IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KAMATI ya Bunge ya Miundombinu imemwagiza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kuendelea kuwavunjia nyumba wananchi ambao wamejenga ndani ya hifadhi za barabara kama sheria inavyotaka.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, amewaambia waandishi wa habari jana kuwa ili nchi iendelee, ni lazima wananchi wake waheshimu sheria na si vinginevyo.
Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), alisema kamati yake imeridhika na kazi inayofanywa na wizara hiyo kwa kuwa ndani ya miaka miwili kuanzia sasa, kilometa 11,000 za barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami, zitakuwa zimekamilika.
“Wizara hii inafanya kazi vizuri na ili nchi hii iendelee ni lazima tusimamie sheria, wale ambao wamejenga kwenye hifadhi za barabara waondoke, wakigoma wabomolewe,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema kamati yake imepitisha bajeti ya wizara hiyo ya Sh trilioni 1.4 kwa vile imeonesha ujenzi wa miundombinu kwa kasi. “Pia wameonesha watajenga daraja la Kigamboni, Malagarasi na Kilombero, kwa kweli tunawapongeza.”
Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alimtaka Waziri Magufuli kupunguza kasi ya kubomoa nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi za barabara, agizo ambalo lililalamikiwa na baadhi ya wachambuzi wa mambo kuwa ni la kisiasa.
Pia Rais Kikwete wakati alipotembelea wizara hiyo alitaka staha itumike katika bomoa bomoa hiyo na kumuagiza waziri huyo awape taarifa wananchi watakaobolewa.
Rais Kikwete pia aliilaumu wizara hiyo kwa kuchangia watu kujenga kwenye hifadhi za barabara kwa kuwa hatua hazikuchukuliwa wakati ujenzi ulipokuwa ukianza.
Kwa upande wa Wizara ya Uchukuzi, Serukamba alisema kamati yake bado haijaridhika na bajeti ya wizara hiyo kwa kuwa haikutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa reli na kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATC).
“Reli ni moja ya vipaumbele vya Taifa kwa sasa, lakini haikupangiwa bajeti, sasa tutatekelezaje ukarabati wa reli hiyo?” Alihoji Serukamba.
Alisisitiza kuwa, kamati yake itabadilisha uamuzi na kupitisha bajeti hiyo iwapo itaonesha marekebisho ya fedha zilizoelekezwa kufufua mashirika hayo.
Mwenyekiti huyo alisema bila reli, uchumi wa Taifa hautaendelea na barabara zinazojengwa zitaharibika haraka kwa kuwa zitabebeshwa mzigo mzito.
Pia kamati hiyo imepitisha bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ya Sh bilioni 64 ambapo Serukamba alisema miongoni mwa kazi walizoainisha kuzifanya ni kuendeleza Mkongo wa Taifa, kuendeleza Chuo cha Nelson Mandela, kufanya utafiti na kusimamia vizuri mtandao wa simu nchini.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wabunge wamtaka Magufuli aendelee kubomoa
0 comments