ufafanuzi juu ya kuachiwa huru wageni hao ndipo wabunge walianza kupiga makelele wakimbeza na kumfanya akae chini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema aliingilia kati.
“Ndugu wabunge, huu ni wakati wa kusema kweli, biashara hii ina fedha nyingi, inahitaji wenye moyo wa simba kushinda vishawishi, kwa kweli lazima tuwe makini sana,’’ alisema Jaji Werema.
Alisema kuwa tatizo lililofanya wageni hao kuachiwa kwa dhamana ni kutokana na upungufu makubwa ya sheria iliyopo kuhusu dawa hizo.Hata hivyo, alisema ofisi yake inafanya uchunguzi juu ya hakimu aliyewaachiwa wafanyabiashara hao ambapo alisema mwisho wa siku sheria itachukua mkondo wake.
Hata hivyo, Werema alisema kuwa suala la kutenga adhabu ya kifo kwa wajumbe hao si la lelemama na akathibitisha uzoefu wake kuwa aliwahi kutoa adhabu ya kifo, lakini mwisho wa siku alijikuta akimwaga machozi kwa kuwa si rahisi kumhukumu mtu kifo.
Kikosi kazi cha dawa wanena
Wakitoa majumuisho ya maswali kutoka kwa wabunge, watoa mada hao walisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu huku wakikosa hata ulinzi licha ya kuwa wako katika vishawishi vikubwa.
Nzowa alisema wamekuwa wakipata taabu kubwa licha ya mazingira ya kufanyia kazi kuwa ni magumu, lakini hawana hata chembe ya ulinzi wowote.“Mimi natumia Zaburi ya 21 na ya 120 kwamba namtegemea Mungu tu maana kazi ni ngumu kweli…,’’ alisema Nzowa.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bakwata, Kanisa Katoliki watajwa dawa za kulevya
0 comments