Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Vipaumbele 5 muhimu bajeti ya Serikali 2011/2012

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SERIKALI imesema misingi kadhaa ikiwamo kupunguza misamaha ya kodi na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, ikitekelezwa kama ilivyokusudiwa, itaweza kugharamia vipaumbele vitano muhimu katika Bajeti ya Serikali ya 2011/2012; cha kwanza ikiwa ni nishati na umeme.

Vipaumbele vingine kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ni usalama wa chakula; miundombinu; ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei.

Mkulo amevitaja vipaumbele hivyo bungeni wakati akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2010 na Malengo ya Uchumi katika kipindi cha muda wa kati wa 2011/12 – 2015/16.

Mkulo amesema,vipaumbele hivyo vinatokana na changamoto zinazowakabili wananchi katika kukabiliana na hali ngumu ya maisha kwa hivi sasa na umuhimu wa kujenga uchumi imara na wenye ushindani.

Katika umeme, alisema Serikali inakusudia kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa uhakika wa umeme ili kuziwezesha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii kufanyika kwa wakati wote.

Kuhusu usalama wa chakula, Mkulo alisema nia ni kuongeza upatikanaji wa chakula kwa kuhimiza kilimo hasa cha umwagiliaji na kuimarisha hifadhi ya chakula ili kujikinga na tatizo la uhaba wa chakula nchini.

“Kuimarisha miundombinu ya maji, reli, bandari na barabara pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam,” alifafanua Waziri Mkulo kuhusu kipaumbele cha tatu.

Kwa upande wa ajira, alisema inakusudiwa kuongeza fursa za ajira na kuwanufaisha wananchi walio wengi hasa vijana ambao ndio kundi kubwa la soko la ajira.

Aidha, alisema wizara, idara na taasisi za Serikali zinaelekezwa kuzingatia suala la kuongeza ajira katika maeneo yao.

“Mfumuko wa bei umesababishwa na kuongezeka kwa wastani wa bei za chakula; bei za mafuta; umeme na gharama za usafirishaji. Hatua zitachukuliwa kudhibiti ongezeko la bei za mafuta, bei za chakula na kuongeza uzalishaji wa umeme,” Mkulo aliliambia Bunge.

Akizungumzia msingi na malengo ya uchumi na maendeleo ya jamii, alisema malengo ya sera za uchumi jumla katika mwaka 2011/2012, yatakuwa saba ikiwamo Pato halisi la Taifa litakua kwa asilimia 6.0 mwaka 2011 na asilimia 7.2 mwaka 2012.

Mengine ni kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji wa bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja na kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano wa asilimia 17.2 ya Pato la Taifa mwaka 2011/12 na kuendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 17.5 kwa mwaka kwa kipindi cha muda wa kati.

“Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi unaotarajiwa kukua kwa asilimia 19.0 mwaka 2011/12 na asilimia 18.6 kwa mwaka 2012/13; Ukuaji huu unalenga kuwiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji wa bei.

“Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.6; kupunguza tofauti ya viwango vya riba na kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha,” alieleza Mkulo kuhusu malengo ya sera ya uchumi jumla.

Mkulo alisema malengo hayo yatafikiwa kwa kuzingatia misingi kadhaa ikiwamo kuendelea kuimarika kwa amani, utulivu na utengamano; vyanzo vya maji vitaendelea kuhifadhiwa na kukidhi mahitaji.

Misingi mingine ni utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii utaendelea kuimarika; mapato ya ndani yataongezeka na kuboreshwa ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya kodi.

Pia kuimarisha ukusanyaji wa kodi ya majengo na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia vipaumbele vilivyoainishwa.

0 comments

Post a Comment