Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - CUF yang'ang'ania kuandamana kesho

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
LICHA ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuzuia CUF kuandamana, chama hicho kimesema maandamano yako palepale, kilivyopanga. Juni 6, mwaka huu, CUF ilitangaza kufanya maandamano makubwa kesho kuanzia saa 3:00 asubuhi kutoka Ubungo hadi Manzese Bakheresa, lengo likiwa kupinga mauji yanayofanywa na polisi dhidi ya raia nchini.




Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alisisitiza kuwapo kwa maandamano hayo aliyoyaita ya kupinga vitendo vya kinyama vya mauaji vinavyofanywa na polisi. Alisema tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1945, linatoa haki ya kuandamana ikiwa watu au chama kinataka kuonyesha hisia zake kwa jamii na kwamba, Tanzania ni mjumbe wa umoja huo na imeridhia tamko hilo


. “Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, ambayo tayari ina viraka zaidi ya 14 inatoa haki kwa raia wa Tanzania, vikundi au taasisi kutoa mawazo au hisia zao na hii iko kifungu cha kwanza Ibara ya 20,” alisema.


Alisema kifungu cha 43(1) cha sheria za polisi na polisi wasaidizi sura ya 322, kama ilivyoandikwa upya mwaka 2002, kinaeleza kuwa waandamanaji wanapaswa kutoa taarifa ya maandamano kwa ofisa wa polisi saa 48 kabla ya maandamano, kitu ambacho kimefanywa na CUF. Mtatiro alisema kifungu cha 43(3), kinaeleza kuwa ofisa wa polisi hawezi kukataza maandamano chini ya kifungu cha 43 (2), isipokuwa, iwapo atajiridhisha kuwa mkusanyiko huo utasababisha uvunjifu wa amani au kuathiri usalama wa nchi.


Alisema maandamano yatakayofanywa na CUF yatakuwa ya amani na kwamba, hayatakuwa na silaha za moto isipokuwa watabeba mabango na kufikisha ujumbe waliokusudia kwa wananchi. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema maandamano hayo ni batili kwa sababu yatapelekea uvunjifu wa amani.


Kova alisema maandamano hayo yamesitishwa kutokana na kuwapo kwa kesi mbalimbali za jinai, ambazo zimefunguliwa mahakamani wilaya za Tarime na Urambo, sambamba na matukio ya vifo vinavyodaiwa kusababishwa na polisi. “Ili kuhakikisha hali ya usalama na amani iliyopo inaendelea na kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 43 (1-6) cha sheria za polisi na polisi wasaidizi sura 322 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, nasitisha maandamano na mkutano huo,” alisema Kova na kuonya:
“Yeyote atakayekiuka maagizo haya, polisi itawajibika kuchukua hatua kali za kisheria.”


Kova alisisitiza kuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime kuna mashauri ya jinai matatu na Wilaya ya Urambo idadi kama hiyo, huku yote yakiwa na uhusiano wa moja kwa moja na malalamiko ya chama cha CUF.


Alisema kitendo cha kulaani askari kwa vifo hivyo ni sawa na kutoa hukumu kinyume na katiba ya nchi, ambayo ndiyo sheria mama, ni vyema na busara kusubiri matokeo ya uchunguzi wa mashauri hayo kabla ya kuchukua hatua zingine za maandamano na mkutano. Kamanda Kova alisema iwapo chama hicho hakitaridhika na uamuzi huo, kina haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini siyo vinginevyo. Imeandaliwa na Elizabeth Ernest, Timothy Marko, Ellen Manyangu na Aziza Masoud

0 comments

Post a Comment