IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAKATI polisi wakituhumiwa kuendeleza wimbi la mauaji dhidi ya raia kwa kujichukulia sheria mkononi, serikali nayo imetakiwa kufuta nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya ili kupunguza matumizi.
Tayari, polisi imekuwa wanatuhumiwa kwa matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya raia kwa baadhi ya matukio.
Ripoti ya nusu mwaka ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), iliyotolewa jana inabainisha kuwa polisi wamekuwa wakitumia nguvu kuua raia na kwamba, kipindi cha miezi sita watu 20 walikufa wakiwa mikononi mwa vyombo vya sheria.
Akitoa ripoti hiyo, Mtafiti wa LHRC, Onesmo Olengurumwa, alisema mambo hayo yamekuwa yakitokea kutokana na serikali kukosa utawala bora.“Serikali iliyopo imekosa utawala bora ndiyo maana ukiukaji wa haki za binadamu unafanywa na kila mtu, tume zinazoundwa na serikali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa jambo lililotokea hazijawahi kutoa taarifa na serikali haijawahi kuchukua hatua zozote, unafikiri kwa miaka ijayo nini kitatokea?,” alihoji.
Pia, alisema serikali inatakiwa kufuta idara za wakuu wa mikoa na wilaya ili kupunguza fedha nyingi zinazotumika na kwamba, iliunda mikoa mipya lakini hadi sasa haijatenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya mikoa hiyo.
“Hakuna haja ya kuwa na wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala waliopo kwenye mikoa wanaweza kufanya kazi vizuri, utashangaa ukienda ofisi hizo utakuwa watu wanakaimu, imeanza kujidhihirisha kwani mpaka sasa serikali imeshindwa kuteua wakuu wa mikoa,” alisema.Olengurumwa alisema serikali imeshindwa kuwekeza nguvu zake kwa jamii kuhakikisha maendeleo ya rasilimali zake.
“Viongozi wameshindwa kuwa wazi kwa wananchi ingawa katiba inaelekeza kuwa wawazi imeshindwa kudhibiti rushwa, katiba mpya inayozungumziwa kila kukicha, hata tatizo la umeme lililopo imeshindwa kulipatia ufumbuzi, hii ni kwasababu hakuna usawa kati ya mwenye nacho na asiyenacho,” alisema Olengurumwa na kuongeza:
“Hakuna matumizi endelevu ya maliasili. Serikali imeshindwa kutoa matokeo katika kukidhi mahitaji ya jamii wakati inatumia maliasili.” Alisema mipango ya maendeleo mbalimbali ni imara, lakini serikali imeshindwa kutekeleza na kwamba ongezeko la uhalifu wa kimataifa ya usafirishaji wa wanyama na dawa za kulevya, serikai imeyakalia.
Naye Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Uwezeshaji wa LHRC, Imelda Urrio, alisema serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha tafiti hizo zinafanyiwa kazi, ili kupunguza ukiukaji wa haki za binadamu nchini.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - LHRC yapendekeza wakuu wa mikoa, wilaya wafutwe
0 comments