IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka madiwani wake wote wa Arusha, akiwamo Naibu Meya, Estomih Mallah, kujiuzulu nyadhifa zote walizopata katika Jiji hilo bila kufuata utaratibu wa chama hicho.
Pia kimeunda kamati ya watu watano kwa ajili ya kufuatilia na kuchunguza malalamiko yaliyotolewa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika dhidi ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, kuwa amekiuka maadili ya wabunge wa Chadema na kuonesha utovu wa nidhamu kwa kuwatuhumu hadharani viongozi wake.
Pamoja na Millah, wengine wanaotakiwa kujiuzulu nyadhifa zao Arusha ambao ni madiwani wa chama hicho ni pamoja na wenyeviti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Kamati ya Elimu na Afya na Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alisema Chadema haina njaa wala kiu ya madaraka yaliyopatikana kutokana na maridhiano ya mgogoro wa umeya Arusha na kuwataka wote waliopewa madaraka katika maridhiano hayo wajiuzulu.
“Jana (juzi) Kamati Kuu ya chama hiki ilikuwa na mkutano na kati ya ajenda zake nyingi, pia ilijadili ripoti ya kamati maalumu iliyoundwa chini ya uenyekiti wa Mwanasheria wetu, Mabere Marando na kutokana na ripoti hiyo, kamati imeamua kutotambua maridhiano ya umeya Arusha,” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia ripoti ya Kamati ya Marando, alisema ilibainisha kuwa hakukuwa na vikao rasmi vya ngazi ya chama katika kujadili maridhiano hayo, kutokana na ukweli kuwa mgogoro huo wa umeya ni wa kisiasa, hivyo hata maridhiano yake yangehitajika kufanyika kupitia vyama vya siasa na si Baraza la Madiwani.
Alisema pia ripoti hiyo ilibaini kuwa taratibu na kanuni za Chadema kuhusu uteuzi wa wawakilishi katika vyombo mbalimbali vya serikali hazikufuatwa kikamilifu kama ilivyopaswa.
“Huyu Naibu Meya na wenzake walitakiwa kujaza fomu ambayo ingejadiliwa na chama na kupitishwa, lakini katika hili, kumekuwa na barua iliyoandikwa kwa Mkurugenzi ambaye saini yake imeghushiwa,” alisema Katibu Mkuu.
Aidha, alisema tayari ameanza mchakato wa kuwaandikia barua madiwani hao waachie nyadhifa hizo na iwapo watakiuka, chama hicho kitawachukulia hatua kwa mujibu wa Katiba yake. Hata hivyo, madiwani hao wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao jana wakiwa Arusha, walisisitiza kuwa msimamo wao ni ule ule wa kutambua mwafaka huo kwa maslahi ya watu wa Arusha.
Walisema wanasubiri barua rasmi ya uongozi wa Chadema Taifa ili kutoa tamko lao rasmi kuhusu uamuzi huo wa kutakiwa kujiuzulu nyadhifa hizo wanazoshikilia sasa Arusha.
Akizungumzia suala la Shibuda, Dk. Slaa alisema, Mnyika aliwasilisha malalamiko yake Julai 14 juu ya utovu wa nidhamu na kukiuka kwa maadili ya wabunge wa Chadema aliouonesha Shibuda kupitia vyombo vya habari na kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Mnyika alitumia vifungu vya Katiba ya chama hicho ambavyo vimeweka wazi kuwa mbunge hatakiwi kutoa taarifa za uzushi, kifisadi dhidi ya chama au viongozi wake nje ya chama na kukashifu chama.
Alisema Kamati hiyo, baada ya kupokea malalamiko hayo iliyajadili ili kuona mantiki kwanza kama Katiba ya chama hicho inavyotaka na kuona kuwa yanastahili kufanyiwa kazi na hivyo kuunda kamati ya watu watano ikiongozwa na Mwanasheria wao, Profesa Abdallah Safari.
Alisema Profesa Safari na wenzake, watatakiwa kuchunguza malalamiko hayo na kuwaita Mnyika na Shibuda kwa nyakati tofauti, ili kuwapa nafasi ya kujieleza na baada ya hapo wataandika ripoti ya uchunguzi wao na kuiwasilisha kwa Kamati Kuu ambayo itaijadili na kutoa uamuzi kwa manufaa ya chama.
“Nataka hili mlifahamu, malalamiko dhidi ya Shibuda hayahusiani kabisa na aliyosema bungeni, wala kamati ya wabunge wa chama hiki haijawasilisha malalamiko yoyote juu ya kauli ya Shibuda.
“Haya ni malalamiko ya utovu wa nidhamu ambayo Mnyika aliwasilisha na ndio tuko kwenye mchakato wa kuyafanyia kazi wala hayahusiani na posho,” alisema Dk. Slaa.
Katika malalamiko dhidi ya Shibuda, ni madai aliyotoa Julai 3 kwa baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya chama chake na viongozi wake ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu Kabwe Zitto na kuahidi kufichua zaidi uovu wao.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Chadema yataka madiwani wake ‘wajivue gamba’
0 comments