Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wabunge waibana bodi feki, Zitto aitimua

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter BODI feki ya Wakurugenzi katika Shirika la Masoko la Kariakoo, mkoani Dar es Salaam imekaa katika shirika hilo kwa miaka 11 na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja na upotevu wa mali za shirika hilo.


Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Alhaji Bakari Kingobi, alikiri kuwa uteuzi wake na wa Meneja Mkuu wa Shirika hilo, si halali.


Alhaji Kingobi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, alifafanua kuwa aliteuliwa kushika wadhifa huo na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) badala ya Rais kama ilivyo kisheria.


Kutokana na kukosekana kwa uhalali wa nafasi yake katika Shirika hilo la umma, Kingobi aliyekaa katika wadhifa huo tangu mwaka 2000, alisema aliandika barua Tamisemi kuomba uteuzi mpya, lakini hakujibiwa.


Kabla ya kuanza kujieleza kuhusu uhalali wake, Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe na baadhi ya wabunge wa kamati hiyo, walihoji uhalali wa Bodi hiyo kujitokeza na kutaka kujibu hoja za Kamati ya Bunge wakati ikitambua kuwa haiko katika nafasi hiyo kihalali.


“Sisi Kamati tunataka kujua uhalali wa nyie kuja mbele yetu kama Bodi, kwa kuwa tunatambua Sheria ya Shirika la Masoko ya Kariakoo ya mwaka 1974 inasema wazi kuwa Mwenyekiti wa Bodi na Meneja Mkuu, watateuliwa na Rais, nyie hakuna hata mmoja wenu mwenye sifa hiyo,” alisema Zitto.


Alisema, Kamati hiyo haiwezi kuendelea kuzungumza na ujumbe huo, kwa kuwa hauko hapo kihalali na kwa mujibu wa sheria, hawaruhusiwi kujibu chochote.


“Hatuwezi kuzungumza na watu ambao si wenyewe wanaotakiwa, Shirika hili lina matatizo mengi yanayohitaji kujibiwa na wahusika, nyie tunasema kwaherini,” alisema Zitto.


Zitto alisema shirika hilo lina matatizo mengi ambayo yalisababisha hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kulikagua.


Alitaja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja, mali kutumika vibaya, kupotea kwa viwanja na baadhi ya wateja kujimilikisha mali za Shirika.


Alitolea mfano wa nyumba ambayo ni mali ya Shirika hilo ambayo hakuitaja ilipo ambayo mteja wake amejimilikisha na hati anayo huku uongozi ukishindwa kufanya chochote.


“Lengo la Kamati ni kuhakikisha kuwa Shirika linarudi kwa manispaa za Dar es Salaam na kwa sasa Serikali ina hisa 49 na zilizobaki ni za manispaa,” alisema Zitto.


Alisema Kamati itawasiliana na Tamisemi, ili kuhakikisha wanateua Bodi haraka iwezekanavyo na kujibu hoja zinazolikabili Shirika hilo.


“Lakini nyie mmekuwa mkifanya kazi kinyume kabisa na sheria na hata kutoa fedha kwenye akaunti ya Shirika ni kosa,” alionya.


Mbunge wa Lindi, Jerome Bwanausi (CCM), alisema alishawahi kuwa Meya wa Manispaa ya Temeke na anatambua uozo wa Shirika hilo, huku akitolea mfano wa jengo la Mbezi ambalo alidai mteja wa Shirika hilo, amemilikishwa wakati bado ni mali ya Shirika.


Kwa mujibu wa Sheria, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, huteuliwa na Rais na hushika wadhifa huo kwa muda wa miaka mitatu wakati Meneja Mkuu hushika wadhifa huo kwa miaka mitano.

0 comments

Post a Comment