Katibu wa Bunge Bw. Thomas Kashililah akimtetea Spika wa Bunge Anne Makinda |
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Gaudence Nyamwihula alisema jana kwamba Spika Makinda amepewa kibali cha muda kufunga barabara hiyo ili awe katika nafasi nzuri ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba yake hiyo na si vinginevyo.
"Kibali alichopewa (Makinda) ni kama kile kinachoweza kutolewa kwa mtu mwingine yeyote iwe kuna shughuli ya msiba, ngoma au ujenzi kama inavyotokea katika maeneo mengine," alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema Spika Makinda hana ruhusa ya kujenga katika barabara aliyoweka uzio na kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Alisema tofauti na madai ya wakazi wa eneo hilo kuwa spika huyo amejenga katika barabara ili kujiongezea kiwanja, Ofisi ya Manispaa ya Kinondoni inamini kuwa jambo hilo haliwezi kutokea na kwamba Makinda ataheshimu taratibu zilizopo.
"Hivi sasa barabara imefungwa kwa muda na ujenzi ukimalizika itafunguliwa na kutumika kama awali," alisema na kuongeza kuwa hakumbuki hasa kwamba spika amepewa kibali cha muda gani, lakini akasistiza kuwa kibali alichonacho ni cha muda ili kupisha ujenzi.
Nyamwihula alisema hakuna mtu aliye na mamlaka ya kufunga barabara moja kwa moja kwa ajili ya matumizi yake, na kwamba ili hilo litokee ni lazima wakubaliane katika ngazi ya mtaa.
Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Ulole Juma Athuman alipoulizwa jana kuhusiana na kauli hiyo alisema anahitaji barua kutoka manispaa inayoeleza pamoja na mambo mengine, muda ambao barabara hiyo itakuwa imefungwa.
Alisema ujenzi wa ghorofa hilo ulianza miaka mitatu iliyopita na kwamba hadi sasa haujakamilika. Alisema tangu ulipoanza, hapakuwa na uzio na kuelezea kushangazwa kwake kuona ukiwekwa sasa na kufunga barabara... “Jambo baya zaidi ni kwamba hata taratibu hazikufuatwa.”
Ulole alisema kama manispaa isipoainisha muda wa kibali hicho, barabara hiyo inaweza kufungwa maisha kwa kisingizio cha kupisha ujenzi akisisitiza kuwa anahitaji kujua yote hayo ili aweze kuyawasilisha katika mkutano na wakazi wa eneo hilo utakaofanyika Jumapili katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kijitonyama.
“Mosi taratibu zimekiukwa kwa Spika Makinda kuziruka mamlaka za mtaa na kata na kwenda kuomba kibali manispaa. Pili, nataka wanieleze itafungwa kwa muda gani kwani ujenzi wa ghorofa hilo una mwaka wa tatu sasa na haujakamilika,” alisema na kuongeza kuwa wananchi katika mkutano huo ndiyo watakaokuwa na uamuzi na siyo yeye.
Alisema mkutano huo ambao umeahirishwa mara mbili kutoa nafasi kwa manispaa kutoa uamuzi, sasa utafanyika Jumapili na maandalizi yake yameanza ikiwa ni pamoja na kutoa matangazo kwa wakazi wa kata hiyo.
Sakata la Spika huyo kuifunga barabara hiyo liliibuka baada ya kubandika kibao kinachoonyesha kuwa imefungwa katika kona unapoanzia Mtaa wa Sahara, mwendo wa dakika takriban tano kwa mguu hadi kufika nyumbani kwake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kijitonyama, Philip Komanya alidai kwamba hakuwa na taarifa za kufungwa kwa barabara hiyo akisema huenda wahusika walimzunguka na kwenda manispaa badala ya kupitia kwake.
Alisema kwamba awali, kulikuwa na maombi ya kutaka kuifunga kwa sababu zilizoelezwa na waombaji kuwa ni za kiusalama jambo ambalo hata hivyo, lilikataliwa katika ngazi ya kata.
Kauli hiyo ya Komanya ilithibitishwa na Msemaji wa Spika, Herman Berege ambaye alikaririwa akisema kwamba bosi wake alikuwa na vibali vyote vya kumruhusu kuifunga barabara hiyo isitumiwe tena na wapita njia na watu wengine na kwa sababu za kiusalama na kwamba hayo yamefanyika kwa baraka zote za Manispaa ya Kinondoni.
Hata hivyo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ilifuatilia sababu hizo za kiusalama na kubaini kwamba hazikuwapo. Mkuu wa wilaya hiyo, Jordan Rugimbana alisema kuwa ofisi yake iliangalia kama pengine kulikuwa na agizo lolote kutoka ngazi za juu lakini akabaini kuwa hakuna kitu kama hicho hivyo suala hilo akaliacha manispaa.
Awali, Komanya aliwataka walioifunga barabara hiyo kuachana na fikra hizo na badala yake kuwashauri kuweka lango la kuingilia na kutokea na mlinzi kwa ajili ya kuhakiki wanaopita na pia muda wa kuitumia, pendekezo ambalo hata hivyo, hawakuliafiki.
Taarifa ya kufungwa kwa muda kwa barabara hiyo imekuja baada ya awali, Mhandisi wa Manispaa hiyo, Urio Athanas kusema kwamba manispaa haishughuliki na barabara za vichochoroni kama hiyo akisema ufungaji wa aina hiyo una taratibu zake za kufuata kuanzia ngazi ya mtaa hadi kata.
0 comments