Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Uamuzi wa Milya kufukuzwa kujulikana leo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MBIVU na mbichi kuhusu hatma ya kumyang'anya kadi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, James Ole Milya sanjari na vijana wanne, leo itajulikana.


Wakati kikao hicho kikitarajia kuketi kesho tayari wenyeviti wa CCM kutoka wilaya zote mkoani Arusha hivi karibuni walikutana na kujadili hali ya mgogoro mkoani hapa na kutoa mapendekezo manne ya namna ya kuutatua mgogoro huo.


Moja ya njia za kutatua mgogoro huo ni kumwondoa mjumbe mmoja wa mkutano wa kesho, Mary Chatanda ambaye ni Katibu wa CCM mkoani hapa kwa madai kwamba yeye ni chanzo cha mgogoro huo.


Tayari baadhi ya vijana wa umoja huo kutoka wilaya mbalimbali mkoani Arusha wakihojiwa kwa nyakati tofauti jana na Mwananchi wameahidi kuweka kambi katika viunga vya jengo hilo usiku wa kuamkia leo huku wakiwatahadharisha wajumbe wa kikao hicho kuwa endapo wakiamua kumfukuza Milya wao wako tayari kurudisha kadi za CCM na kuhamia upinzani.


Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinadai kuwa kikao hicho kinatarajia kuketi leo kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka majira ya usiku na taarifa zinadai kwamba tayari wajumbe mbalimbali wa kikao hicho wamegawanyika katika makundi katika baadhi ya hoja zitakazowasilishwa hususani ya kumfukuza uanachama Milya.


Ajenda zitakazowasilishwa mbele ya kikao hicho ni pamoja na kuwafukuza wanachama wanne wa UVCCM mkoani hapa ambao ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Ally Bananga, Ally Majeshi na John Nyiti ambaye ni katibu wa vijana kutoka wilayani Arumeru.


Taarifa hizo pia zinadai kuwa kikao hicho pia kitakwenda kuamua hatma ya mjumbe wa Baraza la Vijana Taifa, Mrisho Gambo ambaye alituhumiwa na vijana wenzake hivi karibuni mbele ya tume ya maadili na usalama kwamba alipewa Sh60 milioni na mmoja wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne.


Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole alisema kikao hicho kitafanyika na kwamba ajenda kuu itakuwa ni kujadili hali ya kisiasa ndani ya CCM, mkoani Arusha ambayo inaelezwa kuwa tete.


“Hayo mambo ya kuvuliwa uanachama siwezi kuyazungumzia, lakini ni kweli tunakutana kesho na ajenda kuu ni kujadili hali ya kisiasa ya ndani ya chama chetu hapa mkoani Arusha,”alisema Nangole.


Naye, Milya alipoulizwa kuhusu nini maoni yake kuhusu hatama ya kuvuliwa uanachama na kunyanganywa kadi ya CCM, alisema kuwa yote anawaachia wajumbe wa kikao hicho ndio watakaoamua kusuka ama kunyoa.


Baadhi ya vijana ambao nao wametajwa kufukuzwa ndani ya chama hicho, kwa nayakati tofauti walisema hawana wasiwasi, lakini walionyesha kusikitishwa na hatua ya kikao hicho kujadili uamuzi wa kumtaka Chatanda aondoke huku kundi lingine linalowashambulia Edward Lowasa, Rostam Aziz na Andrew Chenge likiachwa bila sababu za msingi.


“Sisi tunashanga kitu kimoja pamoja na kuambiwa kuwa halmashauri kuu kesho itakwenda kutufukuza kesho ndani ya chama kwa kumtaka Chatanda aondoke, lakini tunashangaa mbona lile kundi lingine lililowashambulia viongozi waandamizi ndani ya chama halijajadiliwa huu ni uonevu wa wazi wazi,”alisema mmoja wa vijana hao.

0 comments

Post a Comment