Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Ni vita ya posho bungeni Dodoma

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MBOWE ASEMA NI WIZI WA KITAASISI, MKULO AWAANDALIA MTEGO CHADEMA


WAKATI Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiunga mkono hoja ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe ya kutaka kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wote wa umma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo amesema anasubiri hoja hiyo itakapowasilishwa bungeni. Mbowe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha ndani cha wabunge wa chama hicho alisema hoja ya kufutwa kwa posho siyo ya Zitto peke yake na kwamba mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini anasakamwa bure kwa kudhaniwa kwamba anatafuta umaarufu wake binafsi.


Wabunge wa CCM na Chadema jana wakuwa na vikao vya ndani kwa ajili ya kuweka mikakati ya kujadili Bajeti Kuu ya Serikali, iliyowasilishwa bungeni Jumatano iliyopita. Mjadala wa bajeti unatarajiwa kuanza rasmi Jumatano ijayo.


Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema posho zinazotakiwa kufutwa ni kwa watumishi wote wa umma ambao wamekuwa wakilipwa fedha za vikao hata wanapokuwa katika mazingira ya kutekeleza wajibu wao wa kila siku.


"Tumekokotoa na tunaendelea kukokotoa na inaelekea tunaweza kuokoa hadi kiasi cha Sh900 bilioni ikiwa posho zote zitafutwa, hili linawezekana kama tutakavyoonyesha katika bajeti yetu mbadala tutakayowasilisha Jumanne ijayo," alisema Mbowe.


Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema wabunge wamekuwa wakilipwa mishahara kwa mwezi pamoja na fedha za kujikimu (per diem) wanapokuwa nje ya majimbo yao kikazi na kwamba wanachopinga ni "posho za vikao" (sitting allowance) ambazo ni kikwazo cha utekelezaji wa kazi za Serikali na majukumu mengine katika ofisi za umma.


Alisema utoaji wa fedha za vikao uliasisiwa na Bunge na umesambaa taratibu katika taasisi nyingine za umma na kusababisha watendaji kutunga semina na vikao vingi alimradi wanapata posho huku kazi nyingine zikiendelea kulala.


"Kwa mfano, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi (ya Bunge), nasaini 'sitting allowance' katika kikao cha Bunge, nikiitwa katika kikao cha kamati ya uongozi nasaini tena sitting allowance na hata kama kutakuwa na kikao kingine jioni naweza kulipwa, sasa kama huo siyo wizi ni nini?"


"Huu ni wizi wa fedha za umma ambao umetaasisiwa na sasa unaathiri utendaji katika mfumo mzima wa serikali, si fedha tu kwani hata kazi zinalala kwani watendaji wote wanakimbilia kwenye vikao vya kutunga kwa sababu kuna posho na si vinginevyo."


Alisema hoja si malipo ya posho kwa wabunge wa Chadema pekee, bali kwa watumishi wa nchi nzima ambao ni zaidi ya 500,000 na kwamba malipo ya posho hizo yamesababisha kuwepo kwa tofauti kubwa ya kipato baina ya watu walioko kwenye menejimenti na watumishi wengine.


"Hawa wakubwa, wakurugenzi na wakuu wa idara wanapokutana kwenye vikao vyao na kulipana posho, tujiulize madereva na wafagiaji wanakutana lini na wanalipana nini? Haya ndiyo mambo yanayoleta chuki katika utendaji kwani wengine wanakuwa matajiri huku wengine wakibaki mafukara," alisema.


Alisema pamoja na kwamba wabunge wa Chadema akiwamo yeye wanachukua posho hizo, kamwe hawataacha kusema kwani tatizo si wao kuchukua, bali sera inayoruhusu ufujaji huo wa mali ya umma.


Mbowe alisema kama suala ni mishahara midogo hilo ni jambo linalozungumzika na kwamba Serikali inaweza kujenga hoja na kuipandisha kwa kiwango kitakachowezesha watumishi wa umma wakiwamo wabunge kujikimu, lakini si kuweka posho ambazo zinawanufaisha wachache na kujenga matabaka miongoni mwa watumishi wa umma.


Alisema katika bajeti yao mbadala watatoa mapendekezo magumu ambayo watendaji wa serikali hawajazoea kuyatekeleza na kwamba ikiwa hoja zao zitakataliwa, watakuwa wametimiza jukumu lao ndani ya Bunge.


"Wao ni wengi, wanaweza kukataa hoja hizi ndani ya Bunge, lakini sisi tunafanya siasa ndani na nje ya Bunge, sasa kama wao ni wengi kuliko hao walioko huko nje basi tutajua," alisisitiza.


Kauli ya Mkulo
Mapema Waziri Mkulo kwa upande wake alisema: "Nawasubiri ndani ya Bunge, kwa sababu waziri kivuli ni ndani ya Bunge, sasa kama wakileta mapendekezo hayo mimi nimejiandaa tayari maana huu ni unafiki tu."


Mkulo aliyewasilisha Bajeti ya Serikali bungeni siku tatu zilizopita, alisema ikiwa wapinzani watabeba ajenda hiyo, basi atawaandalia fomu kwa wale wasiotaka posho ili wakajaze na fedha hizo zipelekwe kwa wahitaji wa misaada mbalimbali.


"Nitakapohitimisha hatua yangu nitawaandalia fomu kwa Katibu Mkuu Hazina na nitawaelekeza kama hawataki posho hizo basi wakajaze fomu tuone kama kuna mtu atakayekwenda," alisema Mkulo na kuongeza kuwa kauli ya Zitto ni ya kutafuta umaarufu usiokuwa na msingi.


Alisema Zitto si mkweli kwani mapendekezo ya posho za vikao hupitishwa na kikao cha Kamati ya Uongozi ambacho pia huwashirikisha wapinzani na kwamba kiasi cha Sh70,000 kwa siku wanacholipwa wabunge kilipitia katika mfumo huo unaowashirikisha wapinzani.


"Sasa huu ni mchezo wa ajabu, maana kule wanakaa wanapitisha halafu huku mtu anageuka na kusema hataki," alisema Mkulo.


Akizungumzia tamko la Zitto kuhusu madai ya upotoshaji katika bajeti, Mkulo alikiri kwamba kulikuwa na makosa katika suala la faini ya Sheria ya Usalama Barabarani na kwamba mabadiliko aliyoyasoma hayakuwa yamechapishwa kwenye vitabu kutokana na marekebisho kufanywa dakika za mwisho.


"Tulipokea ushauri wa polisi kuhusu suala hili na baada ya Cabinet (Baraza la Mawaziri), kupitisha mabadiliko hayo tulipeleka taarifa Ofisi za bunge, sema tu kwamba vitabu vilikuwa vimeshachapishwa," alisema.


Kuhusu fedha zilizotengwa kwa ajili ya umeme, Waziri huyo alisema si kweli kwamba hakutakuwa na miradi mipya kama Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alivyodai katika taarifa yake, bali alisema fedha nyingi zimewekwa Hazina badala ya kuwekwa katika wizara za kisekta kutokana na masharti yaliyotokana na jinsi zilivyopatikana.


"Kwa mfano hata fedha za Millenium Challenge Account (MCA), kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya kule Sumbawanga, haziko kwenye akaunti ya Wizara ya Ujenzi, haziwezi kuwa huko kwani masharti yake hayaruhusu, sasa watu hawa jamani wasome Bajeti na maelezo mengine ya ziada," alisema Mkulo.


Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema ni mapema kuzungumzia hoja ya Chadema kuhusu posho, lakini akaahidi kwamba anasubiri hadi itakapowasilishwa rasmi bungeni na upande huo wa upinzani.


"Si vizuri nikaanza kujibizana na mbunge mmoja mmoja, lakini kwa sababu wamesema wataileta kama kambi ya upinzani hapo itakuwa hoja rasmi, tusubiri wakati huo," alisema Ndugai.

0 comments

Post a Comment