Bishop-elect Stanley Hotay of Mount Kilimanjaro |
Wakati Mahakama Kuu ikizuia Askofu Hotay kusimikwa kesho, maaskofu na viongozi mbalimbali wa kanisa hilo wa ndani na nje ya nchi, walikuwa tayari wamewasili Arusha kwa ajili ya ibada hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Jakaya Kikwete.Waumini waliofungua kesi hiyo ni Lothi Oilevo, Godfrey Mhone na Frank Jacob wanaotoka Parishi ya Mtakatifu James katika jimbo hilo ambao pia ilielezwa ni wajumbe wa Baraza la Walei.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Kakusuro Sambo alisema baada ya kusikiliza maombi ya walalamikaji kutaka kesi hiyo isikilizwe kwa dharura na hoja zilizowasilishwa na mawakili wa pande zote, Meinrad D’souza upande wa mashtaka na Arbert Msando upande wa utetezi, mahakama haikuwa katika mazingira bora ya kisheria ya kutoa uamuzi.
Jaji Sambo alisema atatoa uamuzi wa shauri hilo Jumatatu na hivyo kwa kuwa leo na kesho hakuna kazi, ni marufuku kuendelea kwa jambo lolote ambalo litaingilia shauri hilo.
Awali, Wakili D’souza aliieleza Mahakama kuwa kusimikwa kwa Askofu huyo Jumapili, kutaathiri kesi ya msingi ya wateja wake ambao wanalalamikia taratibu mbalimbali za kanisa hilo, ikiwamo ya kukiukwa kwa katiba hadi kuteuliwa kwa askofu huyo.
Hata hivyo, Wakili Msando alipinga hoja hiyo na kuiomba Mahakama kutupilia mbali shauri hilo akisema ina upungufu wa kisheria ikiwapo walalamikaji kushindwa kutoa malalamiko yao dhidi ya ushindi wa Hotay kwa kufuata taratibu za Kanisa tangu ulipofanyika uchaguzi Aprili, 15 mwaka huu.
Wakili Msando pia aliieleza Mahakama kuwa, maombi ya walalamikaji hayo yana upungufu kisheria kwani mmoja wa walalamikaji, Geodfrey Mhone hana hati ya kiapo kuthibitisha madai yake na pia yeye na wenzake hawana uwakilishi wa taasisi yoyote ya kanisa hilo au kutambuliwa kuwa ni waumini wa kanisa hilo.
“Walalamikaji kama wanajua taratibu za kanisa walipaswa kutoa malalamiko yao katika kanisa hilo tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu, mwezi Aprili, lakini wamekaa kimya hadi dakika za mwisho Askofu anataka kusimikwa ndipo wanawasilisha kesi na maombi yao, tayari kadi zimetolewa, chakula kimeandaliwa na maandalizi yote yamekamilika,” alisema Msando.
Wakili Msando akinukuu kesi kadhaa kuhusiana na kuomba kusikilizwa chini ya hati ya dharura na hivyo akaiomba mahakama kutupilia mbali maombi ya kutaka kusitishwa kusimikwa kwa askofu huyo.Hata hivyo, Wakili D’souza alisema wateja wake wana haki ya kufungua shauri hilo kwani ni Wajumbe wa Baraza la Walei katika Kabisa la Mtakatifu James na hakuna kifungu cha sheria ambacho kimekiukwa na wateja wake kuwasilisha shauri hilo mahakamani.
Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ilipanga kumsimika askofu Hotay, kuchukua nafasi ya Askofu Saimon Makundi baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika Aprili 15, mwaka huu ukimshirikisha mgombea mwingine, Dk Emmanuel Mbena.
Waumini hao, wamefungua madai mawili ambayo ni kesi na madai namba 18/2011 na kesi ya jinai namba 48/2011 na washtakiwa ni Maaskofu wote wa kanisa hilo na mshtakiwa wa pili ni Askofu Hotay.
Katika shauri la jinai, waumini hao wameeleza kuwa ushindi alioupata, Askofu Hotay wa kuongoza kanisa hilo lenye Parishi 30, ni batili wakidai kuwa amegushi umri ambao unampa sifa ya kugombea uongozi.
Wanadai kuwa katiba ya Kanisa la Anglikana inaeleza bayana kuwa mchungaji wa kanisa hilo anayeweza kufikiriwa kutwaa cheo hicho cha uaskofu, anatakiwa awe na miaka kati ya 40 na 60. Inadaiwa kuwa Askofu Hotay mwaka jana alikuwa na miaka 38.
Waumini hao watatu wameiomba Mahakama itoe tamko kuwa Hotay amedanganya katika cheti chake cha kuzaliwa cha Februari 12, mwaka jana na kwamba kilitolewa kwa njia ya udanganyifu, hivyo mchakato wote wa uchaguzi ukiwamo wa Aprili 15 mwaka huu uliomweka madarakani pia ni batili.
Aidha, wameiomba Mahakama kutamka kwamba kifungu cha 14 (8) cha Katiba ya Kanisa hilo ni batili kwa kuwa kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa fursa sawa mbele ya sheria na watu wake wasioridhika kufika mbele ya sheria na kupatiwa haki zao.
Pia wameiomba mahakama izuie kusimikwa kwa askofu huyo ambaye wanadai kuwa ametoa taarifa za uongo kwa Msajili wa Vizazi na Vifo (Rita) kuwa alizaliwa 1969 wakati Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilboru alikosoma alidai kuwa amezaliwa mwaka 1972.
0 comments