NATO leo hii imefanya mashambulizi mengine ya anga katika maeneo ya mji wa Tripoli ikiwa ni siku moja baada ya Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kuwasilini nchini Libya na kuzungumza na kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.
Rais Zuma ambaye anawakilisha kundi la upatanishi la Kanda ya Afrika amefanya mazungumzo na Gaddafi wakati NATO ikisisitiza kwamba utawala wa kikatili wa kiongozi huyo unaelekea ukingoni.
Lakini baadaye Zuma aliwaambia waandishi habari katika mazungumzo yake yaliyorushwa moja kwa moja na televisheni za Libya na Afrika Kusini kwamba Gaddafi yupo tayari kutekeleza mapendekezo yaliyopo katika mpango wa Umoja wa Afrika.
Rais Jacob Zuma wa Afrika KusiniAmesema kuanzia katika kusitisha mapigano ambapo itajumuishwa pia kusimamishwa kwa mashambulizi ya anga yanayofanywa na NATO.
Mpatanishi huyo hakuzungumzia kiini cha mazungumzo hayo yaani "kuondoka kwa Gaddafi" lakini waasi wamerudia kauli yao ya kwamba hawatokubali lolote litakaloendelea kumweka kiongozi huyo madarakani.
Zuma alizungumza huku akinukuu maneno ya Gaddafi akisema " Walibya wote wapate fursa kuzungumza wenyewe kwa wenyewe" ili kuweza kujadili hatima ya nchi yao.
Kwa upande mwingine televishini ya serikali ya Libya imeripoti mashambulizi ya anga ya majeshi ya NATO usiku wa kuamkia leo yaliyolenga maeneo ya Tripoli na vitongoji vya Tajura na Al- Jafra, huko kusini mwa mji mkuu huo.
Ripoti ya televishini ya Jamahiriya, imenukuu vyanzo vya habari vya kijeshi vikisema mashambulizi ya kikoloni yameshambulia maeneo ya kijeshi na kiraia katika miji ya Tripoli na Tajura na kusababisha vifo na uharibifu.
Televisheni hiyo imeripoti kwamba mashambulizi mengine kama hayo pia yamefanywa katika mji wa Al-Jafra ambapo maeneo ya kijeshi na kiraia yameshambuliwa.
Mpatanishi, Jacob Zuma anasema operesheni za NATO zinadhoofisha jitihada zao za upatanishi. Alisema hata ukitaka kwenda nchini Libya utachelewa sana kutokana na mashambulizi hayo.
Amesema hali hiyo imekuwa ikizorotesha kwa kuwa hata ukitaka kuingia nchini humo kwanza lazima uombe kibali cha NATO.
Zuma ambaye aliwasili nchini humo muda mfupi baada ya NATO kuripotiwa kwamba imeshambulia mji wa Zliten, uliyopo mashariki mwa Misrata na kusababisha vifo vya watu 11, amehimiza kusitisha mapigano haraka ili kutoa mwanya wa misaada ya kibinadamu.
Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Nkoana Mashabane alizungumzia suluhu ya mgogoro wa Libya
Wakati huo huo Majenerali watano wa kijeshi wameasi dhidi ya utawala wa Gaddafi na kutorokea nchini Italia. Majenerali hao ambao kwa hivi sasa wapo mjini Roma, wakiwemo makanali wawili na meja wametangaza kuachana na utawala wa Gadhafi.
Aidha wamesema uwezo wa kijeshi wa serikali ya Gaddafi kwa hivi sasa umebaki kama asilimia 20. Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, ambaye alikuwa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Libya kabla ya kubadili mwelekeo wake, amesema maafisa hao ni miongoni mwa wengine 120 walioasi utawala huo katika siku za hivi karibuni.
0 comments