IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), jana ilimbana Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na watendaji wake kwa kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei nchini ambao umefikia asilimia nane.
POAC imesema kuwa BoT imeshindwa kusimamia utoaji mikopo kwa wakulima wa mazao ya chakula ili kupunguza makali ya mfumuko huo wa bei, badala yake, wakulima wa maua ndiyo wamekuwa wakinufaika na mikopo yake.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Zitto Kabwe alisema hayo baada ya Profesa Ndulu kuieleza kamati hiyo kuwa mfumuko wa bei nchini si wa kutisha, ikilinganishwa na nchi jirani.Gavana Ndulu alisema mfumuko wa bei nchini kwa sasa ni asilimia 8.6 wakati Kenya ni asilimia 14 na Uganda asilimia 12.
Alisema sababu za mfumuko huo wa bei ni kupanda kwa gharama ya mafuta katika soko la dunia, kupanda kwa bei ya umeme na chakula.
Lakini Zitto alisema mfumuko wa bei Tanzania usilinganishwe na takwimu za Kenya na Uganda, akisema hatua za haraka zinahitajika kukabili hali hiyo kwani wanaoteseka ni wananchi.
“Takwimu hizo za mfumuko wa bei zisilinganishwe na za nchi jirani. Wananchi wanateseka zinahitajika hatua za haraka ili kukabiliana na matatizo hayo,” alisema Zitto,” na kuongeza “Sasa kama bei ya chakula inachangia mfumuko wa bei, kwa nini mnawakopesha wakulima wa maua badala ya kuwapa mikopo wakulima wa mazao ya chakula ili wazalishe zaidi na hivyo kupunguza mfumuko wa bei?”Mwenyekiti huyo alisema kuwa wakulima wa maua wamekuwa wakinufaika na mikopo inayosimamiwa na BoT na kuwaacha wakulima wa mazao ya chakula bila msaada hali aliyosema haitasaidia kupunguza tatizo hilo.
“Tutadhibiti vipi mfumuko wa bei kama wakulima wa mazao ya chakula hawawezeshwi ili kuzalisha zaidi?” aliuliza Zitto.
Akijibu hoja hizo, Gavana Ndulu alisema mpango huo wa ukopeshaji kwa wakulima utawanufaisha pia wakulima wa mazao ya chakula.Profesa Ndulu alisema ili kudhibiti mfumuko wa bei, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kupunguza gharama za usafirishaji wa mafuta na kodi.
Alisema kwa kuwa chakula ndicho kinachochangia mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa, wananchi hawana budi kuzalisha zaidi mazao ya chakula.
BoT ianze kuhifadhi dhahabu
POAC pia imeiagiza BoT kuanzisha utaratibu wa kuhifadhi dhahabu kwa ajili ya akiba badala ya kutegemea fedha za kigeni. Agizo hilo la kamati hiyo ya Bunge limekuja baada ya taarifa ya Gavana wa BoT iliyosema kuwa, BoT ina akiba ya Dola za Marekani 3.8 bilioni kwa ajili kukabiliana na tatizo lolote linaloweza kujitokeza.
Makamu Mwenyekiti wa POAC, Deo Filikunjombe alitaka kujua sababu za kuachwa kwa utaratibu wa zamani wa kuhifadhi dhahabu.Profesa Ndulu alisema waliacha kuhifadhi dhahabu kama akiba baada ya bei ya bidhaa hiyo kushuka mara kwa mara.
“Tuliona tunaweza kuhifadhi dhahabu lakini inaposhuka bei katika soko la dunia tulihofia kuwa tunaweza kupata hasara,” alisema Profesa Ndulu.
Hata hivyo, Filikunjombe ambaye ni Mbunge wa Ludewa (CCM) alisema, majibu hayo hayana msingi kwa sababu hata wanaowekeza kwenye masoko ya hisa wanaweza kupata faida na hasara.
“Hata fedha za kigeni kuna wakati kunapotokea mtikisiko wa kiuchumi zinaweza kushuka thamani, hivyo tunawashauri anzisheni mpango wa kuhifadhi dhahabu katika akiba, msihofie hasara, fikirieni pia faida,” alisema.
Alisema hata nchi zilizoendelea duniani zimekuwa zikitunza dhahabu kama akiba yao.
Profesa Ndulu alikubaliana na mawazo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.
Vipi kuhusu mabilioni ya JK?
Katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Bunge Dar es Salaam, POAC pia iliihoji BoT kuhusu awamu ya pili ya mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na Benki za NMB na CRDB, maarufu kama mabilioni ya JK.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Juma Njwayo alisema katika awamu ya pili ya mikopo hiyo, BoT imekuwa ikipitishia katika benki kubwa badala ya kuvitumia vyama vya kuweka na kukopa.
“Kuna utata wa namna fedha hizi zinavyotolewa, kuna usiri. wananchi hawajui wapi watakwenda kukopa. Kwa nini msitumie benki za wananchi na Saccos ambazo ziko karibu na wananchi?,” alihoji Mbunge huyo wa Tandahimba (CCM).“Mtuonyeshe sifa za benki kupata fedha hizo zilikuwa zipi na mlitangaza wapi na lini mlizijulisha benki kuwa mnatoa awamu ya pili ya mabilioni ya JK,” alisema Njwayo.
Gavana Ndulu alisema ataipatia kamati hiyo taarifa ya namna mchakato huo wa kutoa fedha hizo kwa benki na taasisi za fedha ulivyofanyika.POAC pia ilimbana Profesa Ndulu kwa kuwatumia wanasheria kutoka nje katika kesi zinazoihusu BoT, hivyo kutumia mamilioni ya fedha. Akijibu hoja hiyo, Profesa Ndulu alisema BoT ina uhaba wa wanasheria, hali iliyoilazimu kuchukua wanasheria kutoka nje ya ofisi hiyo.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Kamati ya Zitto yambana Gavana BoT
0 comments